24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

VIJEMBE BUNGENI VINAWAPUNGUZIA SIFA

NA KULWA MZEE- DAR ES SALAAM


NI wazi kwamba, kila mpiga kura anapokwenda kwenye sanduku la kura na kumchagua mbunge wake, anachotarajia ni kuwakilishwa vyema bungeni na kero zake kuelezwa kinagaubaga.

Hata hivyo, baadhi ya wawakilishi wa wananchi, wanapokuwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, wameonekana wakitoa kauli za kejeli wakati ajenda zikijadiliwa.

Ikumbukwe kuwa, Bunge lililoisha, mbali ya kujadili na kupitisha Bajeti ya 2017/2018, pia lilijadili miswada mitatu ya rasilimali za nchi ya madini na petroli.

Mara kadhaa Spika Job Ndugai na Naibu wake Dk. Tulia Ackson, waliwakumbusha wabunge umuhimu wa wao kuwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria na matarajio ya wananchi wao kwao.

Wao wenyewe wabunge kuna nyakati walionekana wakikemeana, akiwamo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliyesema tukio muhimu ikiwamo la kujadili miswada lilipokuwa likiendelea, umuhimu wake ulikuwa hauendani na mjadala uliokuwa ukiendelea bungeni.

Alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakitupiana vijembe bila kuangalia umuhimu wa jambo nzito lililopo mbele yao.

Haikuishia kwa Zitto, hata Mbunge wa Vunjo, James Mbatia alizungumzia hali hiyo ya kutupiana vijembe badala ya kujadili hoja iliyopo mezani kwamba haikuwa na maslahi kwa Taifa.

Wabunge wanachotakiwa kufahamu kwamba wanapokaa bungeni wako kwa maslahi ya Taifa na wapiga kura wao wanatakiwa kuacha tofauti zao za kivyama.

Waungwana hubishana kwa hoja na hatimaye hupata majibu sahihi na uamuzi sahihi kwa jambo husika lakini wanaobishana kwa kuangalia utofauti wao wa vyama bila kujali maslahi ya Taifa wanakosea.

Hakuna Mtanzania asiyejua kwamba tuko katika vyama vingi na wanaotuwakilisha wametoka katika vyama mbalimbali hivyo kuchangia kwa hoja bila kurushiana vijembe haiondoi uhalisia wako wa chama walichotoka.

Waungwana huona aibu pale anapobaini anachofanya si sahihi, kuna kila sababu ya wabunge wanaopenda kurushiana vijembe wajitathimini, wabadilike kwani bungeni unapongezwa kwa kutoa hoja za msingi na si vichekesho kwa kurusha vijembe.

Mnapaswa kulitafakari jambo hili, kujitathimini pande zote mbili na kuchukua uamuzi wa kubadilika kwani kwa kuendelea kufanya hivyo kunawapunguzia sifa za uwakilishi.

Kuna matukio mbalimbali yaliyotokea lakini nitatoa mifano michache, wakati uchangiaji ukiendelea, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika(Chadema) akiwa anachangia, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Morogoro, Goodluck Mlinga(CCM) aliomba mwongozo wa Naibu Spika, Dk. Tulia, akazungumzia mavazi yanayostahili kuvaliwa bungeni.

Akasema vazi alilovaa Mnyika si vazi la kibunge ni la trafiki… vicheko viliibuka lakini Dk. Tulia alisoma kanuni na mavazi yanayostahili kuvaliwa alisema Mnyika alivaa suti hivyo inastahili kuvaliwa.

Mlinga inawezekana kweli aliona hilo ni vazi la trafiki lakini kabla ya kumkatisha kuzungumza alipaswa kujiridhisha kwani ukishamkatisha mzungumzaji ni wazi kwamba kama hakujielekeza vizuri anaweza ashindwe kuendelea pale alipoishia wakati akisikiliza mwongozo.

Wapo wazungumzaji wengine ambao kila wakisimama kabla ya kuwasilisha hoja huanza kwa kuushambulia upande pinzani, kuonyesha wanao upungufu fulani ama kuonyesha kwamba hawaelewi mambo.

Hayo yanafanywa na wabunge wa upinzani na wa CCM pia, hali inayosababisha mara kadhaa Spika ama Naibu Spika kuzuia, kutoa ufafanuzi na wakati mwingine kuwasema kwa kuwakumbusha kanuni.

Upinzani mara kadhaa wamekuwa wakionyesha kuonewa na hata wengine walidiriki kusema Bunge ni dhaifu.

Maneno hayo yaliyoonekana ya kuudhi yalisababisha Spika Ndugai kupandisha hasira na kuzungumza kwa hasira akikemea kauli hizo.

Moja ya tukio ambalo Ndugai alionekana kukasirika sana na kutoa kauli kali ni lililomuhusisha Mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa na Mnyika.

“Bahati nzuri tunatumia fursa hii kuelezea baadhi ya mambo.

Wenzetu ambao muda mwingi wanakuwa hawapo, wakija wanachafua hali ya hewa, alisimama mtu hapa na kusema Bunge hili ni dhaifu.

“Kwa kanuni yangu hizi ndizo lugha za kuudhi, unapowaona wenzako wengi namna hii waliochaguliwa ni dhaifu, lazima kuna tatizo kwako, huwezi tu hivi hivi una akili timamu halafu ukawaona wenzako wote kundi la wajinga fulani, wewe una akili kuliko wao, unatoa wapi maneno ya namna hii,”alisema Ndugai.

Anasema binaadamu lazima uwe na staha ile ndogo kwa binadamu wenzako hata kama hukubaliani nao katika mawazo na kwamba watu wana familia zao hivyo wanahitaji kuheshimiwa.

“Watu wana familia zao  halafu mtu mmoja anasimama anasema dhaifu, ndio hao hao waliowahi kusema Rais Jakaya Kikwete dhaifu”

“Wakati mwingine utawala unaweza kuutengeneza mwenyewe na kuuharibu wenyewe kwa midomo yenu, unasema utawala dhaifu, utawala unaanza kugangamala si umesema dhaifu…….aliyefanya agangamale nani kama sio wewe na mdomo wako?

“Mara mnakimbia huku na kule, mnafungua madudu gani sijui, hakuna kesi wala nini…. nasema mimi ndio Spika, mwaka….. mtu hakanyagi hapa,”alisema.

“Kama mtu hakuheshimu anakusemea mbovu kwanini umsikilize haiwezekani…kinacholeta matatizo ni tabia na lugha za humu ndani, yakirekebishwa hayo mawili tutaenda vizuri,”alisema.

Msigwa ni miongoni mwa waliotoka kauli kwamba Bunge dhaifu.

“Inajionyesha kuwa jinsi Bunge ambavyo linaonekana kuwa halitimizi wajibu wake na kwamba Serikali inatuchukulia poa tu.

“Hivi vifungu ukiwauliza wabunge wanavipitia saa ngapi, kila siku itifaki zinapoletwa zinaletwa siku hiyo hiyo unavipitia saa ngapi unasoma saa ngapi tunapewa dakika tano kuchangia, mikono yetu na nguvu yetu ya Bunge inapungua nguvu kwa mambo kama haya.

“Lazima tuwe na Bunge lenye nguvu ambalo linaweza kuhoji Serikali, nilikuwa naomba Serikali iwe inafanya vitu kwa utaratibu, Serikali zote duniani huwa zinapenda kulifanya Bunge liwe kibogoyo ili ifanye mambo yake na sisi tunatakiwa kuhakikisha tunachukua jukumu letu la kuishauri Serikali na hatuwezi kuchukua jukumu kama Serikali ndio inatusimamia na kuletewa mbuzi kwenye magunia na tunashangilia.

“Ni kukwepa majukumu, nachoomba tuliinue Bunge letu kiwango tunavyokuwa na Bunge dhaifu ndio tunakuwa na Serikali dhaifu, mawaziri lazima tuwashughulishe wafanye kazi na hawa hawatafanya kazi kama wabunge watakuwa dhaifu,”alisema Mchungaji Msigwa.

Mbunge Mnyika alisema Msigwa aliposema Bunge dhaifu huzaa Serikali dhaifu amemkumbusha kauli aliyowahi kusema bungeni na kinyume chake Serikali dhaifu husababisha Bunge kuwa dhaifu na ndio hali waliyonayo hivi sasa kwani Bunge limefanywa dhaifu sana.

“Bunge limefanywa dhaifu na Serikali hii ingekuwa na nguvu ingejihami sana isingefanya Bunge kuwa dhaifu lakini kwa sababu Serikali ni dhaifu imefanya Bunge pia kuwa dhaifu.

Bunge hili limekuwa dhaifu mpaka mkataba mmoja na itifaki mbili zinaletwa kwa siku moja wakati Bunge lenye nguvu lingesema leo tunajadili mkataba huu,”

Mnyika alisema kama wataruhusu Serikali na Bunge kuendelea kuwa dhaifu ni wazi siku zote tutapitisha mikataba lakini utekelezaji wake hakuna.

Hayo yalikuwa baadhi ya matukio machache yaliyokuwa yakiingia katikati ya mijadala mizito kwa maslahi ya umma ambayo mara kadhaa yamekuwa yakichukua muda kwa kuombewa miongozo na kupatiwa majibu.

Huwezi kudharau hoja za wabunge ambao walipewa dhamana ya kuwawakilisha Watanzania lakini pale kwenye haja ya kunyoosheana vidole kwa nia njema ya kubadili mtindo hasi wa kuwasilisha hoja, anayeguswa anapaswa kuliona hilo.

Bunge pamoja na kupitisha Bajeti ya Sh. trilioni 31.7 pia lilipitisha miswada mitatu iliyowasilishwa kwa hati ya dharura na Rais Dk. John Magufuli.

Miswada iliyowasilishwa na kupitishwa ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali zenye upungufu uliojitokeza wa mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Mapitio na majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa mwaka 2017 .

Mwingine ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017. Miswada hiyo yenye maslahi kwa taifa, inayolinda maliasili za nchi ilipitishwa inasubiri Rais Magufuli asaini ili iwe sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles