25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Aina za kazi zinazosababisha maumivu ya mgongo

Na AVELINE  KITOMARY

HUENDA imekuwa  ni jambo la kwaida kukuta mtu anapofanya kazi hasa ikiwa inayomlazimu kukaa, basi hufanya hivyo kwa muda mrefu bila kujipa muda wa kusimama kidogo kunyoosha mgongo.

Lakini je, ni wangapi wanafahamu au kufuatilia madhara ya kukaa muda mrefu? Inaweza isiwe rahisi kufahamu kwa sababu madhara yake huwa hayajitokezi kwa haraka.

Wataalamu wa afya wanasema ili mtu kuepuka madhara mbalimbali na kuwa na afya njema, ni lazima awe na kiasi katika maisha yake.

Nikisema kuwa na kiasi namaanisha kufanya kazi kwa kiwango cha uwezo wako na hata ulaji uzingatie vigezo vinavyotakiwa.

Asilimia kubwa ya wanadamu katika maisha yao kuna wakati wanakumbwa na matatizo ya migongo, shingo, kiuno na maumivu ambayo huenda hadi kwenye mikono.

Wengine hulalamika kuwa na ganzi, kukosa  nguvu na wakati mwingine kuweza kudondosha glasi kwenye mikono au hata kuhisi maumivu, kupata ganzi na misuli kubana miguuni.

Daktari Bingwa wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamau, kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Dk. Laurent Lemery, anaiambia MTANZANIA kuwa tatizo hilo limekuwa likiwapata watu wengi zaidi katika jamii.

Dk. Lemery anabainisha kuwa tatizo hilo limegawanyika katika sehemu mbili ambayo ni maumivu yanayotokea muda mfupimfupi (Acute back pain) na yale yanayotokea muda mrefu (Cronic back pain) ambayo yanaweza kudumu kwa zaidi ya wiki tatu na kuendelea.

SABABU

Watu wengi hujiuliza sababu za kupata matatizo hayo huku kila mmoja akiwaza lake.

Dk. Lemery anataja sababu ya kwanza ya hali hiyo ni kutokana na shughuli zinazofanywa kila siku, ikiwamo mtindo usio bora wa maisha.

“Kwanza, ni kukaa kwa muda mrefu, utakuta mtu anakaa bila kusimama kwa muda wa saa tatu halafu hakai kwa usahihi.  Kuna kukaa kwa kupinda mgongo ili mtu atafute unafuu, kukaa kwa aina hiyo husababisha madhara makubwa.

“Kwa kawaida pingili za mgongo ziko 33, na kati ya pingili na pingili kuna vinyama ambavyo ukikaa kwa kupinda huwa vinasogea nyuma hivyo, kusababisha mifupa ya uti wa mgongo kusagana na kuumiza mishipa ya fahamu ambapo baadae huleta maumivu ya mgongo.

“Hali hiyo ikizidi husababisha maumivu  kwenye miguu au mikono, hutegemea hilo tatizo liko sehemu gani – shingoni, kiunoni au kwenye mgongo.

“Tukiachana hilo, watu wengine wanakaa wanafanya kazi kwenye kompyuta mpakato wakiitumia kwa muda mrefu au kutumia simu kwa kuweka kwenye mapaja, hii pia  inaweza kuleta matatizo kwenye shingo na hata mgongo,” anasema.

Anabainisha kuwa hata watu wanaosimama kwa muda mrefu nao wapo hatarini kupata maumivu ya mgongo kwa kadiri siku umri unavyosogea.

“Mfano askari anaweza kusimama barabarani muda mrefu hata saa nane na   zaidi au unakuta daktari anafanya upasuaji akiwa amesimama kwa zaidi ya saa nane, hali hii inaweza kusababisha matatizo ya kuumwa mgongo au shingo,” anasema.

Anaeleza kuwa ni muhimu zaidi watu kufanya mazoezi ya viungo.

“Hata mazoezi hayatakiwi yazidi kiwango kinachostahili, kwani nayo yakizidi huwa na madhara. Kumbuka kuwa kila aina ya mazoezi huwa yanategemea na umri wa mtu.

“Wakati mwingine unaweza kukuta mtu  anafanya mazoezi kwa nguvu, ukiuliza umri wake unaambiwa miaka 75; huyu tayari mwili wake unakuwa umeshaondokana na ile hali ya ujana hivyo  kinachotokea ni kujiumiza, matokeo yake anaweza kupata matatizo ya mgongo.

Kwa mujibu wa Dk. Lemery, jambo lingine  linalochangia maumivu ya mgongo ni kubeba mizigo mizito kupita kiasi na kwa muda mrefu. 

“Wakati mwingine pia unaweza kuwa kila siku unavyeshea bustani kwa kubeba ndoo  yenye maji kwa mkono wa kulia asubuhi na jioni kwa muda mrefu, matokeo yake ni mgongo unakuwa ukivutwa upande mmoja muda wote na hivyo kukuletea madhara.

“Pia wale wanaoandika muda mrefu ubaoni kuanzia asubuhi hadi jioni, matokeo yake ni lazima baada ya muda utaanza kulalamika kuhisi maumivu ya shingo, mgongo na bega, hii tunasema ni ugonjwa unaotokea kutokana na kazi unazofanya.

“Lakini pia matatizo mengine ya mgongo husababishwa na magonjwa kama yale ya  kuambukizwa na wadudu ambao huingia mwilini na kutengeneza uvimbe katika uti wa mgongo,” anabainisha.

Dk. Lemery anasema kwa kadiri umri unavyozidi kwenda, hali ya afya ya mgongo inaendelea kubadilika na kuwa dhaifu.

“Watu wanapofikisha kuanzia miaka 40 na kuendelea, mgongo unaanza kukua, utakuta kuna vitu vinabadilika hali yake ya uhalisia iliyokuwapo tangu utotoni na ujanani hatimaye vinakuwa havikai sawa hivyo vinaanza kuumiza mishipa ya fahamu na uti wa mgongo hatimaye kusababisha maumivu ya mgongo.

“Pia kuna watu ambao wana uzito ulipitiliza. Utakuta mtu ana kilo 110 hadi 120… hili ni tatizo. Mtu wa aina hii ni lazima apate tatizo kwa sababu uti wake wa mgongo utakuta umetengenezwa kwa ajili ya kubeba kila 70 au 80; lakini alizonazo ni zaidi ya hapo,” anafafanua.

Anasema mara nyingi wagonjwa wanaofika hospitalini huwa ni wale waliofanyakazi za kukaa au kusimama muda mrefu, au walipata ajali.

“Hata hivyo, kuna kiwango kidogo cha wagonjwa waliopata uvimbe unaogusa pingili za mgongo, nyama za maeneo ya mgongo au uti wa mgongo,” anaeleza. 

DALILI ZINAVYOANZA

Kwa mujibu wa Dk. Lemery mara nyingi dalili huwa zinaanza kwa kupata maumivu ya mgongo, wengine hulalamikia kupata shida ya kunyanyuka pindi wanapokaa kwa muda mrefu.

 “Wengine utakuta anahisi moto mgongoni, wakati mwingine akisimama au hata akiwa anajaribu kunyanyuka baada ya kukaa huwa anashindwa kufanya hivyo kwa haraka, inabidi aanze kunyanyuka taratibu na kuondoka taratibu hadi mgongo uachie ndio aanze kutembea vizuri.

“Wengine watakuambia maumivu yako mgongoni yanashuka na mguu mmoja  hadi chini ya  vidole au kwenye unyayo anahisi ganzi na hata misuli kukaza ikitokea amekaa muda mrefu.

“Kwa wale ambao umri umeenda kama kuanzia miaka 50 hadi 60, huwa anashindwa kutembea umbali mrefu  lazima atasikia miguu inauma, anachoka na kujikuta anakaa kwanza apumzike ndipo aanze kutembea tena,” anaeleza Dk. Lemery.

Anasema wakati mwingine mguu mmoja au yote miwili inaweza kukosa nguvu  hivyo kumlazimu muhusika kutembea kwa msaada wa fimbo.

“Wagonjwa wengi tunaowaona asilimia 30 wanapata tatizo kutokana na shuguli wanazofanya (degenerative cause). Wengine ni wale ambao umri umekwenda  hivyo mfumo wa mgongo umebadilika kwahiyo unashindwa kuusaidia mwili, matokeo yake kuanza kupata maumivu; wagonjwa wa aina hii huwa ni asilimia 70,” anabainisha Dk. Lemery.

MATIBABU

Dk. Lemery anaeleza kuwa matibabu yapo ambayo hutolewa kulingana na tatizo lilivyo.

“Kuna dawa za kutuliza maumivu lakin kabla ya kuwapa huwa tunawasikiliza na kufanya vipimo kujua tatizo limefikia hatua ipi, baada ya hapo ndipo tunapanga matibabu kama mgonjwa apatiwe dawa za maumivu za kumeza, kupaka au kumwanzishia mazoezi tiba (backcare program). Hapa anaweza akapewa mazoezi ya jinsi ya kukaa, kuinama, kuokota kitu kilicho chini, mizigo ya kubeba na mengineyo.

“Lakin pia tuna wagonjwa ambao tunawashauri kupunguza uzito na kufikia kiwango ambacho kinakubalika. Tunawatuma kwa wataalamu wa lishe  waweze kuwaangali kwanini wanauzito kupita kiasi hatimaye kubadilishiwa lishe ili kupunguza uzito uliozidi.

“Maumivu yakiwa hayasikii dawa wala mazoezi, tunawachoma baadhi ya sindano  za kuzuia mishipa ya fahamu inayopeleka maumivu ili wasisikie maumivu ambazo huitwa neva block,” anaeleza.

Anasema endapo hatua hizo zote zitashindikana,   mgonjwa hulazimika kufanyiwa upasuaji kwaajili ya kuondoa kinachokandamiza na kumfunga mgongo ili asizidiwe uzito.

“Wagonjwa wengi wanapona kabisa… huwa tunawafundisha mazoezi ya kufanya nyumbani kwahiyo akifanya mazoezi hapa na kufanyiwa upasuaji na huko anakoenda akazingatia masharti anaweza kupona kabisa na kuwa salama.

ONYO

Dk. Lemery anawaonya watu wanaokaa muda mrefu au kusimama waweze kuepuka hilo ili afya zao za mgongo na shingo ziwe salama.

“Watu wanaokaa muda  mrefu nawashauri kuwa kila baada ya dakika 30 hadi 45 wawe wanabadilisha mkao kwa kusimama na kujinyoosha.

“Kwa wale wanaofanya mazoezi wanatakiwa kupata ushauri wa wataalmu  ili kujua ni mazoezi gani ambayo wanaweza kufanya na kwa kiwango gani kutokana na alivyo.

Anatoa ushauri kwa wale wenye uzito mkubwa kuzingatia aina ya ulaji kwa muda unaotakiwa.

“Tunavyokula chakula asubuhi huwa kinaenda kufanya kazi na unatumia nguvu nyingi hivyo ikifika mchana unapunguza na jioni unapunza kabisa… hii ndio aina nzuri ya ulaji wa chakula,” anashauri Dk. Lemery.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles