24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mtuhumiwa wa lukuvi ana kesi ya kujibu

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemkuta ana kesi ya kujibu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group. Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone, Mohamed Kiluwa (50) anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa rushwa ya Sh milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huyo jana baada ya Jamhuri kufunga ushahidi ikiwa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka.  

Hakimu Mkazi Samweli Obas alipanga mshtakiwa kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka yanayo mkabili Desemba 17 mwaka huu.

“Ushahidi uliotolewa umemtaja mshtakiwa hivyo atatakiwa kujitetea kwa mujibu wa kifungu cha 231 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,”alisema Hakimu Obas.

Wakili wa Utetezi, Imani Madega alidai  Kiluwa atajitetea yeye na shahidi mmoja ikiwamo kuwasilisha vielelezo.

Awali, Kaimu Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Ardhi, Wilson Luge (39) alidai jana kuwa alipokwenda kuhakiki fedha alikuta mfuko wa kaki juu ya meza na hakujua ulikuwa na nini ndani.

Alidai walioufungua mfuko huo ni maofisa wa Takukuru na kutoa fedha ambazo ni mabunda manne ya Dola za Marekani40,000 na waliwataka  yeye na Hellen Philipo wahakiki fedha hizo.

Akiongozwa na Wakili wa Takukuru,Maghela Ndimbo, shahidi huyo wa sita alidai Julai 16 mwaka huu alikuwa ofisini kwake Kanda ya Dar es Salaam ambayo zamani ilikuwa makao makuu ya wizarahiyo.

“Kati ya saa 7 hadi saa 10 jioni,tulikuwa tunaangalia mfumo wa  elekroniki tunaoutumia kama unafanya kazi vizuri ambako Kamishna Mkuu wa Ardhi, Mary Makondo aliwaita akiwaelekeza waende ofisi ya Waziri Lukuvi.

“Tulipoingia tulikuta baadhi ya watu ambao ni maofisa uchunguzi wa Takukuru, Waziri Lukuvi na Kiluwa.Tuliambiwa kuna bahasha ifunguliwe na sisi tuhakiki kilichomo…. Ofisa uchunguzi alifungua na sisi kuweka mezani mabunda manne yaliyofungwa,”alidai Luge.

Pia alidai baada ya kuzihakiki waliainisha fedha zote kwenye karatasi ya uchunguzi na kusaini na baada ya kukamilisha kazi hiyo waliruhusiwa kuondoka.

Shahidi akihojiwa na Wakili Madega kuhusu mahali walipozikuta fedha hizo, alidai   walizikuta kwenye mfuko na kwamba ofisa uchunguzi ndiye aliyefungua na  siyo Waziri Lukuvi wala mshitakiwa.

Naye Ofisa Uchunguzi wa Takukuru,Colman Lubisa (36)  alidai hakushuhudia wakati Kiluwa akitoa rushwa kwa Waziri Lukuvi bali walipoingia ofisini walikuta fedha mezani ndipo walipozihakiki.

“Sisi tulipata taarifa baada ya Waziri Lukuvi kupiga  simu kwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru, Mbengwa Kasomambuto na kumueleza kuwa Kiluwa atafika ofisini akiwa na fedha Dola za Marekani 50,000,” alidai Lubisa.

Alidai baada ya taarifa hiyo waliandaa mtego kikiwamo kifaa cha kurekodi ili endapo mshtakiwa atafika na fedha hizowaweze kumkamata.

Shahidi huyo wa tano  alidai baada ya kuandaa mtego walikaa nje kumsubiri mshtakiwa huyo na kati ya saa 6 hadi saba alifika akiwa na mkoba.

Alidai baada ya mshtakiwa kutoa fedha na kuziweka mezani waliingia na kumuweka chini ya ulinzi, waliita mashahidi kwa ajili ya kuzihakiki.

Alidai mshtakiwa alikuwa na fedha  nyingine ambazo ni Dola za Marekani 5,400 na Sh milioni 1.6 na kwamba Waziri Lukuvi alimuuliza fedha ni za nini na mshtakiwa alieleza kuwa ni kwa ajili ya mafuta.

Kiluwa  anadaiwa kuwa Julai 16, mwaka huu kati ya saa 6 na saa 8 mchana  akiwa Mkurugenzi wa kampuni hizo mbili alitoa rushwa ya Dola za Marekani 40,000  (Sh milioni 90) kwa Waziri Lukuvi.

Mshitakiwa anadaiwa kutoa  fedha hizo kwa lengo la kwamba asiwasilishe hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 Block B Kikongo na D Disunyura kilichopo eneo la viwanda  Kibaha mkoani Pwani. Kiluwa yupo nje kwa dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles