32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga, Azam mawindoni Ligi Kuu

yanga-azamNa ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa kuchezwa michezo saba kwenye viwanja tofauti, huku mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga wakiwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kucheza na Majimaji ya Songea.

Yanga ina pointi nne hadi sasa baada ya kucheza mechi mbili, wataingia uwanjani wakiwa na machungu ya kuambulia pointi moja mkoani Mtwara walikocheza na Ndanda FC Jumatano iliyopita.

Yanga inayonolewa na kocha Hans van Pluijm, inatarajia kuwatumia wachezaji wake wa kimataifa, Haruna Niyonzima na Vicent Bossou, waliikosa mechi iliyopita kutokana na kuwa na majukumu ya timu zao za taifa.

Kwa upande wa Majimaji waliopo chini ya kocha Peter Mhina, msimu huu wameonekana kuanza vibaya ligi, watawakabili Yanga wakitoka kupokea vichapo vitatu mfululizo katika mechi zake za awali na hivyo kushika mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Timu hizo zinaingia uwanjani huku Yanga ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuichapa Majimaji mabao 5-0 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya marudiano iliyochezwa Majimaji, Songea msimu uliopita.

Katika mchezo mwingine leo, vinara wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, Azam FC watakuwa wageni wa Mbeya City katika mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Azam FC inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi saba sawa na Mbeya City na Simba zote zikiwa zimecheza mechi tatu lakini zikipishana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

JKT Ruvu nao watacheza na Ruvu Shooting katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi huku Stand United wakimenyana na Mwadui FC katika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

African Lyon wataikaribisha Mbao FC katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaaam huku Ndanda FC ikiialika Kagera Sugar katika Uwanja wa  Nagwanda Sijaona, Mtwara.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili ambapo Simba wataikaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Mtibwa watahitaji kulipa kisasi baada ya msimu uliopita kufungwa mechi zake zote za nyumbani na ugenini.

Kwenye mzunguko wa kwanza msimu uliopita, Simba ilianza kupata matokeo ya ushindi wa bao 1-0 ikiwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kisha kuwafunga tena bao 1-0 katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mechi nyingine kesho itakuwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Tanzania Prisons watakapocheza na Toto Africans ya Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles