WAKULIMA KUPATIWA SOKO LA UHAKIKA-OLE SENDEKA

0
519

Na MWANDISHI WETU-NJOMBE


MKUU wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, amesema suala la upatikanaji wa maji ya uhakika bado ni changamoto kubwa kwa wakulima wa mkoa huo na mikoa jirani katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Pamoja na hali hiyo, amesema sasa Serikali imejipanga kuhakikisha inawapatia masoko ya uhakika wakulima hao ili waweze kunufaika na kilimo chao.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa, katika mkutano wa siku mbili wa kufanya tathmini ya maendeleo ya Kongani ya Ihemi, iliyo chini ya mpango wa kuendeleza kilimo wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ushoroba wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT), ambapo alibainisha shughuli za kibinadamu ndizo zinazosababisha vyanzo vya maji kukauka.

“Hatuwezi kuwa na kilimo chenye tija ikiwa bado tunahangaika kuwa na teknolojia ya kisasa ya kupata maji ya uhakika, vyanzo vya maji vimekauka kutokana na kuharibiwa na shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira. Tuache kilimo cha vinyungu pembezoni mwa vyanzo vya maji.

“Tufahamu kuwa, kilimo endelevu chenye tija ndio kichocheo cha kuzalisha malighafi za viwanda. Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kuwa na uchumi wa kati na kuanzisha viwanda, malighafi zote za viwandani zinatoka kwenye kilimo,” alisema.

Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa Maendeleo ya Kongani ya Ihemi, inayojumuisha mikoa miwili ya Njombe na Iringa, Maria Ijumba, aligusia umuhimu wa kushirikiana wakulima wadogo na wakubwa ili kuimarisha shughuli za kilimo na kubadilishana uzoefu.

Alisema wadau wote wa kilimo, wakiwamo wakulima wenyewe, mashirika ya maendeleo, wafanyabiashara wa mazao, wamiliki wa viwanda na viongozi wa serikali, kwa nafasi zao wajitathmini wameifanyia nini Kongani ya Ihemi ili kuona kama kuna uwezekano wa kuhamia kongani nyingine.

“Tujipime tupo wapi, mipango tuliyokuwa nayo miaka mitatu iliyopita wakati tukianzisha kongani hii imefanikiwa kwa kiasi gani.

 

“Kitu muhimu cha kuangalia kama tumepiga hatua ni miundombinu, ikiwamo barabara, upatikanaji maji, mawasiliano, ikiwamo umeme, maghala ya kuhifadhia chakula. Tuangalie wakulima wanauza vipi mazao yao na wananunuaje pembejeo za kilimo na uhakika wa viwanda vya kuchakata mazao,” alisema.

Alisema hapo ndipo wanaweza kusema wamefanikiwa na wapo tayari kuhamia kongani nyingine kati ya sita ambazo SAGCOT wameziainisha kusaidia wakulima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geofrey Kirenga, alisema kilimo ndilo eneo linalogusa maisha ya wanadamu moja kwa moja, hivyo atahakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anawafanya wakulima wanufaike kupitia shughuli hii.

“Kwa miaka mitatu tuliyokuwapo Ihemi kuna mambo tumefanikiwa na kuna mambo bado hatujafanikiwa na hizo ni changamoto tunazozifanyia kazi ili kwa pamoja tuziondoe,” alisema.

Kongani ya Ihemi ilianzishwa Mei, 2015 kwa kushirikisha wakulima, wawekezaji, serikali na wafanyabiashara kwa lengo la kusaidia wakulima wadogo na wa kati kutambua fursa zilizopo kwenye kilimo na kuongezea thamani mazao ili kupata faida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here