31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Skimu ya umwagiliaji Morogoro yakwama kwa zaidi ya miaka 10

*Milioni 700 zazama

*Yaathiri ndoto za wakulima kufikia kilimo chenye tija

Na Ashura Kazinja, Morogoro

WANANCHI zaidi ya 11,000 wa vitongoji vitatu vya Mbuyuni, Rudewa Batini na Gongoni katika kata ya Rudewa wilayani Kilosa mkoani Morogoro matumaini yao ya kupanua kilimo chenye uhakika cha umwagiliaji bado ni kitendawili kufuatia mradi wa skimu ya umwagiliaji katika eneo hilo kukwama kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Mradi huo wenye ekari 500 umetumia zaidi ya Sh milioni 700, na ulianza kujengwa toka mwaka 2010 ambapo ulifanikiwa kujenga banio na mfereji wa mita 180 pekee, mradi ambao kama ungekamilika ungemwagilia takribani ekari 3,500 na hivyo kuongeza usalama wa chakula kwa wakazi wake.

Mfereji wa asili Rudewa Mbuyuni.

Kwa mujibu wa sheria ya Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na.4 ya mwaka 2013 inaeleza mambo yanayotarajiwa ikiwemo kuongezeka kwa mchango wa umwagiliaji katika uzalishaji wa chakula na lishe, pamoja na kuongezeka kwa pato la wakulima wamwagiliaji na Taifa kwa ujumla.

Pia Sera ya Kilimo na jitihada za kupunguza umasikini Tanzania inaangalia kuhusu mwenendo vijijini na mchango wake kwenye kupunguza umasikini Tanzania, vilevile kuongezeka kwa fursa za ajira na kipato kwa vijana kutokana na vivutio katika kilimo cha umwagiliaji na hivyo kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini.

Mkoa wa Morogoro una eneo la hekta 2,226,396 linalofaa kwa kilimo na kati ya eneo hilo zaidi ya hekta 862,092 ndizo zinazolimwa kwa sasa sawa na asilimia 39, huku eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji likiwa ni hekta 1,510,339.51, na eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni hekta 40,558 sawa na asilimia tatu, pia mkoa una mito 143 inayotiririsha maji mwaka mzima, pamoja na udongo mzuri na mabonde mengi ambayo bado hayajaendelezwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Rudewa, Batini Hamadi Maboga, anasema kuwa kukwama kwa mradi huo kwa muda mrefu kumepelekea changamoto mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi na uhaba wa chakula hususani mchele ambao umepanda bei kutoka Sh 1,200 mpaka 3,000 kwa kilo moja, hali ambayo haijawahi kutokea kwa miaka ya nyuma.

“Sababu ya kukwama kwa mradi huu kwa kweli ni mambo ya kiserikali, huu mradi tunaogopa kuuzungumzia sana kiundani, ni kweli mradi ni wa muda mrefu na umesuasua kwa muda mrefu sana, mpaka watu tulipatwa na hofu kuwa mto unaweza kuhama ukaleta athari kwenye kijiji chetu,” anaeleza Maboga.

Maboga anasema kuwa kwa sasa wao kama viongozi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuchangisha michango mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao kutokana na hali ya uchumi ya wananchi kuwa ngumu kwani hata fedha za kujikimu wao wenyewe hawana.

Anaongeza kuwa mbali na mradi huo kupita katika kijiji chake lakini wao sio wanufaika wa mradi huo kutokana na kukosa eneo kubwa la kilimo, na kwamba mradi huo ulilenga kijiji cha Mbuyuni ambako baadhi ya wananchi wa Rudewa Batini wana mashamba pia.

“Lakini mfereji huu asilimia kubwa umeelekezwa katika kijiji cha Mbuyuni, Mfereji huu wangeupeleka Tembeni ambako kuna mashamba makubwa ya mpunga wangetusaidia sana, wale wataalamu waliokuja walishindwa kutegea juu,” ameongeza.

Hata hivyo ameiomba serikali kukiangalia kijiji cha Rudewa Batini kwa jicho la tatu na kuhakikisha inapatikana mbinu mbadala ya kuwapelekea mfereji katika kijiji cha Tembeni kitongoji cha Peapea ambalo ndilo bonde kubwa linalotegemewa katika kijiji hicho, pamoja na wakulima waliolima kuzunguka banio kufikiriwa, kwani ili wanufaike inawalazimu kununua mashamba Mbuyuni.

Nae, Mkulima na mkazi wa Rudewa Batini, Mohamed Mtalame (Mzee Mobutu) anaeleza kuwa kutokamilika kwa wakati kwa skimu ya umwagiliaji kijijini hapo imewafanya kuishi maisha magumu kwa muda mrefu huku wakiwa hawajui hatima ya maisha yao kiuchumi, chakula na hata namna ya kutunza familia zao kutokana na kilimo wanachokitegemea kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

“Mwaka jana tulikosa kabisa tunategemea mvua lakini mvua yenyewe hakuna haieleweki, bei ya chakula iko juu, mchele madukani hakuna wa 1200 wala 2000, bei ni kuanzia 3000 kwa kilo, mahindi nayo hali ni mbaya, bei yake haijawahi kutokea, lakini kungekuwa na skimu ya umwagiliaji sasa hivi mambo yangekuwa mazuri watu wangeweza kuvuna mara mbili au tatu kwa mwaka.

“Tunahitaji skimu, kwani sisi huku Peapea, Tembeni kutokea Mgombelenga hali ya mchele sio nzuri, gunia la mpunga kwa sasa laki mbili na nusu wakati zamani liliuzwa Sh 60,000  hadi 70,000, je mtu kama mimi na umri nilionao naipata wapi hiyo hela, hapo kweli mtu utakula mchele,” anasema Mobutu.

Miundombinu ya mfereji wa skimu ya umwagiliaji Rudewa.

Mobutu anasema kuwa vijana wengi kijijini hapo wanahangaika na maisha huku wengine wakibaki nyumbani na wazee kutokana na kukosa kazi za kufanya mashambani, na kwamba hata vibarua imekuwa ngumu kwao kupata kutokana na hali ya kiuchumi kwa wananchi kuwa ngumu.

“Vijana wanahangaika sana hakuna vibarua, nani akupe kibarua wakati yeye mwenyewe hajapata, tunateseka sana hali ya mazao imekuwa ngumu, kungekuwa na skimu ya umwagiliaji mtu angeweza kujitahidi na vijana wengi wangepata kazi.

“Hii skimu zaidi ya miaka 12 imeshindikana, hapa Batini hatuna hata mifereji ya asili, mifereji iliyotokea zamani ya Katema na Salama ndio iliyopo huko chini, lakini sisi hapa hatuna mpaka uweke pampu, hata tukija na pampu tunadaiwa Sh 50,000 kwa mwezi, wengine wamepoteza pampu zao wamenyang’anywa kwa kushindwa kulipia.

“Tunaiomba serikali kama inatuelewa banio lingetokea juu kabisa, mradi upite karibu na shamba la Msimba ili watu wa Peapea mpaka Mgombelenga wanufaike pia” ameshauri Mobutu.

Nae Mkulima na mkazi wa Rudewa Batini, Yunus Kasim, anaeleza kuwa mradi huo unasemekana ulikuwa na awamu tatu, na kwamba bajeti iliyotolewa ya takribani Sh milioni 700 ilikuwa ni kwa ajili ya banio na mfereji wa mita 180.

“Huu mradi ulipitishwa katika vikao vya vijiji, wakati mradi umetekelezwa kwa awamu ya kwanza wananchi walikuwa wanategemea utekelezwe kwa awamu ya pili, sasa hiyo awamu ya pili iliyokuwa inategemewa kuchukua mfereji kuanzia hapa ulipoishia mpaka huko Mbuyuni ulikuwa bado ukawa umesimama, hata sisi wananchi tukawa hatuelewi tatizo ni serikali au nini.

“Lakini kwa kumbukumbu zangu mimi ninachokiona kilichofanyika na thamani ya pesa iliyotengwa kwangu mimi ni sawa, changamoto kubwa ilikuwa ni serikali kutimiza kwa awamu ya pili, sasa pale ndio tulishindwa kuelewa changamoto ni nini hasa.

“Na kitu kikubwa ni kwamba mradi ulichelewa haukufanyika kwa wakati, kwahiyo ni sawasawa na hela ya serikali ilipotea bila faida kwa sababu mradi intevo yake ni kubwa, mradi kama huu kuchukua miaka kumi ni changamoto,” anaeleza Yunus.

Hata hivyo, anasema wananchi wa Rudewa wanamuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya kilimo kuwafikiria kwani skimu moja ya umwagiliaji hata ikikamilika haitoshi, na kwamba Rudewa ni sehemu ya uchumi katika wilaya ya Kilosa, na sehemu kubwa wanategemea kilimo hususan vijana.

Vilevile Mkulima na mkazi wa Rudewa Batini, Shani Mohamed, anaeleza kuwa wameathiriwa kwa kiasi kikubwa kwa kukosa skimu ya umwagiliaji, kwani mazao yao yanakauka kwa jua na kwamba wengi wao hawana uwezo wa kutumia mashine (Pampu) na hivyo kipato kutopatikana kama inavyotakiwa.

Mkulima na mkazi wa Rudewa Batini, Salma Maboga, anasema athari wanayoipata kwa kukosa skimu ya umwagiliaji ni uchache wa mazao na uhaba wa chakula ambapo kwa sasa wamekumbwa na baa la njaa baada ya vyakula kama nchele na unga kupanda bei.

Diwani Kata ya Rudewa, Subiri Joseph Mwamalili akiwa katika mashamba ya mpunga ya Mbuyuni.

Hata hivyo, Diwani kata ya Rudewa, Subiri Joseph Mwamalili, anasema sababu za kukwama kwa mradi huo inawezekana kuwa ilikuwa ni sapoti ndogo na kukosa msukumo kutoka kwa viongozi wa kipindi hicho, na kwamba ili kujua kama gharama iliyotumika inaendana na ujenzi uliofanyika ni lazima uwe mtaalamu na sio kuangalia kwa macho.

Anaeleza kuwa mradi huo ulianza toka mwaka 2010, banio lake lilijengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 500, na kwamba ilipofika mwaka 2014 kwenda 2015 ndipo ulijengwa mfereji wa mita 180 badala ya mita 250 baada ya kutolewa Sh milioni 350.

“Lile banio lilijengwa toka mwaka 2010, sisi wenyewe hatukuwa katika uongozi, lakini taarifa tulizonazo lilijengwa kwa Sh milioni 500, lakini baadae 2014 kwenda 2015 ndio ukajengwa ule mfereji, fedha zilitoka Sh milioni 350, ilionekana kwamba utajengwa mfereji wenye urefu wa mita 250 kwa thamani ya fedha zile, lakini baadae ikapungua na kujenga zile chemba mita 180 kwa Sh milioni 329 na zilizobaki kukarabati banio,” anafafanua Mwamalili.

Hata hivyo, anasema mradi huo lengo lake ni kunufaisha kijiji cha Rudewa Mbuyuni na sio Batini, na kwamba maelfu ya wakazi wa Batini wanamashamba huko, ambako wanatumia mifereji ya asili (kienyeji) kumwagilia mashamba yao ambao unahudumu hekta zaidi ya 2,000, na kwamba kama mradi utakamilika utahudumu hekta zaidi ya 3,500.

Aidha, anasema kama skimu ikikamilika wataweza kuvuna gunia zaidi ya 30 kwa ekari moja tofauti na sasa gunia 10-15, hivyo kuondoa kabisa hali mbaya ya chakula na uchumi inayowakabili wananchi wa kata yake.

Akizungumzia mradi huo Mkurugenzi Tume ya umwagiliaji mkoani Morogoro, Elibariki Mwendo, anasema mradi huo haukukwama na kwamba taratibu zote za ujenzi zilifuatwa, bali unajengwa kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni banio, ya pili kuchimba mfereji, anasema Sh milioni 320 zilitumika kuchimba mfereji wenye urefu wa mita 180 huku Sh milioni 520 zikitumika kujenga banio.

“Ule mradi hela ikipatikana wanajenga kidogokidogo, sio kama walikuwa na hela za kufanya kila kitu na kukamilisha hapana, Sh milioni 520 walijenga banio, na Sh milioni 320 wakajenga mfereji wa mita 180 ikaishia hapo, kwahiyo toka hapo kuendelea mbele ikawa hela hiyo hamna,” anaeleza Mwendo.

“Mradi haukukwama wala nini, ni hela tu zilikuwa kidogo tukafanya kile kinachowezekana kutokana na upatikanaji wa fedha, na huko nyuma miradi ilikuwa inafanywa kutokana na fedha iliyopo, hii ni awamu yake ya tatu,” anasema Elibariki.

Mwendo anasema skimu hiyo ambayo mwajiri wake ni Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inajengwa na Kampuni ya C0MFIX & Engeneering LTD ya Dar es salaam na kwamba imefikia asilimia 25 ya ujenzi wake, na kuwa inatarajiwa kukamilika Septemba 5, mwaka huu.

Aidha, anasema kuwa kwa sasa mradi huo utajengwa na kukamilika bila tatizo kutokana na mkataba na fedha iliyotolewa kwa awamu hii ya tatu ya shilingi bilioni saba, na kwamba kuna baadhi ya mashamba yatajengewa banio (intake) lingine.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamndu Shaka, hakutaka kuzungumzia zaidi swala hilo na hali ya wananchi wa kata ya Rudewa kwa ujumla, huku akitoa ahadi ya kufatilia nini hasa kilitokea.

Hata hivyo, miundo mbinu ya banio na mfereji imechakaa sana, kwani miaka kumi na mbili ni mingi hivyo inahitaji ukarabati ambao nao utagharimu fedha za umma, hivyo ni vyema serikali ikahakikisha miradi mikubwa kama skimu za umwagiliaji zinajengwa na kukamilika kwa wakati kuepusha matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya fedha za umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles