26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Kipi kitangulie kati ya madawati, walimu

joyce-ndalichakoTANGU Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kumekuwapo na jitihada mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu kama vile kubaini wanafunzi hewa ambao walikuwa wakinufaika na mikopo ya elimu ya juu, wanafunzi wasio na sifa za kujiunga na vyuo vikuu, kampeni ya madawati pamoja na jitihada nyingine.

Kwa namna ya pekee, napenda kumpongeza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kwa kuonyesha msimamo wake thabiti katika kusimamia suala la ubora wa elimu hapa nchini.

Moja kati ya kampeni iliyokuwa na mafanikio makubwa ni ya madawati iliyoanzishwa na Rais Dk. John Magufuli. Sehemu nyingi za nchi kwa sasa wanafunzi wanasoma wakiwa wamekalia madawati, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kama nchi tukiamua tunaweza.

Elimu ni jambo muhimu sana ambalo halitakiwi kufanyiwa mzaha katika maendeleo ya nchi yoyote ile. Elimu ni nguzo muhimu sana katika kujenga taifa linalojitambua na ni nyenzo ya kupambana na umasikini.

Elimu huwapa watu uwezo wa kujitambua pamoja na kutambua fursa zinazowazunguka na hivyo kuzitumia kujiletea maendeleo. Nchi nyingi zilizoendelea ulimwenguni ni zile zilizowekeza vizuri kwenye sekta ya elimu.

Wakati mataifa mbalimbali yakijaribu kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya elimu ili kujikwamua kiuchumi, Tanzania bado haijaweza kufanya vyema katika kuwekeza kwenye sekta hii muhimu.

Kwa mfano, hivi sasa kumekuwa na suala la madawati ambalo ni jambo jema, lakini suala la kuboresha masilahi ya walimu bado halijapewa uzito wa kutosha.

Ualimu ndiyo taaluma mama wa taaluma nyingine zote. Ili uwe daktari, mhandisi, mchumi, mhasibu, rubani na mwana taaluma yeyote ile ni lazima ukae darasani na ufundishwe na mwalimu.

Kwa mantiki hii, ni kuwa tunapotaka kujenga taifa lenye wataalamu wazuri watakaokuja kusimamia rasilimali za nchi tunapoelekea kwenye uchumi wa kati, ni lazima tuanze na kuwa na walimu bora ambao wamepikwa wakaiva kwa ajili ya kuwaandaa wataalamu bora katika sekta mbalimbali.

Cha kushangaza ni kuwa kwa hapa kwetu Tanzania watahiniwa ambao hawakufanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha nne na cha sita ndio ambao huenda kusomea ualimu huku wale waliofanya vizuri wakienda kusomea taaluma nyingine.

Kama hiyo haitoshi, upo utaratibu unaoruhusu watahiniwa ambao hawakufanya vizuri kuchaguliwa kusomea ualimu kwa ajili ya kufundisha masomo waliyoshindwa kufaulu, hii si miujiza?

Wapo watu wengi ambao wangeweza kuwa walimu wazuri lakini wameamua kuachana na wazo hilo kutokana na sababu mbalimbali. Moja kati ya sababu ni masilahi duni pamoja na hadhi ya walimu katika jamii.

Wakati miaka ya nyuma kuwa mwalimu ilikuwa ni sifa kubwa, leo hii mwalimu anaonekana ni mtu aliyeshindwa shule pamoja na maisha kwa ujumla na ndiyo sababu ya kukimbilia ualimu.

Ni jambo lililo wazi kuwa sekta ya elimu hapa nchini inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kama Serikali ina nia ya dhati ya kuiboresha, ni muhimu ikaanza kwa kuwaandaa walimu wazuri ambao masilahi yao yataboreshwa na hivyo kufanya kazi kwa kujituma zaidi.

Kama tutaendelea kuwa na walimu waliofeli mitihani na kisha kwenda kozi ya wiki tatu na hatimaye kwenda kufundisha, ni wazi kuwa tutaendelea kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Ukitembelea shule za vijijini na ukaona maisha wanayoishi walimu, hutatamani mwanao au ndugu yako wa karibu awe mwalimu. Walimu wengi vijijini hulazimika kuishi kwenye nyumba zisizo na huduma muhimu kama maji na umeme.

Katika hali kama hiyo inakuwa ni vigumu kwa kijana, kwa mfano aliyemaliza chuo kikuu kwenda kuishi katika mazingira kama hayo. Wengi wameishia kubadilisha fani kutokana na mazingira yasiyokuwa rafiki.

Kwa maana hii ni kuwa Serikali itaendelea kuongeza udahili kwa wanafunzi wanaosomea ualimu lakini upungufu utaendelea kuwa pale pale, kwani baada ya kumaliza hufanya shughuli nyingine au kufundisha shule binafsi ambazo zina masilahi bora kuliko zile za Serikali.

Badala ya Serikali kuweka nguvu kubwa kwenye suala la madawati, ni wakati mwafaka wa kuweka nguvu katika kuboresha masilahi ya walimu ili kurudisha ari ya kufanya kazi, la sivyo inawezekana hata matokeo yaliyotarajiwa kufikiwa kutokana na kampeni ya madawati ambayo ni kuongeza ufaulu yasifikiwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,631FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles