22.6 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

NAPE, HII NDIO SHERIA ULIYOITETEA AU TUISUBIRI NYINGINE?

BAADA  ya kasi ya  ajabu ya kuvionya na kuvifungia  vyombo vya habari, nimeyakumbuka  maneno  yaliyotamkwa  bungeni na aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye. Nape alitamka maneno haya wakati akitoa hoja ili kuwashawishi wabunge waiunge mkono sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari mwaka 2016 ambayo alikuwa ameiwasilisha.

Katika sehemu ya hotuba hiyo alisema; “Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichofanya kwenye Muswada huu na hii ni nia ya dhati ambayo nimeieleza hadharani, si mara moja, si mara mbili, ni kwamba tunataka tupunguze control (udhibiti) ya Serikali kwenye uendeshaji wa vyombo vya habari, badala yake tuchukue jukumu hilo kulipeleka kwenye Baraza Huru la Wanahabari ambalo litaundwa na wanahabari wenyewe… Maana yake ni moja tu kwamba tunapunguza mamlaka ya waziri na yamepunguzwa kwa kiasi kikubwa mno.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu tuliouwasilisha, tumemwachia  Waziri makosa mawili tu; usalama wa Taifa na afya ya jamii… Makosa mengine yote tumewapelekea Baraza la Habari washughulike nayo.”

Kwa mujibu wa Nape, sheria hiyo aliyokuwa anaipigia debe ingeshughulika na taaluma ya mtu mmoja mmoja. Alibainisha kuwa “kwa sheria hii, tutashughulika na mwandishi na taaluma yake badala ya kufungia chombo kizima.”

Leo naomba kumuuliza Nape kama sheria hiyo aliyokuwa akiisema ndio hii hii ambayo Serikali imekuwa ikiitumia kufungia vyombo vya habari kwa kasi ya kustaajabisha au kuna sheria nyingine ambayo inatumika?

Tangu kupitishwa kwa sheria hiyo ambayo tuliaminishwa kuwa sasa  suala la vyombo vya habari kufungiwa itakuwa ni historia, Serikali imeweka rekodi ya kufungia vyombo vingi vya habari kuliko ilivyowahi kutokea siku za nyuma.

Hii ni tofautui kabisa na ahadi ya Nape kuwa sheria mpya itapunguza fungia fungia. Ndio maana namhoji leo Nape kama sheria hii inayotumika ni ile aliyoipigia debe bungeni ikapitishwa au tuisubiri nyingine?

Nape alisema kuwa sheria hiyo imemwachia waziri makosa mawili tu ya kufungia gazeti; kuhatarisha Usalama wa Taifa na Afya ya Jamii.

Tunaweza kutofautiana katika tafsiri ya mambo hayo lakini haiingii akilini kuwa makosa (kama kweli kuna makosa) yaliyofanywa na magazeti yaliyofungiwa  kweli yamehatarisha usalama kipo kipimo cha kuonyesha hilo.

Kama habari zilizoandikwa na magazeti hayo kweli zingekuwa hatari kwa Usalama wa Taifa, ni dhahiri kuwa madhara yangeonekana wazi kwa sababu magazeti yalifungiwa baada ya habari hizo kuandikwa. Labda Serikali ituambie ni kwa namna gani habari zile zimehatarisha Usalama wa Taifa.

Hata kama kwa hatua ilizochukua dhidi ya Mwanahalisi na Raia Mwema zinalenga kurejesha nidhamu katika utendaji, hilo litawezekana vipi wakati watendaji wenyewe wamefungiwa kutenda?

Taarifa karibu zote zinazotolewa na Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu kufungiwa vyombo vya habari zinaeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya wahusika kuonywa mara nyingi. Jambo hili limenifanya nifikiri ni nini kimebadilika kiasi cha vyombo vya habari, ambavyo miaka kadhaa iliyopita havionekani  kuwa na makosa mengi  kiasi hiki, leo vimeanza kufanya kazi vibaya kiasi cha kuonywa mara nyingi kiasi hicho na Serikali?

Iwapo hiki kinachofanyika ndio kupunguza ‘control’ ya Serikali kwa vyombo vya habari, sijui hali ingekuwaje iwapo hii ‘control’ isingepunguzwa na sheria mpya!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles