25.1 C
Dar es Salaam
Monday, May 20, 2024

Contact us: [email protected]

TAG wajivunia miaka 85 ya ujenzi wa umoja, amani

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Barnabas Mtokambali amesema miaka 85 ya kanisa hilo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwaunganisha Watanzania na kuchagiza maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.

Kanisa hilo lililoanzishwa mwaka 1939 Igale jijini Mbeya hadi sasa lina matawi zaidi ya 16,000 nchini huku pia likiwa limefungua makanisa katika nchi za Madagascar, Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Kenya na Rwanda.

Akizungumza Mei 8,2024 na Waandishi wa habari, Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, amesema kanisa hilo limekuwa kielelezo cha ujenzi wa umoja, amani na upendo.

Dk. Mtokambali alikuwa akizungumza kuhusu maadhimisho ya miaka 85 ya kanisa hilo ambayo yatafikia kilele Julai 14,2024 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Tunamshukuru Mungu kwa uaminifu wake kwa kutuwezesha kubaki imara kwa miaka 85, tunafurahia kuleta mabadiliko ya kiroho katika maisha ya watu wetu. Kupitia programu za mafunzo na uongozi tunao viongozi wa kiroho na kada nyingine nchini…tumetoa viongozi wakuu nchini ambao wako katika nafasi za juu serikalini wanaochagiza katika kuleta maendeleo,” amesema Dk. Mtokambali.

Aidha amesema wana vyuo tisa vya Theolojia na kimoja cha Uinjilisti ambapo pia wana matawi 71 ya vyuo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu miradi ya maendeleo amesema wanazo shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, vyuo vya afya, vyuo vya ualimu, vituo vya redio

Kwa mujibu wa Dk. Mtokambali, watoto 20,000 wanapata huduma za kijamii kupitia makanisa 94, kaya 3400 ambazo ni maskini zimefikiwa na kuwezeshwa kiuchumi kupitia makanisa 173, vijana 500 waliokuwsa wakitumia dawa za kulevya wamefikiwa kupitia mradi wa Teen Challenge.

Vilevile 22,000 wa shule za msingi na sekondari wamefikiwa kwa kupatiwa chakula na taulo za kike, watoto zaidi ya 2,000 katika Jamii za Wahadzabe na Wagatoga mkoani Manyara wanapatiwa elimu kupitia shule za msingi zilizojengwa na kanisa hilo.

Amesema kabla ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kongamano la vijana zaidi ya 10,000 wenye umri chini ya miaka 35, viongozi wa jeshi la polisi na viongozi wengine serikalini, mkutano mkubwa wa injili utakaoongozwa na Mwinjilisti wa Kimataifa kutoka Sweden na semina kwa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali.

Shughuli nyingine ni kuchimba visima vya maji katika baadhi ya shule za Mkoa wa Dar es Salaam na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi 6,000 wa shule hizo.

Askofu huyo ameishukuru Serikali kutokana na ushirikiano walioupata katika awamu zote ambao umeliwezesha kanisa kutekeleza majukumu yake ikiwemo uhuru wa kuabudu na kuahidi kuwa wataendelea kuwa chanzo cha matumaini, upendo, amani na mabadiliko chanya katika taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles