23.9 C
Dar es Salaam
Monday, May 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake Kipunguni njia nyeupe uchaguzi 2024/25

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

“Wanawake tunapewa mbinu nyingi za kushiriki katika uchaguzi, tunapambana vya kutosha lakini tunarudishwa nyuma. Kuna vikwazo vingi tunaomba Serikali itende haki bila kujali mtu anatoka chama gani,” anasema mkazi wa Dar es Salaam, Rehema Mfaume.

Rehema ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa mwaka 2014 ni mfano wa wanawake wengi wenye kiu ya kuwa viongozi katika ngazi za maamuzi lakini wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na vikwazo mbalimbali.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha ushiriki wa wanawake katika vyombo vya uwakilishi wa wananchi bado ni mdogo ikilinganishwa na azma ya kimataifa ya kufikia uwiano sawa kijinsia na maendeleo endelevu ifikapo 2030 katika vyombo vyote vya maamuzi.

Taarifa ya uchaguzi wa mamlaka za serikali za mtaa mwaka 2019 inaonyesha katika ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa wanawake viongozi ni 1/3 pekee ya viongozi huku wengi wakiwa katika ngazi ya wajumbe.

Aidha kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji katika uchaguzi wa 2019 wanawake ni 246 wakati kati ya wenyeviti wa mitaa 4,171 wanawake ni 528.

Vilevile kati ya nafasi 62,612 za wenyeviti wa vitongoji, wanawake ni 4,171.

Kwa upande wa madiwani katika uchaguzi wa 2020, madiwani wanawake ni 260 kati ya 3,953. Madiwani wa Viti Maalumu ni 1,374 na kufanya idadi ya wanawake kuwa 1,634 kati ya madiwani wote 5,587.

Baadhi ya wajasiriamali wadogo Kipunguni wakiwa kwenye shughuli zao.

Pia wenyeviti wanawake wa halmashauri ni watano kati ya halmashauri 185 na meya ni mmoja.

Kumekuwa na jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali wa maendeleo za kuhakikisha ushiriki wa wanawake unaongezeka katika ngazi za maamuzi kwa kubuni mbinu zitakazowawezesha wanawake wanaotaka kugombea kushinda vikwazo.

‘Muwezeshe Ashinde’ ni mbinu iliyobuniwa na vikundi vya wajasiriamali vinavyounda tapo la vikundi Kipunguni kwa lengo la kuwawezesha wanawake wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Kupitia mbinu hiyo wana tapo 86 wa Kipunguni ambao wote ni wajasiriamali kila mmoja atakuwa akiweka akiba ya Sh 200 kila siku kuwawezesha wanawake watakaogombea.

Mwenyekiti wa umoja huo, Maria Mushumbusi, anasema kampeni hiyo imeanza kutekelezwa kuanzia Mei Mosi,2024 hadi Septemba 2,2024 ambapo wanatarajia kukusanya Sh 2,064,000.

“Kuanzia sasa tuanze kuwashawishi wanawake wenye uwezo wa kuongoza ili kipindi kikifika wachukue fomu na wasio na vyama wajiunge na vyama vya siasa.

“Kikifika kipindi cha kuandikisha wapigakura tuhakikishe tunahamasisha wanawake wote wanajiandikisha kwa ajili ya kupiga kura,” anasema Mushumbusi.

Anasema wanaamini kwenye ofisi nyingi za serikali za mitaa viongozi wakiwa wanawake ukatili utapungua kwa sababu mwanamke akiwa na mamlaka anashughulika na kesi za ukatili kwa karibu kuliko wanaume.

Anasema hata kutengwa bajeti za mrengo wa jinsia itakuwa rahisi kwa sababu suala la zahanati, vyumba vya usiri kwenye vyoo shuleni, pedi mashuleni na kuwekwa mifumo ya maji safi na salama na vituo vya afya ni masuala yanayomgusa mwanamke moja kwa moja na wanawake wakiwa wengi kwenye ofisi za serikali za mitaa watayapigania.

“Kiasi cha shilingi 200 kwa siku ni fedha kidogo kwa mjasiriamali mmoja lakini kwa wingi wetu ni fedha nyingi. Na kwa mwitikio uliopo naamini tutakuwa mfano wa kuigwa,” anasema.

Katibu wa umoja huo, Zainab Omary, anaishukuru Sauti ya Jamii kwa kuwaunganisha wajasiriamali wadogo kwenye tapo la pamoja kwani hivi sasa inakuwa rahisi kutoa sauti zao kwa pamoja tofauti na awali ambapo kila mtu alikuwa kivyake.

“Kupitia umoja huu tumeanzisha vitu vingi ikiwemo mfuko wa kusaidiana, akaunti ya pamoja na tunapeana mikopo midogo midogo.

“Pia tumepata mafunzo ya kifeminia na uongozi kutoka Sauti ya Jamii ambapo kwa sasa kila mwana tapo anaamini katika usawa. Tunashiriki kupambana na vitendo vya ukatili ikiwemo rushwa ya ngono, ukeketaji, ndoa za utotoni na haki nyingine za wanawake ikiwemo wanawake na wasichana wanaolea peke yao,” anasema Zainab.

Katibu huyo anasema hamasa imeanza ambapo wanawahamasisha wanawake wenye uwezo wa kuongoza washiriki kuomba ridhaa kupitia vyama vyao.

“Wakati wa kujiandikisha tutapita nyumba kwa nyumba kuhakikisha wanawake wote wanajiandikisha kwenye daftari la mpigakura ili kazi yetu iwe rahisi kipindi cha uchaguzi kikifika,” anasema.

Baadhi ya wajasiriamali wadogo Kipunguni wakiwa kwenye shughuli zao.

Anasema wanatarajia kuhamasisha wanawake wengine wajiunge katika kampeni hiyo ili kila mwanamke ahakikishe anashiriki kuwaunga mkono wanawake ambao watapitishwa kugombea nafasi za uongozi wa serikaliza za mitaa.

Wana tapo wa Kipunguni ni mfano wa jitihada zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali kuhamasisha wanawake kushiriki katika uchaguzi na kugombea hasa ikizingatiwa kuwa mwaka huu kunafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mathalani Shirika la WiLDAF linahamasisha wanawake kushiriki ambapo limetengeneza kaulimbiu yake ya ‘Mjumuishe ongeza idadi ya Wanawake wa kuchaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles