31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Benjamin Mkapa yadhamiria kufuta sifuri matokeo kidato cha nne, sita

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa inajivunia kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma kwa mitihani ya kidato cha nne na sita huku ikidhamiria kufuta daraja sifuri.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1998 ina wanafunzi 1,669 wakiwemo 148 wenye ulemavu wa viungo, ualbino, wasioona na viziwi.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 24 ya kidato cha sita Mkuu wa shule hiyo, Joseph Deo, amesema maendeleo ya kitaaluma ni mazuri kwani katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2023 ilifanikiwa kupata wanafunzi 117 wenye ufaulu wa daraja la kwanza.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Joseph Deo, akizungumza wakati wa mahafali ya 24 ya kidato cha sita.

Amesema matokeo ya kidato cha sita mwaka 2021 ufaulu ulikuwa asilimia 100, mwaka 2022 asilimia 99 na mwaka 2023 asilimia 99.

“Tunaamini kwa jitihada za walimu na wanafunzi mwaka huu wa 2024 tutaondoa daraja sifuri ikiwezekana kupata daraja la kwanza 150 au zaidi…tunaweza,” amesema Deo.

Mkuu huyo wa shule amesema pia wamefanikiwa kufanya ukarabati wa miundombinu iliyokuwa imechakaa ikiwemo milango 48 ya vyoo vya walimu na wanafunzi pamoja na mtaro wa kusafirisha maji machafu ambao ulikuwa hatarishi kwa wanafunzi.

Mafanikio mengine ni kurudisha umeme kwenye baadhi ya madarasa na maabara, kununua na kukarabati samani na kupata ushindi wa kwanza wa mazingira kwa shule za sekondari za mjini kwa miaka miwili mfululizo.

“Tumetoa wachezaji wawili wa soka kwa wavulana katika timu ya taifa chini ya miaka 17 iliyoshiriki mashindano ya Afrika nchini Ethiopia. Msichana mmoja alichaguliwa kushiriki katika timu ya taifa ya mpira wa pete kwenye mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini Februari 2024.

“Wachezaji wawili wa kikapu wapo timu ya taifa inayoshiriki mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Rwanda mwaka huu. Pia tumefanikiwa kutoa mwanafunzi mmoja wa kikapu kwenda kusoma Marekani na kucheza kikapu,” amesema.

Mkuu huyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ziara yake aliyoifanya Machi 7,2022 ambayo imezaa matunda ya kujengwa ukumbi pamoja na maktaba ambapo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho.

Amesema ujenzi wa uwanja kwa ajili ya kuweka nyasi bandia mkandarasi ameshapatikana na kuanza kazi na miradi yote inatarajiwa kukamilika Mei 2024.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mkuu wa Wilaya mstaafu, Mwalimu Zainabu Mbilo, amewataka wahitimu watambue kwamba wanao wajibu wa kuendelea kusoma mpaka ngazi ya elimu ya juu kwani elimu ndiyo rasilimali pekee isiyoweza kuharibika.

Katika mahafali hayo wahitimu 405 walitunukiwa vyeti na zawadi kwa waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali pamoja na walimu waliowezesha wanafunzi wa kidato cha pili na nne mwaka 2023 kufanya vizuri katika baadhi ya masomo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles