24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA KUJIULIZA KWA NDANDA LEO

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo watakuwa na kibarua kizito watakaposhuka dimbani kusaka pointi muhimu dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ili waweze kupunguza tofauti ya pointi iliyopo kati yao na vinara, Simba.

Kwa sasa Yanga imejikusanyia pointi 37, huku Simba wakiongoza usukani kwa kufikisha pointi 41, zote zikiwa zimecheza mara 17.

Yanga itavaana na Ndanda katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku ikiwa na kumbukumbu ya kubanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza wa ligi uliopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Yanga, iliyopania kutetea ubingwa wake msimu huu kwa mara ya tatu mfululizo, itaingia uwanjani ikiwa na uchu wa kusaka mabao ili kulipiza kisasi cha kutoka suluhu katika mchezo wa awali dhidi ya Ndanda, pamoja na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na African Lyon katika mchezo uliopita.

Kocha wa Yanga, George Lwandamina, ambaye alishinda mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu na kutoka sare katika mchezo uliofuata kwenye duru la pili, leo atalazimika kupanga kikosi cha mauaji baada ya kurejea dimbani kwa mshambuliaji Donald Ngoma, aliyekosa mchezo uliopita kutokana na adhabu ya kadi tatu za njano.

Ikiwa Wanajangwani hao watakosa ushindi wa pointi tatu katika mchezo wa leo, watazidi kupunguza kasi ya kutetea ubingwa wao msimu huu na kuendelea kuwarahisishia kazi mahasimu wao, Simba ambao kikosi chao kimeonekana kuwa tishio Ligi Kuu.

Wapinzani wao, Ndanda wataingia uwanjani wakiwa na machungu ya kupoteza michezo miwili mfululizo waliyocheza katika mzunguko wa pili, ambapo walichapwa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika uwanja wao wa nyumbani, kabla ya kupata kipigo kingine kama hicho walipovaana na Mtibwa Sugar.
Akizungumzia mchezo wa leo, Ofisa Habari wa klabu ya Ndanda, Idrissa Bandari, alisema wana  hasira ya kupoteza michezo miwili mfululizo, hivyo watahakikisha wanapata pointi tatu muhimu ili kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.

Kikosi cha Ndanda kinashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kujikusanyia pointi 19, sawa na Mbao FC na African Lyon, zikiwa zimetofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Bandari alisema wanafahamu kuna changamoto za kupata ushindi wanapocheza ugenini, lakini hilo haliwapi hofu yoyote, kwani watapambana ili waweze kupata matokeo mazuri na kurudisha matumaini kwa mashabiki wao.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Manungu, Morogoro, ambapo timu ya Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa Majimaji FC ya Songea.

Mtibwa, ambayo imejikusanyia pointi 27 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, imepania kuibuka na ushindi nyumbani ili iweze kupanda hadi nafasi ya tatu na kuishusha Kagera Sugar, yenye pointi 28.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles