25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wenyeviti wa Vitongoji Mugumu waandamana wakidai posho zao milioni 30

Na Malima Lubasha, Mtanzania Digital

WENYEVITI 30 wa Vitongoji  wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wameandamana hadi ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya kudai malimbikizo ya posho zao za vikao na madaraka zaidi ya Sh milioni 30 kutoka mwaka 2019 hadi mwaka huu.

Maandamano hayo yamefanyika juzi ambapo wenyeviti hao waliokuwa na sura ya kutokuwa na furaha walilalamika kucheleweshewa posho hizo wakati wa kikao chao cha kawaida cha Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo Mugumu kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hivi karibuni.

Wakichangia hoja hiyo pia akiwepo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Bainga Ismail baadhi ya wenyeviti walisisitiza kulipwa madai hayo ya muda mrefu ambapo suala hilo wamekwisha lifikisha kwenye uongozi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya, kwa mkuu wa wilaya na kuonana uso kwa uso na mkurugenzi ili kusaidia waweze kulipwa.

“Watulipe posho zetu ni haki yetu ya msingi sio hisani,” alilalamika mwenyekiti wa kitongoji cha Nyamerama, Mwita Nyanswi.

Pia, Mikidadi Idd Makamu Mwenyekiti wa Mmlaka ya Mji Mdogo na kitongoji cha Stendi mpya alihoji mwaka huu mwezi  juni wanahitimisha uenyekiti wao na kwamba: “Je, kweli tutalipwa madai yetu huku, halmashauri itutendee haki kama tulivyokuwa tunadai pamoja na madiwa lakini wao wamekwishalipwa posho zao zaidi ya milioni 39,” amesema.

Aidha, Mwenyekiti wa kitongoji cha Seronga kata ya Morotonga, Bruno Lucas Nyawera alisema madai yao ni halali akataka malipo yafanyike huku akionyesha vielelezo vya madai yao.

Ilielezwa kuwa katika kipindi hicho cha miaka 5 wenyeviti hao wanadai shilingi milioni 26 za posho na vikao pia posho ya madaraka zaidi ya shilingi milioni 3 ambapo kila mwenyekiti anatakiwa kulipwa shilingi 50,000/- kwa mwezi zikiwemo fedha za vikao mwezi Machi na Aprili mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Bainga Ismail, amekiri kuwepo kwa madai ya posho za wenyeviti hao tunaangalia kuona tutalipa namna gani naomba muwe na subira.

“Haya ni madeni tuliyorithi kutoka kwa wakurugenzi waliopita kuanzia mwaka 2019, tumeyapokea na tutayalipa yote kwa awamu, hizi ni fedha za serikali, kuanzia sasa tunaendelea kutazama nyaraka tupate yaliyo sahihi yalipwe,” amesema Ismail.

Naye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu, Charles Chacha Ally, amekiri kuwepo kwa ahadi ya ulipaji wa posho hizo na kufikisha malalamiko haya ngazi mbalimbali za wilaya kusaidia ili yaweze kulipwa.

“Ni kweli wameahidi kulipa fedha kidogo kidogo kutokana na vyanzo vya halmashauri japo hiyo siyo ma ra ya  kwanza kutuahidi, walikwisha ahidi zaidi ya mara sita ,naomba watulipe ni fedha zinazofahamika kikanuni na kisheria maana zinatusaidia kutekeleza majukumu yetu ya kuwahudumia wananchi,” amesema Ally.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles