24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Nini hiki kinachojadiliwa kwa miaka 10?

mwenyekiti-wa-jumuiya-ya-nchi-za-afrika-mashariki-rais-dk-john-magufuli-akiteta-jambo-na-rais-wa-uganda-yoweri-museveniKWA takribani miaka kumi sasa, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimekuwa katika majadiliano na Jumuiya ya Ulaya (EU) kuhusiana na Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA).

Majadiliano kuhusiana na ushirikiano huo yalianza mwaka 2007 na ilitarajiwa kuwa mwaka huu pande hizo mbili zingefikia mwafaka.

Lakini wakati tarehe iliyopangwa kwa ajili ya kusaini makubaliano hayo, Tanzania ikaamua kutosaini na ikaeleza sababu zake. Inavyoelekea hatua hiyo iliziudhi baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwani mwelekeo ulionyesha kuwa kimsingi nchi zote zilikuwa zimekubali kusaini makubaliano hayo.

Kwa kuonyesha kuwa hatua hiyo iliziudhi baadhi ya nchi, mara baada ya hatua hiyo, Kenya na Rwanda zikaamua kusaini peke yao bila kuzihusisha nchi nyingine za EAC. Uganda nayo ambayo awali ilionyesha kuiunga mkono Tanzania kwa hatua yake ya kukataa kusaini, ikageuka na kusema itasaini.

Hali hii inasaidia kuonyesha dhahiri kuwa umoja ambao nchi za EAC zimekuwa zikiushadidia kila mara ulikuwa umetoweka. Hivyo, mkutano maalumu wa wakuu wa nchi hizo uliofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita, viongozi wakatoka na makubaliano ya kujipa miezi mitatu zaidi ili kujadili na kuondoa tofauti zao katika jambo hili kabla ya kufikia mwafaka.

Ni jambo zuri sana kuzungumza pale ambapo pande mbili zinapokosa maelewano. Mazungumzo ndio njia mwafaka ya kushughulikia tofauti hizo lakini inapotokea mazungumzo yanatumika kama sababu ya kutofikia mwafaka, mazungumzo hayo yanapoteza maana yake halisi.

Na hili ndilo linaweza kuwa linatokea katika majadiliano haya kuhusu EPA kati ya EAC na EU. Mazungumzo haya yamedumu kwa takribani miaka kumi sasa lakini hata pale ambapo inaonekana kuwa mwafaka ulifikiwa kuhusiana na jambo hilo, bado nchi nyingine zikaja na msimamo tofauti siku chache tu kabla ya kutiliana saini makubaliano hayo.

Muda mrefu huu uliotumika kujadili suala hilo unaweza kuonyesha kuwa suala hilo ni gumu sana. Lakini kwa wataalamu wa uchumi wanafahamu kuwa uchumi unaonyeshwa kwa namba. Iwapo namba hazikubaliani na masilahi yako, ni rahisi kufahamu kuwa mpango husika haukufai.

Katika hili la EPA, ni dhahiri kuwa kwa kutumia wataalamu wake wa uchumi haikuwa kazi kubwa kwa nchi za EAC, kwa pamoja au moja moja, kupima na kufahamu uzuri na ubaya wa EPA kwao. Hivyo, inashangaza ni kwanini wamechukua muda wa miaka kumi kujadiliana suala ambalo kimsingi si gumu namna hivyo kufikia mwafaka.

Lakini kurefushwa kwa majadiliano haya kumeufanya hata mkataba wenyewe wa EPA uwe umepitwa na wakati. Ni dhahiri kuwa hali za kiuchumi za nchi za EAC na EU wakati mkataba unaandaliwa zaidi ya miaka kumi iliyopita ni tofauti sana na hivi sasa.

Hivyo hata mkataba wenyewe utakuwa umepitwa na wakati na hiyo inaweza kuwa sababu kwanini baadhi ya nchi zinaanza kugeuka. Zinageuka kwa sababu mazingira ya sasa hayaendani na yaliyo katika mkataba kwa sababu uliandaliwa katika mazingira tofauti na ya sasa.

Kwa kulifahamu hili, miezi mitatu waliyopeana nchi za EAC ni kupoteza wakati. Kama bado nchi hizi zina nia ya kuendelea na mkataba huu, ni vema wakakubaliana na EU kuwa warudi tena mezani kuandaa mkataba mwingine mpya utakaozingatia hali za kiuchumi za hivi sasa kwa kila upande.

Mkataba huo mpya ndio utatoa fursa ya kujadiliana kitu ambacho kitawanufaisha wote. Na majadiliano yake yasifanywe kwa muda mrefu ili kuepuka kurudia kosa lililofanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles