Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR
KATIBU wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya CCM Taifa, Pereira Ame Silima, amewataka viongozi na watendaji wanaochaguliwa kwenye uchaguzi wa chama na jumuiya zake kwa sasa kuwa na fikra na mitazamo mipya itakayoongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya CCM.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati za Siasa za mikoa ya CCM Mjini na Magharibi pamoja na wajumbe wa sekretarieti za jumuiya za chama hicho jana mjini Unguja, ambapo alisema chama hicho kitaendelea kuwa imara kutokana na utamaduni wa kupata viongozi kwa njia za kidemokrasia.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha chama, sambamba na kujitambulisha kwa viongozi hao, kwani tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni Mjini Dodoma, hiyo ndiyo ziara yake ya kwanza.
“Viongozi na watendaji wenzangu tujue kuwa Chama Cha Mapinduzi kipo kwa ajili ya wananchi wote, hivyo lazima tufanye kazi kwa ushirikiano ili tutimize kwa vitendo dhamira ya mabadiliko yaliyofanywa ndani ya Katiba, yanayolenga kuongeza ufanisi katika nyanja za kisiasa na kiuchumi ndani ya chama chetu.
“Dhana ya CCM mpya itekelezwe na kusimamiwa na fikra mpya na si upya wa viongozi wanaochaguliwa kwa sasa,” alisema.