29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

MWAKA MPYA WA WACHINA NA ZIMWI ANAYEKULA WATU

 

NA MWANDISHI WETU

KWA Tanzania na nchi nyingine duniani ni kawaida kuona tarehe moja ya Januari wakifurahia mwaka mpya.

Utaratibu huu umekuwa tofauti kwa jamii ya China ambao wao wamekuwa wakifurahia mwaka mpya kila ifikapo Januari 14 huku miaka yao ikiwa na majina maalumu.

Hapa nchini, taasisi ya Confucius iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na lengo la kueneza lugha ya Kichina, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaeneza utamaduni wa taifa hilo.

Profesa Zhang Xiaozhen, anasema ni azma ya nchi ya China kuifanya dunia kuwa mahali pa kuishi kwa staha na kujivunia utamaduni wa jamii mbalimbali.

Anasema katika azma hiyo, nchi hiyo ilianzisha Taasisi ya Confucius ambayo kwa sasa ina matawi zaidi ya 555 duniani kote.

“Confucius ni jina la Mchina aliyezaliwa mwaka 551 kabla ya masihi, alikuwa mwalimu, mwanasiasa, mhariri wa maandishi mbalimbali ya Kichina na zaidi mwanafalsafa ambaye aliijenga China akiileta pamoja na kuwa moja kama ilivyo leo.

“Msisitizo wake mkuu katika maisha yake ilikuwa ni uadilifu, usahihi wa kufanya mambo, haki na usawa katika uhusiano wa kijamii.

“Mojawapo ya nguzo kuu za Confucius ni uadilifu katika kazi na maisha ya jamii na heshima miongoni mwa wanajamii,” anasema.

 

Miaka kupewa majina

Anasema kuwa sherehe za kiutamaduni, zinazolenga kuuenzi utamaduni wa kuita miaka majina na hivyo kuielekeza jamii katika kutenda yaliyo mema kwa ajili ya maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla.

“Huu ni mwaka wa jogoo na kama zilivyo jamii nyingi za Kiafrika, mnyama au ndege huwa alama ya koo kadhaa, kupitia alama hizo koo huamini na kushikilia mila fulani.

“Mwaka wa Jogoo unahimiza kazi lakini pia unahimiza kutenda kwa haraka, kwa usahihi na kwa wakati muafaka.

“Chimbuko la sherehe ni kisasili kilichoanza miaka 2,000 kabla ya Masihi. Shamrashamra hizi pia huashiria kuanza kwa sherehe za msimu wa kuchipusha majani, baada ya baridi na nchi kutokuotesha chochote.

“Matumaini ya maisha mapya  huja baada ya kuona miti na mimea inatoa majani na maua yanaanza kuota,” anasema.

Akifafanua zaidi juu ya utamaduni huu, anasema Wachina walikuwa wakiogopa zimwi lililokuwa likija na kula watu usiku.

“Usiku wa kuamkia mwaka mpya, zimwi lilikuwa likija na kujichagulia watu na kuwala kisha linatoweka wale waliosalimika waliishi kutoa simulizi kila mwaka.

“Lakini zaidi walikuwa wakitoa sadaka kumshukuru Mungu kwa kuwanusuru na zimwi hilo, hivyo watu wakagundua kuwa kumbe lilikuwa likitokea mara moja kwa mwaka… Linaweza kuja usiku likafanya vurugu, likala watu na kutokomea milimani alfajiri,” anasema.

Anasema kuanzia hapo, kila mwishoni mwa mwaka watu walijifungia ndani kuhofia zimwi. “Lakini hii ilimaanisha kuwa wawe na chakula cha kutosha, pia wasilale bali kila mwanafamilia ashiriki katika kutoa sadaka ya kupona.

“Hivyo, watu wakajenga utamaduni wa kukaa macho siku ya mwaka mpya… hadi leo imekuwa kama utamaduni kukesha kila ifikapo usiku wa mwaka mpya,” anasema.

UDSM kupitia taasisi ya Confucius, kimekuwa kikishirikiana katika kueneza utamaduni wa taifa hilo hapa nchini ikiwamo kuadhimisha mwaka mpya wa Kichina na kutumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kuchapa kazi, kuwa waaminifu na maadili ili kujiletea maendeleo.

“Katika maadhimisho haya, tutafakari kuhusu maendeleo ya utamaduni wetu wenyewe na hasa kuienzi Lugha ya Kiswahili,” anasema Profesa Aldin Mtembei ambaye ni Mkurugenzi mwenza wa taasisi hiyo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles