23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

UVUVI HARAMU UNAVYOSHUSHA THAMANI YA SAMAKI, UBORA WAKE

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

 SAMAKI ni kitoweo kinachotajwa kuwa na faida nyingi kwa afya ya mwanadamu. Kitoweo hiki kinapendwa na watu wa rika zote kutokana na ladha yake nzuri.

Wataalamu wa afya wanaeleza kwamba kitoweo hicho kina wa ‘utajiri’ wa mafuta yenye kiambata cha madini aina ya ‘omega 3’.

Wanasema mafuta hayo yanapoingia katika mwili wa binadamu humfanya kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kutunza kumbukumbu vizuri.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu yaani hawazeeki mapema.

Wataalamu wa lishe wanaeleza kuwa kitoweo hicho iwapo kitaliwa kwa wakati mwafaka hasa muda mchache baada ya kuvuliwa, huweza kuwa na tija zaidi kuliko kinapokaa.

 

Faida kwa wajawazito

Samaki anatajwa pia kuwa msaada kwa wajawazito kuliko nyama nyekundu.

Inaelezwa kwamba madini ya ‘omega 3’ yaliyomo ndani yake husaidia pia kutengeneza retina kwenye mboni ya macho ya mtoto akiwa tumboni pamoja na mfumo wa neva.

Pia humsaidia mama kuzuia matatizo ya kifafa cha mimba na sonono baada ya kujifungua na mara zote njia kuu ya mtoto hupata ‘Omega 3’ kutokana na vyakula anavyokula mama yake.

Watoto waliopata ‘Omega 3’ ya kutosha huonesha umakini mkubwa kuliko watoto wengine na hukua kwa haraka zaidi kuliko yule wale ambao hawakupata kiambata hicho.

 

Faida kwa watu wazima

Samaki hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na nyinginezo kwa watu wazima.

Vyanzo vinavyoleta madini hayo vinapatikana katika samaki na mafuta yake, hasa wale wenye mafuta mengi kama vibua, sato, salmon, sangara na dagaa.

Madini hayo pia yapatikana kwenye juisi, mikate, mboga za majani, mayai, alizeti, mafuta ya samaki na vyakula jamii ya mbegu.

 

Faida zingine

Virutubisho kama vitamini D na B2, ndio madini ya chuma, zinc, iodine, magnesium na potassium hupatikana katika kitoweo hiki.
Mtu anayekula samaki anapata faida nyingi mwilini mwake kwani husaidia pia kuyeyusha damu na kuifanya iwe nyepesi, huilinda mishipa ya damu isiharibike, huzuia damu kuganda na kushusha shinikizo la damu.

 

Tishio la uvuvi haramu

Pamoja na uzuri wa kitoweo hicho, sasa inaonekana kuwa tishio kwa afya za walaji nchini.

Hiyo ni kutakana na kuwapo kwa baadhi ya wavuvi wasiokuwa waaminifu, wanaodaiwa kuvua kwa kutumia baruti.

Hali hiyo inawafanya samaki kuwa na athari kwa afya za walaji kuliko faida kwa maisha yao ya baadae.

Kwa mujibu wa wataalmu, mlipuko mmoja unatosha kuua samaki na viumbe hai vilivyo umbali wa mita mraba 20 na kuua samaki wapatao 400 kwa wakati mmoja.

Hali hiyo inatajwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira chini ya bahari ambayo huwezesha samaki kuzaliana na kuongezeka.

Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam, sasa wamelazimika kubandika mabango yanayotoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya samaki hao na jinsi ya kuwatambua.

Meneja wa soko hilo, Eliakimu Mniko anasema wanalazimika kutoa elimu kwa sababu wananchi wengi hawajui kumtofautisha samaki aliyevuliwa kwa njia halali na haramu.

“Wengi hawajui matokeo yake wanajikuta wakila samaki waliovuliwa kwa sumu na kupata madhara kiafya,” anasema.

 

Tani 1.5 zakamatwa

Ofisa Uvuvi wa soko hilo, Victoria Mwandike anasema mwishoni mwa mwaka jana walikamata zaidi ya tani 1.5 za samaki ambao walivuliwa kwa njia ya milipuko walipofanya msako maalumu sokoni hapo.

“Samaki hao walikamatwa wiki iliyopita katika msako maalumu kabla ya kuanza kusambazwa kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kuuzwa, tayari watuhumiwa walifikishwa mahakamani kama uongozi wa soko ulivyokueleza,” anasema.

 

Mikakati ya soko

Anasema wanampango wa kuhamasisha samaki wanaovuliwa katika Bahari ya Hindi waanze kuuzwa katika mabucha maalumu ya samaki badala ya mitaani kama ilivyo sasa.

 

“Uongozi wa soko upo kwenye mchakato wa kupendekeza hatua hiyo ili kuzuia uuzwaji holela wa samaki kama wale wanaouzwa mitaani hasa kwenye vituo vya mabasi,” anasema na kuongeza;

“Bado tunahimiza Watanzania kuwa makini kwani wavuvi wasiokuwa waaminifu wanaendelea kuvua kwa njia haramu.

Anasema ni vema pia mamlaka zinazohusika na uuzwaji na usimamizi wa milipuko hasa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Wizara ya Kilimo na Mifugo na Jeshi la Polisi wadhibiti upatikanaji holela wa bidhaa hiyo ili tutokomeze uvuvi haramu ambao kwa sasa umekithiri katika Bahari ya Hindi.

“Kwa sababu wavuvi baada ya kununua milipuko hiyo huipooza kwa kuchanganya na kemikali wanazozifahamu wao kisha huitumia kwa kuvua samaki. Zipo athari nyingi za uvuvi haramu lakini kikubwa eneo hilo hupoteza uhalisia wake kwa zaidi ya miaka 100 na baada ya hapo ndiyo huanza kurejea katika hali ya kawaida, jambo ambalo limesababisha hata samaki siku hizi kupatikana maeneo ya mbali tofauti na zamani,” anasema.

 

Jinsi ya kumtambua samaki wa sumu

“Tunalazimika kutoa elimu kwa jamii ili kujua tofauti zilizopo kati ya samaki hawa. Kwanza samaki aliyevuliwa kwa njia ya mlipuko unapomning’iniza juu huchuruzisha damu nyingi tofauti na yule aliyevuliwa kwa njia ya kawaida,” anasema.

Anaongeza kuwa samaki aliyevuliwa kwa mlipuko huwa ametoa mno macho yake nje lakini aliyevuliwa kawaida huwa ameyatoa kidogo.

Pia ukitazama uti wa mgongo wa samaki aliyevuliwa kwa mlipuko utakuta umevunjika tofauti na aliyevuliwa kawaida.

Njia nyingine za kumtambua ni pindi unapompasua kwa ndani utakuta utumbo wake unaonekana kama umepasuka tofauti kabisa na wale wanaovuliwa kawaida.

 

Waingizwa sokoni feri

Mniko anasema kipindi cha nyuma samaki hao walikuwa wakiingizwa hadi katika soko hilo na kuuzwa kwa wachuuzi hali ambayo iliwalazimu kufanya msako.

“Katika msako huo tumefanikiwa kukamata wafanyabiashara 13 hadi sasa ambao walikuwa wakiuza samaki kwenye kizimba namba tano hapa sokoni, bado tunaendelea kusaka wengine,” anasema.

Anasema kesi hiyo imeanza kusikilizwa katika Mahakama ya Sokoine Drive tangu Desemba 30, mwaka jana.

“Wapo pia mama lishe watatu ambao nao walikamatwa wakiwa na samaki waliovuliwa kwa kutumia baruti na wamechukuliwa hatua za kisheria,” anasema.

 

Mniko anasema kuwa wanajitahidi kudhibiti uingizwaji wa samaki hao Feri, lakini hajuia katika masoko mengine hali ipoje.

“Kwa kuwa wavuvi hao hawatumii gharama zozote mara nyingi huuza samaki wao kwa bei ya chini hali hiyo inafanya samaki waliovuliwa kihalali kudoda.

“Hii inachangia pia soko kukosa mapato na wafanyabiashara nao kuyumba.

Hali ya mauzo

Kuhusu hali ya upatikanaji wa samaki na makusanyo ya soko hilo kwa mwezi, anasema hutegemeana na msimu ulipo.

“Biashara ya samaki haitofautiani na ile ya madini, huwa ina msimu na mara nyingi hutegemea hali ya hewa iliyopo.

Samaki hupatikana kwa wingi katika kipindi cha joto kwa mfano Oktoba hadi Januari.

Mawaziri saba wapanga mikakati

Kukithiri kwa uvuvi haramu hasa wa kutumia mabomu kumesababisha mawaziri wa wizara saba kukutana ghafla ili kujadiliana namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

Mawaziri hao ni January Makamba (Muungano na Mazingira), Dk. Charles Tzeba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi), Dk. Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani ya Nchi).

Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Seleman Jafo (Naibu Waziri wa Tamisemi) wakati Wizara ya Uchukuzi iliwakilishwa na Katibu Mkuu, Dk. Leonard Chamulilo.

Makamba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali za bahari na samaki, lakini zinaathiriwa na uvuvi haramu.

“Tumejadiliana kwa kirefu na tumetafakari hatua za kuchukua ili kukomesha tabia hii. Kikao kilikuwa cha kazi, mikakati na mbinu za kukabiliana na watu wanaofanya uvuvi haramu,” alisema Makamba.

“Shughuli hii ni vita, lazima tupambane. Nguvu ya Serikali iliyopo hapa (mawaziri) itawashukia wahusika pasipo kujua,” alisema Makamba.

Naye Dk. Tzeba alisema mazingira ya bahari yanazidi kuharibika na kwamba asilimia 40 ya matumbawe ya samaki yameathiriwa na uvuvi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles