24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wakunga watakiwa kuzingatia weledi kwenye utoaji wa huduma

*Waomba Serikali kutambua taaluma ya ukunga katika utumishi na kuboresha maslahi yao

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Wakunga na wataalamu wengine wa afya nchini kufanya kazi kwa weledi na kuongeza bidii katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.

Amesema kuwa kada zote za afya zinasimamiwa na miiko na maadili ya taaluma na miongozo iliyowekwa. “Hivyo, basi kila mmoja ahakikishe anazingatia maelekezo mahsusi ya utendaji wa kazi,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ameyasema hayo Jumapili, Mei 5, 2024 alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Mkunga Duniani na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakunga uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amesema Chama cha Wakunga kiwe mstari wa mbele katika kukemea baadhi ya Wakunga wanaofanya kazi kinyume na maadili ya taaluma zao.

Majaliwa ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu na mazingira ya kutolea huduma ikiwemo kujenga majengo mapya, kufanya ukarabati wa majengo ya zamani na kujenga nyumba za watumishi karibu na vituo vya kutolea huduma ili kuhakikisha watoa huduma wanapatikana wakati wote.

“Serikali imeweka juhudi kubwa katika kununua vifaa tiba, dawa, pamoja na magari ya kusafirisha wagonjwa ili kurahisisha rufaa kati ya vituo vya kutolea huduma na wakati inapotokea dharura,” amesema.

Amesema Serikali imeimarisha mfumo mzima wa rufaa kwa kushirikiana na wadau unaojulikana kama M-Mama.

Aidha, amesema maboresho hayo yamezingatia sana sehemu za kutolea huduma za mama na mtoto na kuhakikisha kuwa wodi za watoto wachanga na wale wenye matatizo (Neonatal Intensive Care Units) zinajengwa kwenye hospitali za Mikoa, Wilaya na baadhi ya vituo vya afya.

“Maboresho hayo yamechangia kuimarika kwa ubora wa huduma za Afya kwa kuwa yamegusa moja kwa moja mazingira ya kazi ya Wakunga na watendaji wengine wa sekta ya afya,” amesema Majaliwa.

Kwa Upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa zaidi ya asilimia 80.

“Tunashukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za afya, hususan huduma ya mama na mtoto, ambayo imetuwezesha kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80,” amesema Ummy.

Ummy amesema kuwa Serikali imeridhia maombi ya muda mrefu ya Chama cha Wakunga ya kutofautisha kada ya wauguzi na wakunga.

“Naomba nitoe taarifa kwako tumepokea maoni na ushauri wa wakunga hususan katika mafunzo ya wakunga ngazi za chini, tunayo changamoto tunaenda kuibadilisha ili tuanzishe stashahada ya Ukunga,” amesema Ummy.

Mapema, Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dk. Beatrice Mwilike, aliomba Serikali itengeneze mfumbo wa kuwawezesha wakunga kuhudumia akina mama na watoto wachanga wakati wa maafa.

“Tunaomba taaluma ya ukunga itambulike katia mifumo ya Utumishi wa Umma kwani wakunga wakihitimu bado wanaajiriwa kwa cheo cha Afisa Muuguzi ambacho kinapunguza morali ya kufanyakazi.

“Wakunga wanahitaji kujengeewa uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, athari zake kwenye afya ya uzazi, jinsi ya kuwahudumia wahanga na kuzuia matatizo yatokanayo na athari hizo. Pia kuiongeza idadi ya wakunga katika vituo vya kutolea huduma kwa kutoa ajira mahususi kwa wakunga wanaomaliza mafunzo na kuhitimu ambao bado hawaja ajiriwa.

“Kuboresha zaidi mazingira ya kutolea huduma kwa wakunga ikiwamo kuwa na nyumba karibu na vituo vya kutolea huduma ikizingatiwa kuwa huduma zao zinahitajika saa 24 na wakati mwingine ni za dharura,” amesela Dk. Beatrice.

Aidha, katika hatua nyingine, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya sekta ya Afya ambayo yamewezesha Wataalam wa huduma za Afya kufanya kazi katika mazingira bora.

Naibu Mwaklishi Mkazi UNFPA Tanzania, Melissa McNeil Barrett, alisema “Mabadiliko ya tabianchi hubeba vitisho maalum kwa wanawake na wasichana: Utafiti unaonyesha kuwa joto kali linaweza kusababisha matatizo ya ujauzito na linaweza kusababisha au kuzidisha matatizo ya afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na kuzaa kabla ya wakati na kuharibika kwa mimba.

“Lakini wakunga sio tu waitikiaji wa kwanza katika mzozo wa hali ya hewa, kama watoa huduma salama na endelevu wa mazingira, wanawakilisha pia suluhisho muhimu la hali ya hewa kwa siku zijazo.

“Kwa mfano, wanaweza kuchangia katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa kusaidia unyonyeshaji badala ya maziwa ya matiti, ambayo lazima yafungashwe na kusafirishwa.
Kwa kuzingatia hilo, mada ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga mwaka huu ni “Wakunga: suluhisho muhimu kwa mabadiliko ya tabiabinchi,” amesema.

Maadhimisho haya ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Wakunga Duniani yaratibiwa na TAMA kwakushirikiana na UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani(UNFPA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles