24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

PPRA yasaini mkataba wa makubaliano na UNDP kuongeza ufanisi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesaini mkataba wa makubaliano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 17 (zaidi ya Sh bilioni 40) unaolenga kuiwezesha mamlaka hiyo kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mkataba huo umesainiwa leo Aprili 24, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa PPRA makao makuu jijini Dodoma kati ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Eliakim Maswi na Mwakilishi Mkazi wa UNDP – Tanzania, Shikegi Komatsubara.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi, amesema mkataba huo ni kwa ajili ya kusaidiana katika maeneo makubwa matatu ambayo ni kuijengea mamlaka hiyo uwezo katika manunuzi ya umma, kujengea uwezo wadau wa ununuzi wa umma, na kuiwezesha PPRA kuwa na vitendea kazi.

“Kama mnavyojua UNDP ni ya Ulimwengu kwahiyo kutokana na kwamba wanafanya manunuzi makubwa katika ulimwengu ni vizuri tukawa nao wakatusaidia ili kujiimarisha katika eneo la kujenga uwezo kwetu sisi kama taasisi lakini uwezo wa watu wetu ambao wanahusika na ununuzi wa umma,” amesema na kuongeza;

“Eneo la pili ambalo tumesaini mkataba wetu ni katika kujengea uwezo wadau wetu. Kama mnakumbuka Sheria yetu ya manunuzi ya umma ilipitishwa mwaka jana na moja ya eneo ambalo tulilijadili na waheshimiwa wabunge walilijadili sana ni kuwezesha wazawa katika kusimamia miradi mikubwa nchini.

“Na kama mnakumbuka katika ile Sheria tulisema kwamba miradi yote ambayo iko chini ya Sh bilioni 50 lazima iwe ni ya wazawa, na ile mikubwa zaidi ya hiyo lazima kampuni itakayosimamia iwe ni ya wazawa pia ili kampuni za wageni zihamishe utaalam walionao kwa wazawa. Kwahiyo UNDP wamekubali kutujengea na kujengea uwezo wakandarasi wetu wadogo ili waweze kuwa na uwezo wa kufanya kazi vizuri,” amesema Maswi

Baadhi ya viongozi wa PPRA wna UNDP wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusaini mkataba huo.

Ameongeza kuwa katika eneo la tatu la makubaliano hayo ni kuiwezesha PPRA kuwa na vitendea kazi vitakavyoisaidia katika shughuli zake za ukaguzi wa thamani halisi ya fedha, hivyo, shirika hilo litawasaidia kupata vifaa kwa ajili ya kufanyia ukaguzi wa thamani halisi ya fedha katika nchi yetu.

“Kwahiyo makubaliano haya tulianza kujadili mwaka 2022 yakapita wizara ya fedha yakaja tume ya mipango baadaye yakakubalika kwa ajili ya kusaini kwahiyo ni makubaliano endelevu na tunaomba Mungu atujalie tuweze kuyatekeleza vizuri ili yawe endelevu na tuwe ununuzi endelevu katika nchi yetu.

“Moja ya vitu tulivyokubaliana atatusaidia ni ununuzi wa vitu kwa bei nzuri ya kimataifa. Kwahiyo tulichokubaliana kwenye mkataba ni kwamba tukishaingia mkataba wanakwenda kutafuta hela zinazopatikana wanaleta, kwahiyo wamesema kwa kuanza wamesema hii miezi miwili ya mwanzo watatupatia Sh milioni 500.

“Lakini kwa mfano mwaka kesho pia wameniahidi kwamba wanaweza kutoa Sh bilioni 2 za kujenga uwezo wa watumishi na wadau. Niwahakikishie kwamba mkataba huu kwetu sisi una manufaa makubwa sana tunahitaji tuone thamani ya fedha kwa taasisi zetu,” ameeleza Maswi

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Shikegi Komatsubara, amesema changamoto kubwa inayokabili mchakato wa manunuzi ni thamani ya fedha ambapo Serikali ya Tanzania imekuwa ikikumbana na bei ya juu ya bidhaa, huduma na shughuli katika utekelezaji wa programu zake za maendeleo, hivyo kuikabili nchi na kushindwa kutoa huduma sahihi na zilizo bora kwa wananchi wake.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Shikegi Komatsubara (kushoto) wakisaini mkataba huo.

Ameongeza kwamba nchi nyingi ikiwemo Tanzania zimekuwa zikikumbana na tatizo la ucheleweshaji, kutokuwepo kwa uwazi na uadilifu kwa baadhi ya taasisi za ununuzi zinapofanya manunuzi ya bidhaa, miradi au kazi na huduma ambazo zimekuwa zikihitajika kuhudumia nchi na kusaidia katika kufikia malengo yake ya maendeleo ikiwemo malengo ya milenia na ajenda ya mwaka 2063 ya umoja wa Afrika.

“Katika kukabiliana na hizo changamoto, UNDP kupitia programu yake ya Country Program Document (CPD) 2022 – 2027 imeazimia kuisaidia Serikali na Watanzania kuimarisha mfumo wa manunuzi wa nchi ili kuleta thamani halisi ya fedha, ufanisi na uimara wa mfumo. Kupitia CPD, UNDP itawashawishi wadau wengine wa maendeleo kuisaidia Tanzania kuunda ajenda ya mageuzi ya mfumo wa manunuzi utakaochangia kufanikisha malengo ya milenia na utoaji huduma kwa wananchi wa Tanzania,” amesema Komatsubara

“Kupitia jitihada hizi, UNDP itaimarisha mfumo wa Sheria, usimamizi na sera ili kuwa na ununuzi wa umma wa bidhaa, huduma na shughuli zenye ubora kwa serikali ya Tanzania na wananchi wake. Hili linalenga katika kuhakikisha taratibu za ununuzi inazingatia uimara, ubora na maslahi mazuri ya wananchi na serikali,” ameongeza:

“Pia tutaisaidia Serikali ya Tanzania kuanzisha na kukuza Mahusiano na wasambazaji wakubwa wa bidhaa na huduma kama vile Toyota Gibraltar. Huu ni mwanzo wa ufanisi wa manunuzi wa bidhaa hizo, ambapo UNDP Tanzania itaweza kutumia miundombinu iliyopo ikiwemo Mahusiano ya muda mrefu kurahisisha ununuaji wa bidhaa.

“Katika kutekeleza hili, shirika letu litaingia makubaliano na taasisi ama idara husika ndani ya Serikali ya Tanzania kupitia na kuanzisha uratibu wa kitaasisi utakaosimamia upangaji, uendelezaji, usimamizi na utekelezaji wa mikataba na kutengeneza kada ya wataalam wa ununuzi watakaoongoza na kubeba majukumu hayo,” amesema Mwakilishi huyo.

Naye, Mtaalam wa miradi ya Maendeleo katika Shirika hilo, Deogratias Mkembela, amesema kupitia makubaliano hayo faida mbalimbali zitapatikana ikiwemo kuisaidia Serikali kuwafikia vijana, wanawake na makundi maalum kupitia uwezeshaji biashara ndogondogo, kuzalisha na kuingiza bidhaa zenye ubora zilizokidhi vigezo ambazo zitatunza mazingira na kulinda tabianchi.

Baadhi wa washiriki wa Mkutano wa nne wa baraza la wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi w Umma (PPRA).

“Tunafurahi kufikia hatua hii ni safari ya muda mrefu, mkataba huu na makubaliano haya yanatupa fursa zaidi ya kuwa na mashirikiano makubwa na PPRA na inaturahisishia ufanyaji kazi na PPRA.
Mradi huu utatupatia fursa kama nchi kuweza kuleta wadau wengine wa maendeleo kushirikiana na PPRA, hususan eneo la manunuzi ambalo sisi kama UNDP tuna uwezo kuwafikia wazalishaji wengi wa vitu kwahiyo tunaamini baada ya muda mrefu wa mkataba huu nchi itafaidika,”

“Faida ambayo unaweza kuzipata kwa kufanya kazi na wazalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ambazo tunazitumia kusaidia wananchi wetu katika shughuli za maendeleo na shughuli za kijamii kiujumla ni kuweza kupata vitu katika bei ambayo inaonyesha uhalisia, bei ambazo ziko pungufu,” amesema Mkembela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles