27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Tuwe na Katiba itakayolinda machaguo ya wananchi

dr-harrison-mwakyembeNa FREDERICK FUSSI

MFUMO wa Katiba yetu tuliyonayo hivi sasa una msingi wa kuhudumia chama kimoja, ambacho ndicho kilichopo madarakani. Katiba hii tuliyonayo ni aina ya katiba ambayo ina mifumo ambayo haiwezi kabisa kulinda mapenzi ya wananchi katika sanduku la Kura.

Hii ni Katiba ambayo haushindi uchaguzi kwa sababu umepata kura nyingi ndani ya sanduku la kura, ila unashinda uchaguzi kwa sababu ya uwezo wako kama mgombea kulinda kura nyingi ulizopata dhidi ya mpinzani wako.

Sasa hatuhitaji Katiba ambayo inamlazimisha mgombea kulinda kura zake, tunahitaji aina ya Katiba ambayo inaweka mifumo inayolinda uchaguzi na mapenzi ya watu ndani ya masanduku ya kura.

Hatuhitaji mgombea mwenye uwezo wa kulinda kura zake ila tunahitaji katiba ambayo itaweka mifumo itakayowezesha ulinzi wa machaguo ya wananchi. Hii ndio demokrasia iliyokomaa!

Wizi wa kura katika uchaguzi huweza kuzuiliwa endapo mifumo inayoshughulikia uchaguzi inaweka ulinzi wa hizo kura. Hivi sasa hapa nchini kama wewe ni mgombea ubunge na ukashindwa uchaguzi kwa sababu umeibiwa kura na hukuweza kulinda kura, Katiba inatoa fursa ya kupinga matokeo yale mahakamani na ukiwa na ushahidi usiotiliwa shaka kuwa ulishinda uchaguzi ule na Mahakama ikajiridhisha na ushahidi huo basi unapewa ushindi wa ubunge, lakini sivyo kwa nafasi ya urais.

Tuna aina ya Katiba ambayo kwa kutoruhusu mgombea urais kupinga matokeo ya mgombea urais mwenzake aliyetangazwa kuwa mshindi, inatoa mwanya wa mazingira ya wizi wa kura kufanyika kwa kuwa hakuna hatua za Kikatiba ambazo mgombea urais anaweza kuzichukua ili kutafuta ukweli wa mambo kwa njia ya Mahakama ambayo kwa kiasi kikubwa ni chombo cha kutoa haki.

Katiba ya sasa kutoruhusu mgombea urais kupinga matokeo ya urais mahakamani ni sawa na kitendo cha kuhalalisha wizi wa kura unaoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi. Katiba yetu ya hivi sasa imefanikiwa katika hili, haijatoa haki kwa mgombea kupinga matokeo ya urais mahakamani.

Watu wanaounga mkono Katiba ya hivi sasa kwa jinsi ilivyo wanaweza kuwa na sababu zao kwanini Katiba hii ya sasa haitoi haki ya matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Nina uhakika hata kama sababu hizo zingekuwepo basi hazitoshi kuondoa dhana kuwa kwa hali ilivyo hivi sasa katiba yetu inaruhusu wizi wa kura kufanyika kwa kuendelea kukaa kimya juu ya kutotoa haki ya kupinga matokeo ya urais mahakamani.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Katiba hii kutotoa haki ya mgombea kupinga matokeo hayo mahakamani. Ni katiba hii hii ambayo haisemi lolote juu ya mgombea binafsi, yaani mtu ambaye hana chama kupewa fursa ya kugombea urais.

Ni katiba hii hii ambayo kabla ya mwaka 1984 haikuwahi kuwa na vifungu vya Haki za Binadamu yaani ‘the Bill of Rights’, mpaka zilipoingizwa mwaka 1984 baada ya kutokuwa na haki hizo tangu Taifa linapata Uhuru mpaka mwaka huo. Tunaposema katiba hii ni mbovu na haifai lazima watu wajue ni kwa sababu zipi.

Ni kwa sababu kama hizi za kuwa na viraka viraka kama ambavyo ilikuwa Haki za Binadamu hazikuwepo nchini kisheria kabla ya mwaka 1984, hii maana yake ni kuwa haki za binadamu zilikuwa zinaminywa kama ambavyo haki ya wapiga kura kulindiwa kura zao kwa mujibu wa Katiba inaendelea kuminywa kwa kutotoa fursa kwa matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Kwa kawaida unapoapa kuilinda hii Katiba unaapa kuulinda na udhaifu wote na uzuri  wake. Kiapo cha kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kinajuisha ulinzi dhidi ya uminyaji wa haki ya mgombea binafsi pamoja na haki ya mgombea urais anayedhani kuwa ameibiwa kura katika uchaguzi.

Mapambano ya kudai haki za Binadamu zitambuliwe Tanzania hayakuwa kitu kidogo kilichofanyika kirahisi na wepesi mpaka ilipofika mwaka 1984, kadhalika mapambano ya madai ya mgombea binafsi na haki ya kupinga matokeo ya urais mahakamani si jambo dogo na ni mapambano yenye mwelekeo wa kufanikiwa huko mbele ya safari.

Pamoja na kuingizwa kwa haki za binadamu ndani ya Katiba ya Tanzania na uundwaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora bado kumekuwepo changamoto kadhaa katika ulinzi wa haki za binadamu.

Yamejitokeza matukio kadhaa ya vifo vyenye utata yaani ‘extra judicial killing’ kwa baadhi ya watu wanapotimiza majukumu yao ndani ya mazingira ya kisiasa na kijamii kama ambavyo ilikuwa kwa mwanahabari Daudi Mwangosi, ambaye inasadikiwa alifariki kwa kupigwa bomu tumboni huko Iringa na Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mwenye  namba G .2573 Pacificius Cleophace Simon (27) ambaye baadaye Mahakama ilimtia hatiani kwa kuua bila kukusudia na kufungwa jela miaka 15.

Pamoja na kuwa hakuna haki ya mgombea binafsi wala hakuna haki ya kupinga matokeo ya urais mahakamani, jambo ambalo linabakia kuwa changamoto ya karne ya kidemokrasia hapa nchini.

Haki ya mgombea binafsi na haki za kupinga matokeo ya urais mahakamani ni sawa na haki za binadamu, pengine mtu angeweza kuziweka haki hizo katika fungu la haki za kisiasa, hizi ni haki ambazo zinapanua wigo wa uhuru wa wananchi na kwa kuwa zinalenga kuimarisha ushiriki wa wananchi ambao ndio binadamu wenyewe.

Hivi sasa wananchi wako huru kupiga kura kwa mtu wamtakaye, lakini kura zao kwa mtu wamtakaye si kigezo pekee cha mtu huyo kushika hatamu ya uongozi katika ofisi ya umma. Kura pekee inakuwa si kigezo kwa sababu siasa imejawa na michezo michafu ambayo inazidi nguvu kitendo cha kupiga kura.

Ukiongezea kutokuwepo kwa haki ya mgombea urais kupinga matokeo ya urais mahakamani na uwepo wa Tume ya Uchaguzi ambayo mwenyekiti wake na Mkurugenzi wote ni wateule wa mhimili wa Serikali, maswali juu ya Uhuru wa tume kutimiza majukumu yake bado unabakia kwenye mashaka, mashaka ambayo njia pekee ya kuyaondoa ni Katiba mpya inayoweka mifumo yenye kulinda machaguo waliyofanya wananchi, ikiwamo uhuru wa Tume ya Uchaguzi na haki ya mgombea urais kupinga matokeo hayo mahakamani kama ikibidi kufanya hivyo.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Sera na Uongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles