22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Skimu ya umwagiliaji Morogoro yakwama kwa zaidi ya miaka kumi-3

*Wananchi wakata tamaa, wasema ni sawa na ngamia kupenya katika tundu la sindano

Na Ashura Kazinja, Morogoro

WANANCHI zaidi ya 11,000 wa vitongoji vitatu vya Mbuyuni, Rudewa Batini na Gongoni katika kata ya Rudewa wilayani Kilosa mkoani Morogoro matumaini yao ya kupanua kilimo chenye uhakika cha umwagiliaji bado ni kitendawili kufuatia mradi wa skimu ya umwagiliaji katika eneo hilo kukwama kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Skimu hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2010 na taarifa zaidi zinaeleza kuwa imejengwa kwa awamu tatu mpaka sasa na bado hakuna matumaini ya kukamilika ifikapo Septemba 5, kama ilivyo elezwa awali.

Mbali na jitihada mbalimbali za kuiendeleza ikiwemo Serikali kuendelea kutoa fedha, lakini bado matumaini ya wananchi ya kupanua kilimo chenye tija na uhakika cha umwagiliaji yanazidi kuwa kitendawili.

Mradi huo wenye ekari 500 umetumia zaidi ya Sh milioni 700 kujenga banio na mfereji wa mita 180 pekee mpaka mwaka 2012, na kutolewa Sh bilioni saba mwaka 2022 ili kuuendeleza, mradi ambao kama ungekamilika ungemwagilia takribani ekari 3,500, na hivyo kuongeza usalama wa chakula kwa wananchi hao na taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa sheria ya Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na. 4 ya mwaka 2013 inaeleza mambo yanayotarajiwa ikiwemo kuongezeka kwa mchango wa umwagiliaji katika uzalishaji wa chakula na lishe, pamoja na kuongezeka kwa pato la wakulima wamwagiliaji na Taifa kwa ujumla.

Sera ya Kilimo na jitihada za kupunguza umaskini Tanzania inaangalia kuhusu mwenendo vijijini na mchango wake kwenye kupunguza umaskini Tanzania, pamoja na kuongezeka kwa fursa za ajira na kipato kwa vijana kutokana na vivutio katika kilimo cha umwagiliaji, na hivyo kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini.

Ujenzi wa mifereji skimu ya umwagiliaji Rudewa.

Mkoa wa Morogoro una eneo la hekta 2,226,396 linalofaa kwa kilimo na kati ya eneo hilo zaidi ya hekta 862,092 ndizo zinazolimwa kwa sasa sawa na asilimia 39, huku eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji likiwa ni hekta 1,510,339.51, na eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta 40,558 sawa na asilimia tatu, pia mkoa una mito 143 inayotiririsha maji mwaka mzima, pamoja na udongo mzuri na mabonde mengi ambayo bado hayajaendelezwa.

Wananchi wanasemaje

Mkazi wa Rudewa Batini, Amina Athumani anaeleza kuwa haoni matumaini ya skimu hiyo kukamilika Septemba 5, mwaka huu, kutokana na kasi ndogo ya ujenzi huo na kuwaomba wahusika kutumia vyema fedha zilizotolewa na serikali ili kuweza kukamilisha ujenzi wa skimu hiyo kwa wakati.

Vilevile Mkulima na mkazi wa Rudewa Batini, Sheila Kikoti, anasema kwa upande wa kina mama wanaisubiri kwa hamu skimu hiyo ikamilike, ingawa matumaini bado ni madogo, ili iweze kuwakomboa wanawake ambao wengi wao ndio wanafanya kazi mashambani ili kutunza familia zao.

“Sisi kina mama tunatamani sana skimu hii ikamilike kama ilivyopangwa, itatukomboa kwani wengi wetu ndio tunalima mashambani ili kutunza familia, wengine wajane, wengine tunale watoto peke yetu (wazazi pweke) lakini hata wenye waume wengine ndio wanategemewa kutunza familia, baba unamkuta yupo yupo tu,” anaeleza Sheila.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Rudewa Batini, Hamadi Maboga, akisikitishwa na kusuasua kwa skimu hiyo, anasema kuwa skimu hiyo ni muhimu kwa wananchi ili kuweza kulima kilimo chenye tija na kuweza kujipatia kipato kitakacho wafanya waweze kuchangia kazi mbalimbali za maendeleo kijijini hapo kama vile ujenzi wa zahanati na shule.

