24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WAFYATUAJI FATAKI MWAKA MPYA WADHIBITIWA

LEONARD MANG’OHA NA FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM


 

fatakiMKESHA wa kuukaribisha mwaka mpya wa 2017 umepokewa kwa aina yake jijini Dar es Salaam, huku Jeshi la Polisi likilazimika kuwatia mbaroni baadhi ya wananchi waliokuwa wakivyatua mafataki.

Hatua hiyo inatokana na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupiga marufuku ulipuaji wa mafataki na uchomaji wa matairi.

MTANZANIA ilishuhudia baadhi ya askari polisi wakitumia nguvu kuwatia mbaroni baadhi ya wakazi wa Mwananyamala Komakoma hadi Hospitali ambapo vijana zaidi ya watano walijikuta wakiishia katika mikono ya polisi.

Mbali na hilo pia jeshi hilo lilikuwa likitumia helkopta na kufanya doria usiku wa jana katika jiji hilo kama njia ya kuimarisha ulinzi.

Ilitimu saa 6:10 usiku askari polisi walionekana wakishuka katika magari yao na kwenda kuzima mafataki yaliyokuwa yamelipuliwa na wananchi ambao walikuwa wakisherehekea kuingia kwa mwaka mpya 2017.

Pamoja na hali hiyo baadhi ya wananchi katika maeneo ya Posta na Kariakoo walionekana kuwazidi ujanja polisi ambao walionekana wakifyatua mafataki wakiwa juu ya maghorofa wanayoishi lakini baada ya muda askari walipofika kila mmoja alikimbilia ndani kwa hofu ya kukamatwa.

Timu ya MTANZANIA ilipiga kambi katika maeneo ya Kinondoni, Magomeni, Ubungo, Kariakoo, Msasani na Temeke ambapo wananchi wengi walifurahi mwaka mpya kwa utulivu huku wengine walionekana wakicheza muziki nje ya nyumba zao.

Hata hivyo kwa mwaka huu shamrashamra hazikuwa kubwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo wananchi hususan vijana walikuwa wakipita mitaani huku wakiwa katika makundi wakicheza ngoma.

Licha ya hali hiyo Jeshi la Polisi lilionekana kuimarisha ulinzi katika maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo katika nyumba za ibada ambapo askari waliokuwa wamevalia kanzu na kiraia waliokuwa wakifanya doria.

“Huu si uungwana kabisa watu tunafurahia kuupokea mwaka mpya alafu tunakamatwa, yaani tunakuwa kama wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe.

 

“Sasa unamkamata mtu muda huu unampeleka wapi usiku huu, huu ni mwanzo wa kuharibiana sikukuu si jambo zuri kabisa hili linalofanywa na hawa Polisi tupo nyumbani kwetu, hii ni nchi yetu lazima tufurahi sisi siyo wakimbizi,”alisema mmoja wa wakazi wa Mwananyamala aliyejitambulisha kwa jina moja ya Omari

Pamoja na hali hiyo MTANZANIA jana ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro ili kupata ufafanuzi namna sherehe za mwaka mpya zilivyopita katika jiji hilo lakini hakupatikana.

 

Naibu Spika

Akizungumza katika maombi ya mkesha wa mwaka mpya, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson aliwataka Watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli.

“Mambo ya nyakati wa pili mlango wa saba mstari wa 14 inasema,  ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekesha na kuomba, kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe zambi yao na kuiponya nchi yao.

“Sisi lazima tuenende kwa jinsi ambavyo hatutaiangamiza nchi yetu, tuombe kwaajili ya Taifa letu,” alisema Dk. Tulia.

Alisema mwaka huu utakuwa ni wa mabadiliko chanya ikiwa kila mmoja atafanya kazi kwa bidii.

“Tanzania mpya na nchi mpya yenye matokeo chanya kwa mwaka 2017 inawezekana,” alisema Dk. Tulia kwenye mkesha huo.

 

Viongozi wa Dini

Wakati huohuo viongozi mbalimbali wa madhdhebu ya dini walitumia mkesha huo kuwasihi waumini wao kudumisha amani kwa kujenga tabia ya kuvumiliana na kusameheana.

Akizungumza kwenye Misa takatifu ya mkesha huo uliofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Poroko Joseph Matumaini, alisema popote palipo na watu wawili au zaidi lazima tofauti ziwepo na kwamba uvumilivu ni jambo muhimu.

Aliwataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kuwasamehe watu wengine pale wanapowakosea hata kama waliowakosea ni watu wao wa karibu na kuondokana na hali ya kinyongo.

Naye Msaidizi wa Askofu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chedieli Lwizo, aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwa na tabia ya kusamehe hasa pale inapotokea kuumizwa au kukwazwa na watu wao wa karibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles