24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga Azam nani kuwa mtamu?

Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM

WABABE wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba, Yanga na Azam, zinatarajia kushuka dimbani leo maeneo tofauti ya nchi kusaka pointi tatu muhimu.

Simba itashuka dimba la Sokoine jijini Mbeya kuumana na wenyeji Mbeya  City ,  Yanga itakuwa mwenyeji wa Namungo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam , wakati Azam itakuwa ugenini mkoani Kagera kuumana na wenyeji wao Kagera Sugar, mchezo utakaochezwa dimba la Kaitaba, Bukoba.

Timu zote hizi zinatarajia kushuka dimbani kibabe, kila mmoja akikumbuka kile alichovuna katika michezo  iliyopita, lengo kuendelea kuweka heshima.

Simba inahitaji pointi tatu, ikitaka kujiwekea mazingira mazuri ya kutangaza ubingwa mapema, wakati Yanga na Azam kila mmoja anafukuzia nafasi ya pili.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Simba inaongoza ikiwa na pointi 75, Azam ya pili na alama 58, wakati Yanga ikiwa nafasi ya tatu na pointi 56, zote zikicheza mechi 30.

Kwa idadi hiyo ya pointi, tayari Simba imewaacha mbali wapinzani wake, licha ya kwamba ikipoteza mechi kadhaa kati ya nane zilizobaki, inajiweka  katika wakati mgumu na haitaweza kutangaza ubingwa hadi dakika za mwisho.

 Hali hiyo inaashiria kwamba, katika michezo ya leo, vigogo hao, kila mmoja anahitaji kuweka heshima na zitakuwa mechi za kusikiliziana matokeo.

Kazi kubwa ipo kwa Yanga na Azam wanaopigania nafasi ya pili, ikumbukwe zimetoka kutoka suluhu Uwanja wa Taifa.

Ni mechi zitakazokuwa na ushindani mkubwa, ukizingatia pia timu wanazokutana nazo zinahitaji pointi tatu kwa hali na mali, kutokana kasi ya ligi hiyo kila mmoja akimpania mwenzake.

Kati ya timu hizo, Simba  inaoneka kuwa na kibarua  kigumu zaidi, kwa sababu inakutana na Mbeya City,  iliyopo katika mstari hatari wa kushuka daraja, huku ikiwa imetoka kufungwa  bao 1-0, katika mchezo uliopita na Alliance kwenye uwanja huo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Mbeya City ipo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 30, zilizotokana na michezo 30, huko Kocha Mkuu wa timu hiyo, Amri Said akitaka kuepuka kunyooshewa vidole kutokana na uhusiano wake na Simba.

Pia Wanamsimbazi hao ambao wametoka kupata ushindi mnono   wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui,  watahitaji kuendeleza ushindi utakaowasaidia kuongeza morali kuelekea mechi yao na Tanzania Prisons.

Ili kutangaza ubingwa, Simba inahitaji pointi nane, hivyo ikifanikiwa kuvuna sita , itabakiwa na mbili ambazo inaweza kuwa rahisi kwake kuzipata kwakua itacheza nyumbani.

 Upande wa Yanga, kibarua ilichonacho, pamoja na kufukuzia nafasi ya pili, inatakiwa kurejesha furaha ya mashabiki wao, baada ya kuumizwa na matokeo mechi mbili zilizopita.

Wanajangwani hao walitoka suluhu na Azam,  lakini kabla ya hapo walibanwa sare  kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Namungo inayokutana na Yanga, ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 54, baada ya ushindi wa mchezo uliopita dhidi  Kagera Sugar, ulichezwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Azam inapata presha kubwa kutoka kwa Yanga ndiyo maana inapigana kufa au kupona kupata ushindi ili kuwakimbia mbali Wanajangwani.

Nahodha wa Simba, John Bocco, ametamba kuwa uwezo wa kuchukua pointi sita Mbeya ni mkubwa kutokana na morali waliyonayo.

Alisema wakipata ushindi katika mechi hizo watakuwa wamemaliza kazi na itawaongezea ‘mzuka’ kuelekea mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho(ASFC) dhidi ya Azam, ikatayochezwa Julai Mosi, mwaka huu.

“Mawazo yetu yote ni ushindi, tunajua ugumu wa mechi za Mbeya, lakini  tumejipanga kukabiliana na chochote kitachotokea ili kupata pointi sita,” alisema Bocco.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, alisema kitu kilichomuangusha katika  mchezo na Azam, ni safu ya ushambuliaji ilishindwa kufunga mabao licha ya kupata nafasi.

Alisema suala hilo ameshalifanyia kazi katika mzoezi ya siku mbili, anatarajia kuona mabadiliko baada ya kukaa na wachezaji wake na kuwaeleza wanachokiwa kufanya.

“Ushindi katika mchezo na Namungo ni muhimu kwetu, nimezungumza na wachezaji kila kitu na kuwaeleza tunakutana na timu bora, ni lazima kupambana,” alisema.

Michezo mingine inayotarajia kupigwa leo, Alliance FC itaikaribisha Polisi Tanzania Uwanja wa CCM Kirumba,  wakati Biashara United itakuwa mgeni wa KMC, dimba la Uhuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles