23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

WILLIAM NGELEJA SHUJAA WANGU

Na JULIUS MTATIRO, NEW YORK


KAKA  yangu mpendwa William Ngeleja amefanya uamuzi wa kishujaa sana, ameamua kujitakasa kwa kurejesha fedha za wizi ambazo aliyempa anadaiwa kutuibia huko nyuma na jambo hili lilishafanyiwa uamuzi na Bunge lakini hayakutelezwa.

Hata hivyo namkumbusha Ngeleja, kwamba makosa ya jinni hayafi milele. Ukiua mwaka 1970 halafu ukaombwa ujitokeze, ukakataa, halafu mwaka 2017 (miaka 47 baadaye) ukajitokeza na maburungutu ya pesa au roho na mwili wa mtu mwingine ili uwakabidhi ndugu wa mtu uliyemuua kwa maana ya kuwalipa fidia, vitu vyako vitapokelewa lakini havifuti jinai.

Ukiiba fedha za walalahoi mwaka 1950, halafu miaka 67 baadaye ukajitokeza na fedha mara milioni elfu moja ya zile ulizoiba, zinaweza kupokelewa kwa mbwembwe kubwa, lakini hiyo haifuti jinai. Hata kama leo ungelikuja na viwanda vyote vya MO na Bakhresa na vya Dangote AKHRESA  uwakabidhi uliowahi kuwaibia senti tano huko nyuma, hiyo haifuti jinai!

Ukishatenda jinai (makosa ambayo humaanisha umeshindwa kuwa mwaminifu) kama hili la kina Ngeleja, wewe ni mtenda jinai na dunia yote sheria ziko wazi, jinai haijadiliwi, haitafutiwi ufumbuzi, haifanyiwi maridhiano. Jinai ni makosa yenye adhabu kwa mujibu wa sheria na adhabu hizo hazina mjadala.

Kama tungelikuwa na Serikali makini na inayokata kote kote, baada ya mkutano na waandishi wa habari ilipasa TAKUKURU wamsubirie geti la Habari (MAELEZO) na asionekane hadharani hadi awe mahakamani, kama kina Rugemarila!

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ni juzi tu hapa alitumia ile sheria ya kikoloni, kibaguzi na ya kitumwa, akaamuru Halima Mdee akamatwe mara moja na kusota rumande, kwa sababu tu Halima alizungumza na vyombo vya habari na akaonya juu ya mienendo ya Rais Magufuli.

Ni juzi pia wale viongozi karibu 50 wa Chadema waliokuwa kwenye kikao halali wa ndani huko Geita, walizingirwa na polisi na kukamatwa kwa nguvu kubwa sana, kisa walikuwa wanatimiza haki yao ya kikatiba kama chama cha siasa.

Huwa najiuliza, hivi tuna dola ngapi Tanzania? Hivi tuna Serikali zinazofanya kazi kwa kutumia sheria zipi kuhusu wale wa Geita au zipi kwa Mbunge wa Kawe?

Godbless Lema alipotangaza ile ndoto yake. Aliishia gerezani miezi minne. Lakini Ngeleja ametangaza hadharani kuwa amerudisha fedha zinazodaiwa kuwa ni za wizi wizi, hadi sasa yuko kwake! Are we kidding?

How could you arrest a person who predicted Ideal things which you are framing them to being against the Lawa and leave free the one who said real things which are absolutely against the law? (Unawezaje kumshughulikia mtu aliyetabiri mambo ya kufikirika tu ambayo umeamua kuigiza kuwa mambo hayo ni kinyume na sheria na wakati huo huo ukamuacha huru mtu ambaye ameeleza mambo halisi ambayo ni makosa ya jinai yasiyo na mjadala?)

Rugemalila pia ni binadamu jamani, kama yeye yuko gerezani kwa sababu ya fedha anazodaiwa kuziiba, vipi kuhusu wale waliopokea fedha hizo za wizi na tena wengine wakasema ni hela za mboga?

 

Kama Rugemalila yuko gerezani kwa kudaiwa kukwapua fedha za umma. Vipi wale watendaji na viongozi wa Serikali na Benki Kuu ya Tanzania  (BoT) walioidhinisha fedha zile zitoroshwe BoT wako huru, mitaani? YaAni unamkamataje anayedaiwa kuiba fedha halafu wale waliomfungulia geti na kumhesabia fedha kwa hiyari na wale waliowatuma wakiwamo hadi watendaji wa ikulu, wako mitaani salama?

Unamshughulikiaje Rugemalila na kuwaacha watendaji wa Benki ya Stanbic na Benki ya Mkombozi ambao walizitumia benki zao kutakatishia fedha hizo bila kujali kuwa kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za fedha na sheria za nchi?

Tunakumbuka kuwa Bunge liliazimia fedha zile zirejeshwe kwa kulipiwa kodi? Ilikuwa mwaka 2014, kina Ngeleja hawakurudisha fedha hizo, kina Chenge, Askofu wangu Kilaini nakadhalika. waliendelea kuwa na misimamo kuwa zile ni fedha halali. Nini kinachotokea hii leo? Wanawezaje tu kuzirudisha kienyeji namna hii?

Kama kweli Taifa langu lingekuwa na sheria zinazokata kote kote, Askofu Kilaini ni askofu wangu, mimi ni Mkatoliki. Huku Marekani, wapo wachungaji, maaskofu, mapasta, mapadre wako gerezani, walishtakiwa na kufungwa, kama watu wengine. Siwezi kuwatetea watu walioshiriki kuliibia Taifa, hata kama angelikuwa Papa wa Kanisa!

Unamshughulikiaje  Rugemarila kwa madai ya wizi wa fedha zile kama mwizi mkuu, halafu ukamuacha Jaji wa Mahakama Kuu ambaye alipokea fedha za umma kama rushwa au fedha haramu, Jaji! Unamstaafisha kwa maslahi ya umma, yeye hawezi kukaa jela! Kwamba Jaji ana mke mzuri na muhimu kwake kuliko Ruge? Double Standard!

Chenge pamoja na kudaiwa kushiriki kwenye masakata yote makubwa ya wizi kuanzia Rada nakadhalika na bado kupokea Sh. bilioni 1.6 za rushwa kutoka kwa Rugemalila, Chenge ameendelea kuwa mtu muhimu ndani ya CCM na nchi na leo hii Chenge ni Mwenyekiti wa Bunge. Kweli, are we serious? Yaani Rugemalira yuko gerezani kwa makosa makubwa, lakini walionufaishwa na fedha zinazomponza Rugemalira wanapeperusha bendera za Serikali mitaani?

Yaani inaingiaje akilini kuwa umuweke Mdee ndani saa 120, umuweke Lema gerezani miezi minne nakadhalika lakini Chenge yeye yuko mtaani tu! Aisee tunadanganyana sana! Hivi Chenge na Lema nani ameihasidi nchi hii to Death? Hivi Chenge na Mdee nani ameichafua nchi hii? Yaani hawa wanaotoa maoni yao, na kushauri na kuonya Serikali, wao wanaishia jela. Yale yanayodaiwa majizi makubwa yanadunda mtaani na bado watu wanakwambia nchi imebadilika kweli kweli, JPM ameinyoosha!

Na kichekesho kikuu kinaweza kuwa kwamba, hata hao wanaochukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani, TAKUKURU haifanyi hivyo kwa weledi wao, bali wana Bip  kwa Rais na kuona kama angelipenda mtu fulani afikishwe mahakamani. Sote tunajua kuwa kwa utawala wa sasa hakuna anayefanya uamuzi, kila kitu watu wanasubiria kupima upepo ikiwa kina madhara kwao (kitamfurahisha Rais au La!) Maana kwa sasa unaweza kufanya uamuzi mzuri lakini Rais asiyapende, utatumbuliwa na ukifanya uamuzi mbaya akayapenda unaweza kubaki (na kinyume cha kila moja), kwa hiyo pona pona yako ni kutokufanya lolote hadi uwe na uhakika kuwa litamfurahisha Rais.

Unaweza kukuta TAKUKURU wana ushahidi dhidi ya Askofu  Kilaini, kwamba anastahili kushtakiwa, lakini unaweza shangaa wakubwa wanawaambia, “huyo mwacheni, huyo ni askofu! Kwa kweli hili ndilo Taifa tunalojenga, Taifa linaloongozwa na utashi wa mtu mmoja mmoja katika uongozi kuliko kuongozwa na taasisi ambazo zinafuata standards (viwango).

Nchi zinazofuata viwango, askofu akibaka na mvuta bangi akibaka, wote watashtakiwa na wote watafungwa ikiwa wana hatia. Lakini kwa Tanzania, Ruge na Chenge watadaiwa kuiba pesa na kugawana, kisha Ruge atakwenda gerezani na Chenge atabaki mtaani na bado Watanzania wanapiga makofi kuwa hatua zinachukuliwa! Tutasubiri milele, kama hakuna Standards katika hatua zetu hatutapiga hatua. Kama tukisubiri kuongozwa na sauti ya mtu mmoja hatutakwenda mbele.

Tunaendelea kujenga Taifa lenye ubaguzi mkuu na lenye aibu. Ndiyo maana leo Rais anakwenda Sengerema anahutubia mkutano wa chama chake kwa kigezo cha Urais wake lakini vyama vingine vimezuiliwa kufanya mikutano, hata ya ndani na wapo watu wanashangilia kuwa “ngoja awakomeshe wapinzani, 2020 wawe wamemalizika” Na anayesema hayo ni Mtanzania maskini ambaye hata Bima ya Afya ya uhakika hana.

Nani amesema kuwa kwa hatua hizi za Double Standards za sasa eti Mbowe anakomeshwa? Eti Maalim Seif anakomeshwa? Eti Mbatia anakomeswa? Eti Zitto Kabwe anakomeshwa? Hivi hata hiyo 2020 ikiwa Watanzania wataichagua CCM kwa asilimia 100, Zitto ataathirikaje? Mbatia ataathirikaje? Maalim ataathirikaje? Mbowe ataathirikaje?

Yani tu-assume kuwa wote si wabunge na wako mitaani tu, wataathirikaje kukushinda wewe ambaye hadi leo hujui utaajiriwa lini na nani? Au wewe ambaye umeajiriwa na mshahara wote unatumika kupandia daladala na kula lunch?

Nchi yetu inapoendeshwa kwa Double Standards (Viwango viwili au zaidi kwa jambo lile lile au linalofanana na lile lile) au kwa kuchukua hatua dhidi ya watu fulani na si wengine kwenye jambo lile lile, nchi hiyo haiwezi kupiga hatua, itakuwa inarudi nyuma kweli kweli.

 

Kwenye masuala ya Standards katika masuala ya msingi yanayohusu nchi na sheria zake, askofu ana wajibu ule ule alionao mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Rais ana wajibu ule ule alionao mama kule kijijini Kyabakari, Mwenyekiti wa chama cha siasa kinachoongoza dola ana haki na wajibu ule ule wa yule Mwenyekiti wa chama ambacho hakina dola, Shehe ana wajibu ule ule ambao anao mfanyakazi au mkulima. Sote tuna wajibu katika  (viwango) standards zetu.

Tukiendelea kwenda mbele bila Standards  tutaona baadhi ya watu wanakomeshwa na wengine wakila bata! Kwangu mimi, Rugemalila ana haki sawa sawa na Chenge na Ngeleja na Tibaijuka nakadhalika. Rugemalira ni binadamu pia, ana watoto, mke ndugu nakadhalika na wana uchungu naye.

There is no way kwamba askofu/ waziri/ mbunge fulani  yeye ni muhimu katika nchi kuliko na ana  utaratibu tofauti mbele ya sheria na haki tofauti na mtu wa kawaida. Ndiyo maana kila siku nasema na nakumbusha maneno ya Obama alipokuwa Ghana, “Africa does not need strong men, it needs strong institutions” (Afrika haihitaji watu imara, inahitaji taasisi imara).

Mfano huu wa Obama kwa baadhi ya watu wanaofikiri kinyume chake, nawapa changamoto, wale wanaoamini kuwa JPM ni Rais bora sana, anapambana na rushwa, ufisadi nakadhalika. NATAKA niwaambie kuwa kama huo uimara wa JPM hatautumia kujenga taasisi imara na akaendelea kujilimbikizia madaraka na amri na kila kitu, baada ya miaka yake mitano au kumi kwisha. Tanzania itabakia na Bunge dhaifu, Mahakama dhaifu, Serikali dhaifu, TAKUKURU dhaifu na kila kitu dhaifu.

Na hapo ndipo wale watetezi wa hoja kuwa ujenzi wa taasisi imara unahitaji watu imara, wataelimika kwamba  kiongozi imara asiyejenga taasisi imara ni sawa na mtu anayechota maji kwa kutumia tenga.

Kitendo cha kaka yangu Ngeleja nakiita cha kishujaa kwa sababu kimeivua nguo Serikali nzima, kwamba anayedaiwa mwizi anaweza kusimama hadharani na kutamba kuwa anarudisha fedha zinazodaiwa juwa za wizi na baada ya tambo zake akarejea hadi kwake na kulala huku wanaodaiwa wezi wenzie waliomuibia fedha hizo wako gerezani.

Yani ni sawa na mmeibiwa Ng’ombe, mwizi halisi mkamkamata na huku mkiwajua wale ambao mwizi alikwenda kuficha ng’ombe hiyo kwao na wao wakijua ng’ombe ni wa wizi na wakakaa na ng’ombe kwa miaka kadhaa kisha siku moja wanairudisha bila hofu na mnaipokea na mnawaacha watunza ng’ombe wa wizi wakirejea makwao huku mwizi mkuu yuko gerezani!

Nakushukuru sana kaka Ngeleja, Shujaa wangu wa leo!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles