24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

UTAWALA USIBWETEKE NA SIFA KUTOKA NJE YA NCHI

NA HILAL K SUED


Kama kipo kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimechangia katika uzorotaji wa utendaji ndani ya utawala wowote, basi kitu hicho ni kubweteka kwake kutokana na sifa kutoka nje ya nchi.

Sifa zinazoporomoshwa kwa serikali kutoka baadhi ya serikali na taasisi za fedha kutoka nje huzifanya tawala mbali mbali kujisikia unafanya vizuri hivyo hakuna haja ya kufanya zaidi ya hapo, kitu ambacho si sahihi.

Wananchi wenyewe ambao ni wapokeaji wa huduma za utawala kama vile elimu, afya maji na pia katika kujikwamua kutoka umasikini ndiyo mahakimu wazuri zaidi kwani methali isemayo ‘siri ya mtungi aijua kata’ ni kielelezo tosha kwa ninalolisema.

Mara kadha, wakati wa usomaji wa bajeti ya serikali Bungeni tumekuwa tunasikia upigaji makofi na ugongaji meza unaofanywa na Wabunge kila pale Waziri wa Fedha anapotaja nchi au taasisi ya fedha kutoka nje zinazotusaidia na sifa wanazotumwagia katika hatua za maendeleo nchi inavyopiga.

Sipingi sifa kutoka nje, lakini ni vyema tukaangalia hatimaye zisitulemaze – badala yake ziwe chachu katika jitihada za kujitegemea sisi wenyewe. Tusisahau nchi yetu ina maliasili nyingi, hususan madini ambayo yangeweza kutukwamua kutoka kwenye dimbwi la umasikini tulio nalo.

Swali hapa ni kwanini serikali yetu inapuuza maoni ya wananchi wanaolalamikia hali ngumu ya maisha, malalamiko ambayo hata makada wa chama tawala nao siku hizi wanapambana nayo wanapotembela huko vijijini, na badala yake kukumbatia sifa kutoka nje?

Lakini kumekuwapo sifa nyingine kutoka nje ambazo zinatia mashaka sana – hasa zile kutoka taasisi, majarida na watu binafsi. Miaka minne iliyopita katika Awamu ya Nne jarida moja la Marekani – ‘African Leadership Magazine Group’ lilimtunikia Rais Jakaya Kikwete tuzo ya kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo barani Afrika kwa mwaka 2013.

Tuzo hiyo ilipokelewa na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe kwa niaba ya Rais Kikwete ambaye baadaye aliikabidhi kwa wananchi wa Tanzania akisema bila wao asiingeipata tuzo hiyo kwani inatokana na mchango wao (wananchi) katika maendeleo ya nchi.

Na Kikwete mwenyewe angekuwa dhati iwapo angesema kwamba anawakabidhi Watanzania Tuzo hiyo kutokana na uvumilivu wao mkubwa wanaouonyesha mbele ya matatizo makubwa wanayokabili.

Kufuatana na jarida hilo tuzo hiyo hutolewa kwa viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao na ilitolewa kwa Rais Kikwete kutokana na mwelekeo wake usiokuwa wa kawaida na wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya utawala bora.

Jarida liliongeza kuwa Kikwete “amepata sifa kubwa kimataifa na leo ameifanya Tanzania kuwa nchi ya kuigwa mfano kama kituo cha uhakika cha uwekezaji kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa katika sera na mifumo ya uchumi.”

Nilijiuliza sana jarida hilo lilitumia vigezo gani hasa kumpata ‘mshindi’ wa mwaka ule lakini baadaye nilijibiwa na jarida hilo hilo. Lilisema Kikwete alikuwa chaguo kubwa na la kwanza la wasomaji wa jarida hilo ambao walipiga kura kupitia njia mbali mbali za mawasiliano za jarida hilo.

Nilihangaika sana kutaka kujuwa ni watu gani hao waliopiga kura hizo, iwapo wamo pia Watanzania wa kawaida miongoni mwao, au ni watu wa nje tu wanaowakilisha wale waliowekeza hapa nchini hasa katika madini, gesi asilia, makampuni ya uwindaji na kadhalika, lakini sikuweza kujua.

Kwani kama ni wawekezaji wa madini, hilo sasa linaeleweka baada ya Rais Johm Magufuli kuibua wizi mkubwa wa madini kutoka kwa wawekezaji hao, wizi uliokuwa ukifanywa kwa miaka mingi. Au kupewa ardhi zilizoporwa kutoka kwa wanavijiji?

Laiti Watanzania wa kawaida wangeweza kupewa fursa ya upigaji kura wa jarida hilo, nadhani matokeo yangekuwa tofauti sana. Kama nilivyosema hapo mbele, watu wa nje hawajui vilio vya Watanzania kwani mara kadha runinga zimekuwa zikionyesha malalamiko ya wanavijiji sehemu mbali mbali nchini wakilalamika kuporwa ardhi yao.

Halafu hao watu wa Tuzo ile walisema eti Kikwete aliweza “kusimamia uchumi ambao umekua kwa wastani wa asilimia saba kwa miaka yote ya uongozi wake.” Hivi hawa watu wanaishi dunia gani? Huo uchumi umekua ukikua kwenye mifuko ya mafisadi na wawekezaji waliokuwa wakilelewa na serikali.

Wale akinamama na watoto waliopoteza maisha kwa kukosa dozi ya malaria walikua wanaishi kwenye uchumi gani? Wale watoto wanaokaa chini bila madawati waliongozwa na serikali ipi? Halafu wakifeli katika mitihani waziri husika anasimama Bungeni na kutoa tamko kwamba serikali inarekebisha viwango vya ufaulu na hivyo wajisikie wamepasi.

Kwa upande wangu, tuzo ninayoiamni ya kuwatunukia viongozi bora barani Afrika ni ile ya kila mwaka ya Mo Ibrahim Award of Leadership Excellence ya bilionea wa Sudan ambaye yeye binafsi hana haja ya kitu chochote kutoka nchi yoyote ya Afrika, isipokuwa tu kusisitiza utawala bora, kuheshimu vipindi vya utawala, na jitihada za dhati katika kusaidia uchumi wa nchi yake.

Kwa kuwa Tuzo ya Mo Ibrahim hutolewa kwa marais waliostaafu, hakuna uwezekano wowote kwa mtoa tuzo kubeba tuhuma kwamba anataka upendeleo wowote kutoka kwa rais anayemtunuku.

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Hapo umenena. Mzungu jarida lake ni kuupata mwanya mkubwa nchini kwa kuwa hatuna sheria ngumu , kali , zenye msimamo hata. Viongozi wote wawili wamepata sifa sababu wanatumika na mataifa haya makubwa. Wanajua hasa hatuna demokrasia. Watu wanauawa kama wanyama. Serikali haina majibu wala haijali. Upinzani upo juu kuhakikisha tunajirudi kwenye msitari, lakini Serikali yetu na utawala hauna uwezo wa kupima haya hata. Wanajua ni vita ya sisi kwa sisi, wanatumia fursa hiyo kujikita zaidi wakijua tunazidi kuangamia tukisani mikataba mibovu bado, huku hatuna uzalendo, muungano na tumeshindwa kujiokoa kwa haya. Ni Aibu sana kwa Taifa lettu, kama unajielewa, unajiuliza sifa hizi za Wazungu je ziko wapi? mbona sisi wenye nchi hatuzioni? Hii ni propaganda kubwa inayotumika na mataifa makubwa kuja kwa kuwasifia viongozi wasiojitambua nia zao, na kukipata kile watakacho. Ubepari ni unyama. Kokote Duniani hakuna ubinadamu na undugu kama Afrika. Hata wakikaa Afrika sababu kwenye damu zao haupo, hawatakuwa. Watanyonya tu. Tatizo Kwetu Waafrika tunakwenda mbelehatua moja tunarudi nyuma hatua tano. Tulikwenda utumwani kwa njia hizihizi. Na tunaingia ukoloni mambo leo kwa mfumo uleule. Sababu, wengi bado werevu mdogo kujua mbinu gani wanazitumia. Mtu moja anauza Taifa kwa kusifiwa nao. Wanajua, wanaingia kivyao. Nakusifu ndugu Hilal, Je wangapi Tanzania wanaelewa hili. Je unauwezo gani kuwaelimisha, na kuitisha vikao watu wengi wakaelewa. Jifunge mkanda jitolee kulisaidia Taifa. Tanzania imechaguliwa kuchezewa na Mataifa. Naijua hii. Inauma. Mimi ni mdogo, lakini najua sababu niko nao. Wanajitamba kutengeneza pesa nyingi Tanzania kuliko kwingine kote. Wameungana Ulaya, Marekani china nia, Tanzania iangukiwe kwao kabla watu hawajaamka. Lisu, Mbowe, Zitto, Msigwa, CCm wa nzega Bashe, Lema, msigwa, Padre aliyejitolea wa Katoliki mwanza, Askofu wa cct, Askofu wa Dar anayetaka kununua ndege, Waislau wa mwamko waliowekwa ndani, Mboye, Msigwa, Lema, ndugu Lazaro Nyalandu najua upo CCM bali unaelimu tofauti na wengi wa CCM, Halima Mdee, Na yule anayepigwa vita sana na Wasira,Mkiungana, weka rangi ya bendera chooni, pigania kwa Umoja Tanzania. Tutaigeuza nchi.,
    MUNGU IEPUSHE NCHI YANGU HUKO INAKOKWENDA. MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE.MUNGU IBARIKI AFRICA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles