25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Khadija: Ulemavu sio sababu ya kushindwa kumlea mtoto wako

Na Patricia Kimelemeta

“ULEMAVU sio sababu ya kushindwa kumlea mtoto wako,” hayo ni maneno ya Khadija Abdalah (43) mlemavu wa miguu mkazi wa Mbagala Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Khadija ni ombaomba anayependa kukaa maeneo tofauti yakiwamoKmtaa wa kisutu na Lumumba Manispaa ya Ilala, ana mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu ambaye amekua akiongozana nae kila siku asubuhi kuelekea kwenye shughuli zake za kuomba omba huku akiwa amembeba mwanae na kuendeshwa kwenye kitimwendo.

“Mimi ni mlemavu wa miguu, nilipata ugonjwa wa polio nikiwa na umri wa miaka miwili kijijini kwetu Njinjo mkoani Lindi, wakati huo hakuna matibabu wala chanjo zaidi ya familia kuamini kuwa ugonjwa wa polio unatokana na imani za kishirika kwamba nililogwa na ndugu zangu na kusababisha kupata ulemavu.

“Hali hiyo iliwafanya wazazi wangu kuangaika kwa waganga wa tiba asili ili waweze kunitibia lakini ilishindikana badala yake nimebaki kwenye ulemavu mpaka leo,” anasema Khadija.

Ameongeza kuwa, tangu kipindi hicho hakubahatika kusoma wala kujishughulisha na shughuli yoyote mpaka wazazi wake walipofariki na maisha kuwa magumu, jambo ambalo lilimlazimu kutoka kijijini kwao na kuja Dar es Salaam na kuanza kuomba msaada kutoka kwa watu mbalimbali ambapo alibahatika kupatiwa kitimwendo ambacho amekua akikitumia mpaka leo.

Anasema, mwaka 2020 alibeba ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume lakini baba wa mtoto huyo alimkimbia na kumuacha peke yake.

“Sasa hivi mwanangu ana umri wa miaka mitatu na miezi minane, kila siku asubuhi nikitoka nyumbani nambeba na kuja nae katikati ya jiji kwa ajili ya kuomba msaada kwa wasamaria wema ili waweze kunisaidia, nashukuru, Mungu hamtupi mja wake, napata hela ya kula japo si kiasi kikubwa lakini ninachokipata kinanisaidia kumnunulia nguo mwanangu na kumudu gharama za maisha za hapa na pale,” anasema Khadija.

Anaongeza kuwa, licha ya kuishi kwenye mazingira magumu, lakini ulemavu wake haumfanyi kushindwa kumlea mwanae au kumpatia huduma zote za kimaisha, kwa sababu inapofika wakati wakumpeleka kwenye chanjo amekua akianzia hospitali na kumpatia mwanae chanjo halafu anakuja mjini kwa ajili ya kuomba.

Siyo hivyo tu, bali hata mwanae anapougua amekua na utaratibu wa kumpeleka hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu na hajawahi kupanga foleni kama walivyo wagonjwa wengine au wazazi wanaowapeleka watoto wao hospitali, badala yake madaktari na wauguzi wamekuwa wakimsikiliza na kumpatia matibabu mapema na kuondoka.

“Ulemavu sio sababu ya kushindwa kumlea mwanangu, napambana nae kila kukicha, asubuhi natoka nae nyumbani, nakuja nae mjini, jioni naondoka nae, nikifika huku, naweka oda ya chakula kwa ajili ya mwanangu kwa mama lishe anakula kadri ya uwezo wangu na maisha yanaendelea,” anasema Khadija.

Khadija anasema kuwa anampenda mwanae kwa sababu anaamini ndiyo ndugu yake na kwamba akifika umri wa kwenda shule atampeleka ili aweze kujiendeleza kielimu.

“Mimi sikusoma, ila nataka mwanangu asome, yeye ndo ndugu yangu naamini akikua ataweza kunisaidia na huu ulemavu wangu, nampenda sana mwanangu,” anasema.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaomfahamu, Khadija wanamuelezea kuwa amekuwa akifika maeneo hayo na mwanae huku akiwa kwenye kitimwendo ambacho kimewekewa mwamvuli kwa ajili ya kumkinga na jua.

“Khadija tumemzoea, mara kwa mara kwa mara anakuja na mwanae huku akiwa amembeba na kumficha kwenye mwamvuli, anaombaomba na ikifika jioni anaondoka, siku nyingine usipomuona maeneo haya ujue yupo mtaa wa kisutu, anaomba na kuondoka, amekua akitutuma kumnunulia chakula na kumsaidia kumsafisha mwanae pale anapochafuka na wala hakuna anayemkatalia kwa sababu hali yake tunaijua,” anasema Amina Yusuph mfanyabiashara katika eneo la Lumumba.

Nae, Jumanne Idd anasema kuwa, Khadija ni omba omba anayefika mtaani hapo akiwa na mwanae, lakini hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kumfanyia vitendo vya ukatili sio yeye wala mtoto wake.

“Khadija ni dada yetu, tupo nae hapa muda mrefu, kila siku anakuja na mwanae, hakuna mtu aliyewahi kumfanyia ukatili kwa sababu ya ulemavu wake, kwanza ni mjanja, hajachukulia ulemavu wake kuwa sababu ya kuwa tegemezi hata kama anaomba lakini anaamka asubuhi na kuja mjini kujitafutia kipato,” anasema Idd.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha anasema, mtoto wa Khadija ana umri wa miaka mitatu na miezi nane, ambapo yupo kwenye utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ambayo inaanzia umri sifuri hadi miaka minane.

Anasema utekelezaji wa mpango huo ulizinduliwa rasmi Mwaka 2021 hadi 2026 ambao unatekelezwa katika afua tano za afya, lishe, elimu, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama.

“Mtoto wa Khadija ana umri wa miaka mitatu, bado anahitaji malezi ya wazazi wote wawili, ana haki ya kupata huduma za afya ikiwamo chanjo na mambo mengine, kupata lishe bora, malezi ya jamii husika iwe ndugu, jamaa au wanajamii katika mtaa na kupata fursa ya kujifunza kulingana na umri wake, lakini pia anahitaji ulinzi na usalama,” anasema Nyamara.

Anaongeza kuwa, Serikali ya mkoa imekua na utaratibu wa kuwatumia maofisa ustawi wa jamii waliopo kwenye kata kwa kushirikiana na watendaji wa mtaa kwa ajili ya kuangalia mahitaji ya watoto pamoja na malezi yao, ushiriki wa jamii katika malezi pamoja na ulinzi na usalama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kaya Foundation ambayo inajishughulisha na watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, Anapili Ngome anasema kuwa, walemavu wanahitaji msaada wa karibu ili waweze kujiendeleza.

Amesema kuwa, taasisi yake imekua ikitoa msaada kwa walemavu kwa kuwapatia vitimwendo pamoja na kuwaunganisha na wadau mbalimbali ili waweze kupata ufadhiri wa masomo na mahitaji mengineyo.

“Nimekua nikitoa msaada mbalimbali kwa walemavu, wengine nawaunganisha na serikali ili waweze kupata ufadhiri wa masomo au vitimwendo jambo ambalo litawasaidia kujiendeleza kielimu,” anasema Ngome.

Anapili anasema, Taasisi hiyo imekua ikiwachukua watoto wenye ulemavu wenye vichwa vikubwa kwa ajili ya kuwatafutia wafadhiri ili waweze kupata msaada wa matibabu.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Kitengo cha walemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Joyce Maongezi anaesema kuwa, Serikali ipo kwenye mchakato wa kufanya marekebisho ya Sera ya watu wenye ulemavu ya Mwaka 2004 pamoja na Sera ya Mtoto ya Mwaka 2004 na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Anasema, sera hiyo itaweza kutengeneza mfumo rafiki ili walemavu waweze kujishughulisha na kazi mbalimbali zinazojitokeza nchini kama walivyo wananchi wengine wasio na ulemavu na kupata haki sawa.

“Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na asilimia mbili ya watu wenye ulemavu, ripoti ya sensa ya mwaka 2022 inayohusu taarifa za walemavu bado haijatolewa, hivyo basi tunaamini idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na viashiria mbalimbali ikiwamo ya kukua kwa teknolojia pamoja na ongezeko la ajali zinazotokana na vyombo vya usafiri ikiwamo magari na pikipiki.

“Tumekuwa tukishirikiana na madaktari kutoka hospitali mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchukua taarifa za watu waliopata ajali za barabarani na wengine kupata ulemavu Kutokana na ajali hizo na taarifa hizo tunaziwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kuziunganisha Ili Serikali iweze kuchukua hatua,” anasema Maongezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles