26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Waliokufa Indonesia wafikia 1,200

JARKATA, INDONESIA

Idadi ya watu waliofariki dunia katika tetemeko la ardhi lililoambatana na kimbunga cha tsunami  nchini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita inazidi kuongezeka na sasa imeripotiwa kufikia 1,200.

Taarifa hiyo imetolewa jana na kitengo cha maafa, ambacho juzi kilitangaza waliokuwa wamepoteza maisha ni watu 844.

Katika hatua nyingine, Serikali imeomba msaada wa jumuiya za kimatafa wakati huu ikihangaika kupata chakula sambamba na vifaa vya uokoaji katika Kisiwa cha Sulawesi, ambacho kimeharibiwa vibaya kwa kimbunga na tsunami.

Hadi sasa nchi za Thailand na Australia tayari zimetoa misaada yao huku vikosi vya uokoaji vikiendelea na juhudi za kutafuta watu waliokwama katika majumba makubwa kwenye mji wa Palu, huku uwezekano wa kuwakuta wakiwa hai ukiendelea kupungua.

Vikosi hivyo vya uokoaji bado vinajaribu kuwafikia mamia ya watu ambao inawezekana wakawa hai katika mji wa Palu ambao miundombinu yake imeharibika vibaya huku wengi wao wakitajwa kukwama katika maduka na majumba makubwa.

Katika ziara yake kwenye mji wa Palu, Rais Joko Widodo aliwaambia viongozi wa eneo hilo kuwa Serikali kuu itatoa mahitaji yote muhimu ili matengenezo mapya ya mji huo yaweze kufanyika.

“Hakika hii ni hali ya dharura kama ilivyo ya Lombok. Kutakuwa na ugumu kwa siku moja au mbili na ni kazi kubwa. Uelekeo wa barabara hii haupo, imefungwa, hata uwanja wa ndege haufanyi kazi ipasavyo.

“Vituo vya kuzalisha umeme pia vimeharibiwa, na kati ya saba ni viwili tu ndivyo bado vinafanya kazi na wasambazaji wa mafuta wasingeweza kuyafikia maeneo kutokana na kuharibika kwa barabara. Lakini tayari tumeagiza kila kitu kama mafuta, na wasambazaji watafika siku mbili kuanzia sasa,” alisema Rais Widodo.

Alisema vifaa vyote vizito vitawasili katika eneo hilo ili viweze kuvitumika pamoja na misaada kama vile chakula na maji safi.

“Baada ya kuona kila kitu kinafanya kazi kama kawaida, tutaingia kwenye hatua ya kujenga na kuzirekebisha nyumba zilizoharibika,” alisema Rais Widodo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles