24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI WANAOSOMA CHINA WAFUNGUKA

Asha Bani na Kulwa Karedia-DAR ES SALAAM


 

simonBAADA ya Serikali kutangaza kusitisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu juu nchini China, hatimaye wanafunzi hao wamefunguka na kumwomba Rais Dk. John Magufuli kutengua uamuzi huo kwa sababu unawaathiri kimasomo.

Wiki iliyopita Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia elimu ya juu, Profesa Simon Msanjila, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maelekezo kutoka ngazi za juu.

Alisema maelekezo hayo yanahusu wanafunzi wanaosoma katika nchi za China na Algeria wakiwamo waliojiunga na vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo 2016/17.

Akizungumza na MTANZANIA kutoka Beijing juzi, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi wa Tanzania Wanaosoma China (TASAFIC), Kassim Jape ambaye anasoma Chuo Kikuu cha Mawasiliano Beijing mwaka wa pili akichukua kozi ya uandishi wa habari za zimataifa, alisema uamuzi wa Serikali utawaathiri maelfu ya wanafunzi ambao wamekuwa wakitegemea fedha hizo kwa mahitaji mengi ya kila siku.

“Tupo ugenini tunasoma, leo hii unatangaza kuzuia mikopo ya elimu ya juu tutaishije ughaibuni…tunamuomba Rais Magufuli afikirie mara mbilimbili uamuzi huu kwa sababu una athari kubwa kwetu.

“Serikali ya China, haitupatii mikopo kwa maana hiyo kama Serikali yetu imeamua kufanya hivi ni sawa na kututia kitanzi kipya kwa sababu hapa kila kitu ni fedha…hatuna kaka wala dada ambaye atutapatia fedha za kujikimu jambo hili linaweza kusababisha dada zetu wakageukia biashara ya uchangudoa,” alisema Jape.

Alisema uamuzi wa Serikali kuwanyima fedha za mikopo na tiketi za ndege za kwenda na kurudi unapaswa kufikiliwa upya na mamlaka husika.

“Umenyimwa fedha za mikopo, tiketi ya ndege za ndege hivi kwa akili ya kawaida utarudije nyumbani? alihoji Jape.

Alisema, wamemwandikia barua Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu, Abdulrahman  Shimbo ili aiwasilishe Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

“Tumemwandikia barua Balozi Shimbo, tunategemea kabisa kwamba atashughulikia jambo hili kwa nguvu zote, tumefanya hivi baada ya jambo hili kufanywa bila sisi kushirikishwa,” alisema Jape.

Alisema kama kweli Rais Dk. Magufuli anataka Tanzania yenye viwanda, iweje awanyime wanafunzi mikopo ambao siku zijazo ndiyo wanaotarajia kuwa wataalamu kwenye sekta hiyo.

“Rais Magufuli anataka Tanzania yenye viwanda, sasa inakuwaje hawa wasomi ambao ndiyo wa siku zijazo unawanyima elimu bora ya kuendesha viwanda hivyo…hali hii inatuvunja moyo mno,” alisema.

Alisema mpaka sasa kuna wanafunzi wa kitanzania zaidi 1,000 wanaosoma katika majimbo 26 na wanatarajia kukutana kupitia jumuia ili kujadili suala hilo kwa kina.

Wiki iliyopita Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru  alisema kuanzia sasa wanafunzi hao hawatanufaika na mikopo kama ilivyokuwa ikitolewa miaka ya nyuma, baada ya kupata maelekezo kutoka ngazi za juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles