24.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kuwathamini Mabalozi ni kukirudisha Chama kwa wananchi-Shemsa

Na Samwel Mwanga, Bariadi

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amesisitiza dhamira ya chama hicho chini ya Uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kukirudisha Chama hicho kwa wanachama kupitia mabalozi wa CCM huko chini ambao ndiyo wenye wanachama wengi.

Akizungumza leo, Mei 2, 2024 na Viongozi wa CCM ngazi mbalimbali kuanzia mashina hadi Kata katika Tarafa ya Ntuzu wilaya ya Bariadi kwenye mkutano wa ndani uliofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Baraidi Alliance amesema kuwa anatambua ukubwa wa nafasi ya Balozi na Shina ndani ya chama hicho.

Amesema mabalozi wanapaswa kuheshimiwa kwani wao ndiyo wenye chama huko kwenye maeneo yao hivyo hawapaswi kudharauliwa.

Sehemu ya Viongozi wa CCM katika Tarafa ya Ntuzu wilaya ya Bariadi wakiwa kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Alliance mjini Bariadi kumsikiliza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed.

“Mimi ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa, lakini nimeweka heshima kubwa kwa mabalozi sababu najua wao ndiyo msingi wa shina la CCM na ndiyo maana tumeelekeza nguvu kubwa kuhakikisha viongozi wote wa Chama wanatambua, hakuna viongozi wakubwa zaidi ya mabalozi na kwa mantiki hiyo chama kinarudi kwa wanachama na sisi viongozi tunaochaguliwa wanachama hawa ndiyo mabosi wetu na ndiyo sababu mnamuona hapa mbele ya meza kuu yupo balozi,”amesema Shemsa.

Amesema mabalozi ni viongozi muhimu katika kukijenga chama hicho na amewasihi kuendelea kukitumia kwa moyo wote huku akiwapongeza kwa kufanya kazi yao vizuri ya kukisimamia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na ndiyo maana katika mikutano yake ya kusikiliza kero anawapatia kipaumbele mabalozi hao ambao ndiyo wenye wanachama kuanzia ngazi ya shina.

Pia, amewataka viongozi hao wa CCM kufanya vikao vya kamati ya siasa katika maeneo yao na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama ili waweze kuwaeleza wananchi fedha ambazo zimeletwa na Serikali.

“Mwenyekiti wa tawi ana nguvu sawa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa na anatakiwa kufanya kazi za utekelezaji wa Ilani kama wanavyofanya viongozi wa wilaya na mkoa kuisimamia serikali kwenye maeneo yao maana miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa huko na fedha nyingi zinapelekwa huko kazisimamie,” amesema.

USHINDI CHAGUZI ZIJAZO

Aidha, amewataka viongozi hao kujiandaa na kuhakikisha wanashinda chaguzi zinazokuja za Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 kwa nafasi za Wenyeviti wa Vitongoji, Mitaa na Vijiji kwa serikali za mitaa na madiwani, wabunge na Rais katika uchaguzi mkuu wa 2025.

Sehemu ya Viongozi wa CCM katika Tarafa ya Ntuzu Wilaya ya Bariadi wakiwa kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Alliance mjini Bariadi kumsikiliza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed.

“Tutahakikisha kuwa tutasimamisha wagombea wanaokubalika katika jamii ili CCM iweze kushinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu na kuendelea kushika dola na kuwaletea maendeleo wananchi,” amesema.

Naye, Balozi Jacobo Suki wa Shina la Somanda, tawi la Butiama mjini Bariadi amesema Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu amewaheshimisha mabalozi wa chama hicho na ndiyo maana leo ameteuliwa kuongoza kikoa hicho.

Amesema kwa sasa ni vizuri mabalozi wakatembea kifua mbele kwani wanatambuliwa na kuthaminiwa na kiongozi wa juu wa chama hicho katika mkoa huo na ameahidi kwa niaba ya wenzake kufanya kazi za kuimarisha chama hicho.

“Kwa niaba ya mabalozi wote mlioko katika mkutano huu jisikieni nyote mko jukwaa kuu kwa heshima hii niliyopewa na Mwenyekiti wa CCM kuwa huku inaonyesha wazi kuwa anatuthamini na mimi nikuhaidi na mabalozi wenzangu tutafanya kazi kwa moyo ili kukijenga chama chetu,” amesema.

Mkutano huo uliojumuisha viongozi mbalimbali wa chama, Serikali, dini na wazee katika tarafa ya Ntuzu ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya mwenyekiti huyo kutembelea Tarafa zote za mkoa huo na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles