24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 60 YA MUUNGANO: Rais Samia ahimiza falsafa ya 4R kuuenzi

Nora Damian na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili muungano uendelee kudumu Watanzania hawana budi kuitekeleza falsafa ya maridhiano, kuvumiliana, mageuzi na kujenga nchi.

Amesema kutekelezwa kwa falsafa hizo kutajenga amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu.

Akizungumza leo Aprili 26,2024 wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, amesema Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume wamejenga taifa huru, madhubuti na lenye matumaini hivyo, zawadi pekee wanayopaswa kupewa ni kuendelea kuudumisha muungano na kuyaenzi maono yao.

“Kwa msemo wa siku hizi tunasema tuwape maua yao, Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia muungano huu kwa sababu kwa miaka 60 tumeweza kulilinda taifa na kudumisha amani na utulivu.

“Tumejenga umoja na mshikamano wa kitaifa, tumeimarisha undugu na tumepiga hatua kubwa za maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kudumisha mil ana desturi zetu.

“Nawasihi ndugu zangu Watanzania katika kuuendeleza muungano wetu hatuna budi kuitekeleza falsafa yetu ya maridhiano, kuvumiliana, mageuzi na kujenga nchi yetu…haya ndiyo yataendelea kutujengea amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu,” amesema Rais Samia.

Aidha ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili kukuza tija kwa taifa.

Rais Samia amesema nchi imefikia uchumi wa kati ngazi ya chini na tathmini zinaonyesha kuna mwelekeo mzuri wa kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu na kuwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani ili kujenga uchumi na kuleta ustawi zaidi wa wananchi.

Kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha amesema serikali inafanya kila linalowezekana kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na kuwataka wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa ili kuepuka madhara.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amesema hatua ya waasisi kuwaunganisha Watanzania ilikuwa na dhamira ya kuimarisha undugu hivyo, taifa lina wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maendeleo makubwa ambayo imeyapata katika sekta mbalimbali.

Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupata sifa na heshima kubwa kimataifa kutokana na kudumu kwa muungano huku kukiwa na amani, umoja na mshikamano.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

“Tutaendelea kuwa waumini wa dhati wa muungano wetu na tutahakikisha unadumu na unazidi kuimarika kwa faida ya kizazi cha sasa na wale watakaokuja baadaye,” amesema Dk. Mwinyi.

MARAIS COMORO, BURUNDI

Akizungumza kwa niaba ya SADC, Rais wa Comoro, Azali Assoumani, amesema muungano umejenga misingi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuwapongeza waasisi kwa maono yao.

“Tanzania ni nchi ya mfano kwa amani, maendeleo na demokrasia. Sifa moja kubwa naweza kuitoa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watawala wote wamekuwa na ushirikiano wa karibu na Comoro.

“Tanzania imekuwa ni mwenyeji wa vuguvugu la kutafuta uhuru wa nchi zetu barani Afrika ikiwemo nchi yangu, viongozi waliotutangulia wamejenga misingi ya kukaribisha nchi zetu kuwa na ushirikiano wa karibu…ninaahidi kuendeleza na kudumisha ushirikiano uliopo,” amesema Assoumani.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye ambaye amezungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amesema Muungano wa Tanzania ni wa jumuiya hiyo kwa kuwa wananchi wote ni wamoja.

Marais wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tishsekedi, Rais wa Shirikisho la Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Kenya, Dk. Wiliam Ruto na Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba.

Vilevile wamo Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima, Makamu wa Rais Uganda, Jesca Alupo, Mwakilishi wa Rais wa Zimbabwe, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Adriano Afonso Maleiane, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Jenerali mstaafu James Kabarebe na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Dk. Akinwumi Adesina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles