RAFIKI TEGEMEO WA MOI AFARIKI DUNIA

0
582

NAIROBI, KENYA


ALIYEKUWA waziri mwenye nguvu na ushawishi wakati wa utawala wa Rais wa pili wa Kenya, Daniel Toroitich arap Moi, amefariki dunia jana asubuhi.

Nicholas Kipyator Biwott (77) aliyekuwa akijulikana kama ‘Total Man’ (Mwanaume Kamili), alifariki dunia katika Hospitali ya Nairobi, ambako alikuwa amekimbizwa kwa matibabu mapema jana, lakini saa 3.30 asubuhi aliaga dunia.

Jina hilo la utani aliliasisi mwenyewe wakati akihutubia bungeni, akisema kuwa ni muhimu kwa mwanasiasa kuwa ‘mwanaume, mwanaume kamili’.

Binamu wake, Mark Chirchir aliviambia vyombo vya habari kuwa Biwott aliamka vyema jana kabla ya kuanza kujisikia vibaya.

Biwott hata hivyo alikuwa akiugua kwa muda mrefu, hali iliyomfanya awe mwathirika wa uzushi wa mara kwa mara kumtangaza kuwa amefariki dunia.

Akiwa amewahi kuhudumu kama mbunge wa Keiyo- Marakwet na Keiyo Kusini kwa kipindi cha miaka 28, hadi anafariki dunia alikuwa akiendelea na siasa akiwa kiongozi wa chama cha National Vision (NVP).

Ni hivi majuzi tu alitangaza kuwa chama chake hicho kitaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Biwott aliyezaliwa katika kijiji cha Chebior, Wilaya ya Keiyo katika Mkoa wa Bonde la Ufa, alichaguliwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Keiyo Kusini mwaka 1974 hadi Desemba 2007, wakati alipopoteza kiti hicho kwa Jackson Kiptanui wa chama cha ODM.

Kufuatia kuchaguliwa kwake mwaka 1979, Biwott alihudumu kama waziri wa nchi akisimamia Wizara ya Sayansi na Teknolojia; pia aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi na Kilimo cha Umwagiliaji.

Mara ya mwisho kuhudumu uwaziri ilikuwa 2001 akiwa Waziri wa Biashara, Viwanda na Utalii wa Afrika Mashariki wakati wa utawala wa Moi, mwaka mmoja tu kabla ya anguko la Chama cha KANU katika siasa za Kenya.

Akiitikia kifo hicho, Rais mstaafu Moi alieleza kuwa amepoteza ‘rafiki tegemeo.’

Moi alisema Total Man, kama alivyojulikana alikuwa mtumishi mwenye moyo wa kazi na mfanyabiashara mwenye akili na mhisani.

“Alianzisha miradi mingi ya kijamii kuondoa mahangaiko ya watu aliowawakilisha wa Keiyo,” alisema.

Mzee Moi alisema Kenya imepoteza rasilimali, ambayo utumishi wake ulisaidia vilivyo taifa.

Mbali ya mwanasiasa Godfrey Gitahi Kariuki maarufu kama GG Kariuki, aliyefariki wiki iliyopita, Total Man, alikuwa mtu mwingine asiyekuwa na kizuizi cha kupanda gari moja la kirais na Rais Moi.

Nick kama marafiki zake walivyopenda kumwita, atakumbukwa zaidi na wengi kama mtu mwenye nguvu kuwahi kutokea katika siasa za Kenya nje ya urais.

Hakuwa mtu wa kuunguruma majukwaani, lakini nguvu na ushawishi wake ndani ya viambaza haukupingika na ulivuma mno hadi mbali kwa masafa marefu hasa wakati wa kilele cha utawala wa kiimla wa KANU.

Waziri huyo wa zamani na mfanyabiashara mashuhuri daima hakukaukiwa na utata wakati wake wa kilele cha umashuhuri wake.

Jina lake kamwe halikuwa mbali na kila aina ya ‘uchafu na ushetani’ ulioukumba utawala wa Kanu: kuanzia ufisadi wa kiwango cha juu, rekodi mbaya ya haki za binadamu wakati wa utawala wa Moi hadi vifo vya kutatanisha vya wapinzani wengi wakuu wa utawala wa KANU.

Wakati wa kilele cha nguvu na ushawishi wake, Biwott aliogopwa mno, unapomzungumzia kwa baadhi wanaosikiliza ilitosha kuwatetemesha.

Biwott alitajwa na jasusi wa Scotland Yard, John Troon kama mtu muhimu katika kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Robert Ouko mwaka 1990.

Maofisa 10 wa serikali akiwemo Biwott walikamatwa na polisi na kuhojiwa kwa wiki mbili Novemba 1991.

Hata hivyo, uchunguzi huo wa Polisi wa Kenya ulipokamilika ulikosa ushahidi wa kumhusisha Biwott na kifo hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here