Aidha, Maboga ameiomba Serikali kukiangalia kijiji cha Rudewa Batini kwa jicho la tatu, na kuhakikisha utakapokamilika mradi huo inapatikana mbinu mbadala ya kuwapelekea mfereji katika kitongoji cha Peapea, ambalo ndilo bonde kubwa linalotegemewa katika kijiji hicho.

Mwenyekiti Kamati ya Ujenzi

Naye, Mwenyekiti Kamati ya ujenzi skimu ya umwagiliaji Rudewa, Mahmudu Limbembembe, anasema skimu hiyo ilianza kujengwa mwaka 2010, na kwamba ilifanikiwa kujengwa kwa awamu mbili ya banio na mfereji wa mita 180 kwa Sh milioni 700.

Anasema baada ya Serikali kutoa fedha za ujenzi kwa awamu ya tatu kiasi cha Sh bilioni tisa, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilimtafuta Mkandarasi aliyekubali kuendeleza ujenzi kwa sh. bilioni saba, na alikabidhiwa kazi hiyo Septemba 5, mwaka 2022, huku akitakiwa Septemba 5, 2023 akabidhi mradi ukiwa umekamilika kwa kutengeneza miundombinu ikiwemo ya mfereji mdogo na mkubwa.

“Kwa isivyobahati huyu mkandarasi ni mbabaishaji, kasi yake ni ya taratibu mno, kwa kuthibitisha kuwa ni mbabaishaji huyu Meneja mradi aliyepo ni wa nne kwa kipindi cha miezi saba, kila mmoja akija kabla ya kujipanga anabadilishwa, na hatutafikia lengo la taifa tulilomuwekea la Septemba 5, mwaka huu kuweza kukabidhi kazi, hataweza kukamilisha,” anasema Limbembembe.

Limbembembe anaeleza kuwa baada ya kamati ya ujenzi kuona mkandarasi ni mbabaishaji walimuita, na Mei 12, mwaka huu alifika, na wakamwambia kuwa huo ni mradi mkakati wa mwaka mmoja, lakinikasi yake ni ndogo sana kama ya mtoto anaetaka  kutambaa na kwamba hataweza kumaliza kwa muda uliowekwa, lakini mkandarasi akatoa ahadi ya kutengeneza kila siku mita 45 na kuongeza watumishi, lakini hakufanya hivyo.

“Tatizo ni utendaji kazi wa kampuni, jinsi wanavyofanya kazi, hawajajipanga vizuri kiufanyaji kazi, wanakuwa wanashtukiza, mpaka leo mimi mwenyewe ninae simamia kamati ya ujenzi ratiba yao ya kazi sijapewa, alisema kutakuwa na dabo shifti ambazo watu watafanya kazi usiku na mchana, alisema ujenzi wa mfereji wa mita 500 kwa kila siku atajenga mita 45, lakini mpaka leo hakuna hata siku moja ambapo amejenga hata mita 20 kwa siku, anaishia kumi au kumi na tano.

“Tayari hatua za mwanzo zimeshachukuliwa na mkandarasi mshauri ya kumuandikia barua ya onyo projekti meneja kwamba kazi yake anafanya taratibu sana, sasa hivi ujenzi haujafikia hata asilimia 33, wakati alitakiwa kwa sasa awe asilimia 80 ya ujenzi,” anasema Limbembembe.

Katibu Skimu

Katibu Skimu ya umwagiliaji Rudewa, Kasimu Mhina, anaeleza kuwa mradi huo unasua sua na hauna matumaini ya kumalizika, na kwamba toka ulipoanza kujengwa ni miaka 13 sasa, baada ya kujengewa banio na kukamilika mwaka 2010, walitegemea kupata mfereji kwa wakati lakini mwaka 2010 walipata fedha ya kuendeleza mfereji, hata hivyo ulijengwa mfereji wa mita 181 pekee, na mwaka 2012 mradi ulisimama mpaka ulipofufuka tena mwaka 2022.

Anasema tumaini la wananchi lilikuwa ni kunufaika kiuchumi kwa kujipatia kipato kwa kulima kilimo chenye tija cha umwagiliaji na kwa wakati wote, tofauti na sasa ambapo wanategemea mvua isiyokuwa ya uhakika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Mpaka sasa tungekuwa na kilimo cha uhakika, tungebadilika sana katika kilimo hasa cha kutegemea mvua, kilimo cha kutegemea mifereji ni cha uhakika na ni kipindi chote tungekuwa tunalima na kujipatia mazao, hata uchumi acha wa mtu mmoja mmoja, bali kuanzia kata, wilaya hadi taifa ungeongezeka, watu wa ushuru wangekata ushuru fedha zingeweza kupatikana,” anasema Mhina.

Chama Cha Mapinduzi

Kwa upande wake Mwenyekit Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Rudewa, Abdallah Kiemka anasema changamoto iliyopo ni mradi kusuasua na kwamba kitu kinacho leta ugumu  ni aina ya utendaji na uwajibikaji wa mradi huo, na kwamba wanaosimamia mradi huo sio wazalendo.

“Kusema kweli kama mwenyekiti sehemu iliyonikwaza na nashindwa kuitolea majibu ipasavyo ni swala la mradi wa banio, tunataka tupate muhtasari wa kupeleka ngazi za juu kulalamikia udhaifu wa ule mradi, yaani hakuna majibu, kwa mradi ulipo pale hauwezi kusema utaisha mwezi wa tisa, ni sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano, niseme inauma sana hususani kwa wananchi wa Rudewa na viongozi tuliokuwa na dhamana,” anasema Kiemka.

Diwani

Diwani kata ya Rudewa, Subiri Joseph Mwamalili, anasema sababu za kukwama kwa mradi huo kwa zaidi ya miaka kumi inawezekana kuwa  ni kukosa msukumo kutoka kwa viongozi wa kipindi hicho.

Tume ya Umwagiliaji

Awali akizungumzia mradi huo Mkurugenzi Tume ya Umwagiliaji mkoani Morogoro, Elibariki Mwendo, anasema mradi huo unajengwa kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni banio, ya pili kuchimba mfereji, anasema shilingi mil. 320 zilitumika kuchimba mfereji wenye urefu wa mita 180 huku shilingi mil.520 zikitumika kujenga banio.

“Hela ikipatikana wanajenga kidogokidogo, sio kama walikuwa na hela za kufanya kila kitu na kukamilisha hapana, Sh milioni 520 walijenga banio, na Sh milioni 320 wakajenga mfereji wa mita 180 ikaishia hapo, kwahiyo toka hapo kuendelea mbele ikawa hela hiyo hamna.

“Mradi haukukwama, ni hela tu zilikuwa kidogo tukafanya kile kinachowezekana kutokana na upatikanaji wa fedha, na huko nyuma miradi ilikuwa inafanywa kutokana na fedha iliyopo, hii ni awamu yake ya tatu,” anasema Mwendo.

Anasema skimu hiyo inajengwa na Kampuni ya C0MFIX & Engineering LTD ya Dar es salaam na kwamba imefikia asilimia 25 ya ujenzi wake, na kuwa inatarajiwa kukamilika Septemba 5, mwaka huu, kutokana na mkataba na fedha iliyotolewa na serikali kwa awamu ya tatu ya Sh bilioni saba.

Hata hivyo, siyo vyema kwa miradi muhimu kama huu wa skimu ya umwagiliaji unaotegmewa na wananchi na taifa kwa ujumla, kuchukua muda mrefu wa zaidi ya miaka kumi na mbili bila kukamilika, kwani inaweza kutoa mianya ya ubadhirifu, pia mamlaka husika ihakikishe inafanya kazi yake vyema ili kukamilisha skimu hiyo kwa wakati uliowekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles