26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Profesa Janabi aeleza sababu magonjwa ya moyo kuongezeka

Na AVELINE KITOMARY
-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, amesema magonjwa ya moyo na yasiyo ya
kuambukiza yataendelea kuongezeka kutokana na kuendelea kukua kwa uchumi.


Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu jana viwanja vya Mwembe Yanga, Dar es Salaam wakati wa
maonyesho ya One Stop Jawabu yanayolenga
kusogeza huduma kwa wananchi, Profesa
Janabi alisema chanzo cha kuongezeka kwa
magonjwa ni mfumo mbaya wa maisha na
kutokufanya mazoezi.


“Magonjwa ya moyo, kisukari, saratani
labda nikwambie tu yataongezeka zaidi kwa
sababu hii, na naomba mnielewe vizuri, kadiri uchumi wa nchi zetu unavyokwenda juu, na haya magonjwa yanakwenda juu kama hatutachukua hatua.


“Kwa sababu watu sasa hivi wana uwezo wa kununua chakula kingi zaidi, lakini bahati mbaya chakula ni kipi hilo ni suala jingine kabisa, watu wengi sasa hivi hata kama hana usafiri wake mwenyewe kuna bodaboda, daladala na bajaji, kwahiyo yale mazoezi yamepungua sana,” alisema Profesa Janabi.


Alisema kuwa maisha ya watu wengi yamekuwa marefu kutokana na kuwepo kwa vituo vya afya na hospitali.

“Ina maana mtu akianza kunywa dawa hapa mimi nazungumza kama daktari sio Mungu, kwamba unaongeza maisha yake, sasa kadiri umri utakavyokuwa mkubwa na yale magonjwa ya watu wazima tutakutana
nayo,” alisema Profesa Janabi.

Alibainisha kuwa mazoezi yana nafasi kubwa katika kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo moyo, hivyo watu
wakizingatia itawasaidia.


“La pili ni hili la mazoezi, huwa natoa mfano mimi nilikuwa nakaa Kinondoni nasoma Azania, asubuhi tukiangalia ule mkondo
kama maji yako kidogo mnakatiza na kwenda shule, sasa hivi watoto wangu hawatembei, asubuhi school bus, kama haipo watachukua bodaboda au bajaji, kwahiyo mazoezi yamepungua sana.

“Lakini lingine ni elimu, kwamba kama mgonjwa wa presha anatumia dawa mara moja na kufikiri kuwa atapona, ni kwamba sisi upande wa sekta ya afya tunatakiwa kuongeza nguvu ili kuelimisha na tusiongeze nguvu sana kwenye tiba, yaani tiba na kinga ziende sambamba,” alifafanua Profesa Janabi.


Alisema kuwa ni vyema sekta za afya zikawekeza zaidi katika kutoa elimu kwa watu ili kuweza kujikinga kuliko kupata tiba.

“Kwahiyo haya magonjwa yataongezeka na kwa bahati mbaya ni ya nchi zinazoendelea na sisi tumo kwenye kundi, ni kujua tu ni jinsi gani sasa tunaweza kutoa elimu za kinga zaidi,” alisema.

Aliongeza kuwa ni vyema Watanzania kuzingatia upimaji ya afya kwa hiari ili kujua afya zao mapema.

“Watanzania wengi hatuna tabia ya kupima afya, lakini upimaji wakati mwingine ni gharama kidogo, sasa inapotokea huduma za bure wagonjwa wengi ndio wanapatikana kuliko kawaida kwa sababu moja, anachukulia
kuwa ngoja tu nikacheki afya yangu.


“Na kwa bahati mbaya magonjwa ya moyo hayatoi dalili mpaka pale hali inapokuwa mbaya, hivyo ni bora watu wakaelimishwa kuhusu chakula na unywaji wa dawa, na tumekuja na dawa nyingi sana za kuweza kuwasaidia za kuanzia na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kunywa dawa,” alibainisha Profesa Janabi.

Alitoa wito kwa watu kupata bima ya afya ili kurahisisha gharama za matibabu ambayo ni bei ghali.

“Lengo la Serikali ni kila mtu awe na bima, kwa wengi wetu tukikata bima, kwa wale wachache Serikali ikiingilia, ile dhana na afya njema kwa kila mmoja itaweza kutimizwa,” alisisitiza Profesa Janabi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles