29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Meneja wa TANROADS Kigoma atakiwa kukamilisha barabara ya Kasulu – Manyovu

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amemtaka Meneja wa Wakala Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Kigoma kuhakikisha barabara ya Kasulu-Buhigwe- Manyovu yenye urefu wa kilomita 56 Sehemu ya Kasulu hadi Buhigwe KM 35 inakamilika kwa kiwango cha lami ifikapo Oktoba, mwaka huu.

Waziri Mbarawa ametoa agozo hilo juzi ambapo barabara hiyo ambayo ni sehemu ya Barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Kilomita 260. 6 inatarajiwa kuufungua na kuunganisha mkoa wa Kigoma na Kagera kwa barabara ya lami na hivyo kuchochea shughuli za kilimo, biashara na uwezekezaji katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania.

“Hakikisheni TANROADS Kigoma na TANROADS Makao Makuu mnakagua miraid hii mara kwa mara ili kufahamu changamoto za wakandarasi na kuzipatia ufumbuzi wa haraka kabla ya msimu wa mvua kuanza,” amesema Profesa Mbarawa.

Ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo katika sehemu ya Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Kilomita 56 na Mvugwe hadi Nduta Junction yenye urefu wa kilomita 59.35 na Nduta Junction-Kibondo Junction hadi Kabingo yenye urefu wa kilomita 62.5 ambayo kasi ya ujenzi wake inaridhisha na kumuonya Mkandarasi anayejenga sehemu ya Kanyani Junction hadi Mvungwe yenye urefu wa Kilomita 70.5 ambaye bado yuko nyuma ya muda.

“Serikali imedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara zake zote ili kuimarisha shughuli za biashara, kilimo na usalama hivyo haitamvumilia Mkandarasi anayefanya kazi nje ya mkataba kwa kuwa lengo la Serikali ni kuwahakikishia wananchi wake wanapata huduma bora kwa wakati ‘amesisitiza.

Aidha, amewataka wakazi wa Kigoma na mwambao wa Ziwa Tanganyika kutumia uwekezaji wa miundombinu kuibua fursa za biashara na maendeleo ili kupunguza umasikini.

Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua barabara ya Chankere hadi Mwamgongo katika Jimbo la Kigoma Kaskazini ambayo inapita kwenye mlima mkali na maeneo yenye uzalishaji wa mazao ya biashara na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuzingaia alama za barabarani na kujenga nje ya hifadhi ya barabara ili kuepuka usumbufu na kulinda usalama.

“TANROADS hakikisheni ujenzi huu unaofanywa hauathiri wananchi pindi utakapokamilika na barabara kuanza kutumia’ amesema Prof. Mbarawa.

Nae Meneja TANROADS Kigoma, Mhandisi Narcis Choma amesema wamejipanga kuhakikisha wakandarasi wote wanne wanaojenga barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu KM 260.6 wanasimamiwa kikamilifu na hakutaongezwa muda kwa mkandarasi atakayezembea na kushindwa kumaliza kazi kwa wakati.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa namna inavyosimamia ujenzi wa barabara mkoani Kigoma na kuahidi ushirikiano mkubwa kwa wakandarasi ili watimize majukumu yao kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Profesa Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Kigoma ya kukagua miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege na Bandari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles