29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

HAKI ZAKO ZIKIONDOLEWA NI KAMA UKO JANGWANI

Umeshawahi kwenda msituni na ukapiga makelele kweli kweli na mrejesho unaopata ni kelele za pori na ndege msituni. Kama hakuna mtu wa kusikia kilio chako basi utapiga makelele mpaka unageuka rangi kuwa rangi  ya majani na miti iliyokuzunguka hakuna atakayekusikia.

Je, upo peke yako, hao waliokuzunguka hawaoni na hawasikii? Labda wanyama pori watakao kukurupusha na kukimbia, ndege wataruka, lakini mimea, miti na majani watabaki kukutazama bila kukuona wala kukusikia.

Labda watalisikia lile joto ambalo linatoka mdomoni kwako na jasho linalotiririka kutoka mwilini kwako lakini kukusikia bila ya kushtuka au kuamka kwa vitendo. Jangwani hakuna hakimu wala muhukumu. Jangwani upo peke yako.

Upweke hauji kwamba unajiona upo peke yako, yaani hakuna watu wa kujumuika nao, upweke upo wakati hata kama kuna watu wengine na wewe hakuna mtu ambaye anakusikiliza au kukusikia, au hamna lugha moja ambayo wote mnaweza  kusikilizana, kuendesha mazungumzo na kuelewana basi utakutana na upweke mara nyingi tu.

Upweke pia unaweza kuwa ni kwa sababu hakuna kiunganishi cha namna yoyote kati yenu au kwenye jumuiya. Hata hivyo kama msingi ni mbovu na kama jumuiya zinazooteshwa kwenye msingi huo, basi ni lazima kutakuwa na mipasuko kwenye ukuta juu ya msingi.

Sehemu yoyote ile kama msingi ni mbovu hatutakuwa na maendeleo na kama kuna maendeleo basi ni muundo unaonekana lakini ndani ya muundo wa hiyo sehemu nafsi ina ufa na hata kumomonyoka. Sasa ni vigumu kujenga jumuiya kwenye jangwa la namna hii, mtapiga kelele lakini hakuna atakayesikia.

Haki zako zikiondolewa ni kama upo jangwani unapiga kelele na hakuna ambaye anayekusikia. Kutunga sababu ya kuondoa haki zangu kutumia sheria hapo tupo kwenye jangwa lisiloisha na utu umefikia kikomo. Tunajenga jumuiya ambayo haina upendo wa dhahiri tumechagua njia ambayo inakuza zaidi utengamano na uhasama usiokuwa na msingi.

Diaspora wanakutana sana na changamoto za namna nyingi na changamoto moja ambayo ni ya umuhimu ni jumuiya kubwa kuahirisha na kuhalalisha ya aina nyingi za mienendo-kihistoria, kitamaduni, taasisi na watu binafsi – ambayo mara kwa mara inawasaidia wazungu wakati huo huo kuzalisha matokeo mabaya na ya muda mrefu kwa watu ambao si wazungu.

Huu ni mfumo ambao upo sehemu nyingi duniani na kwa bahati mbaya unakuta kwamba kuwa na ngozi nyeusi ni leseni ya kubaguliwa kwenye jamii nyingi. Mfumo kama huu unazima sauti yako na hata kama unapiga makelele mpaka mbingu zinafunguka sauti yako haitafika pale panapohusika. Upo peke yako mno.

Sheria ni  moja au inatakiwa kuwa sawa kwa wote lakini unakuta kwamba inakata upande mmoja na kulinda pande mmoja. Sheria hiyo hiyo inatumika kukuangamiza ingawa unafikiria kwamba una haki zote. Kilio chako unakipeleka wapi?

Kama haupo kwenye jumuiya ambayo inaweza kukusaidia katika kutafuta haki basi hapo ni kama upo msituni na kupiga makelele bila ya kusikiwa. Jumuiya ikikaa vizuri basi hapo sauti yako itasikika kwani jumuiya inachukua sauti yako na kuikuza ikawa kilio cha pamoja.

Wengi ambao hawapo katika hali hii na kuelewa changamoto Diaspora wanazozipata hawatakuwa na uelewa na huruma kwamba hapa wengi wetu wanafamilia na wao pia wanatutegemea.

Ni rahisi sana kupoteza familia yako hapa kwa njia moja au nyingine. Watoto wakishaingia tu katika picha basi wewe ujue ni vigumu kuchukua uamuzi wowote bila ya kuweka familia yako katika mahesabu na uamuzi. Utajikuta kwamba umetekwa nyara na makali yapo pande zote za upanga. Tegemezi lako lipo kwenye jumuiya yako ambayo kama haina nguvu basi unaweza kupotea katika jangwa au msitu.

Jumuiya kama haina msingi mzuri wa kuweza kuona na kusaidia katika matatizo ya jumuiya yake basi malalamiko yote hayatafika mbali kwa sababu muundo wote haufai kutokana na msingi mbovu.

Jumuiya ikijengwa na upendo bila ya kubagua basi ni mwanzo wa msingi mzuri. Upendo ni lugha ya ulimwengu wote, unaozunguka na kupenyeza katika kila aina ya jamii na viumbe, ni lugha yote inayoelewa.

Upendo unapunguza urasimu na ubabaighaji na ukiritimba na kuvuka dhana hadi dhana na kugusa umri wowote. Upendo ni lugha ya ulimwengu.

Yakiwekwa mazingira kama haya ya upendo basi masuala mengi ambayo yanasumbua jumuiya zetu yatatoweka. Sauti yako itakuwa na thamani kama ya mwengine. Upweke unatoweka.

Ukisha fahamu haya yote basi iliyobakia ni kujipanga tu na kutekeleza uliyoyalenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles