22.6 C
Dar es Salaam
Sunday, May 5, 2024

Contact us: [email protected]

Mbio za Kilimanjaro Marathon 2024 zazinduliwa

Na Safina Sarwatt, Moshi

Toleo la 22 la Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024 limezinduliwa Ijumaa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ikiwa ni ishara yakuanza kwa msimu wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Februari 25, mwaka huu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Tixon Nzunda, aliwapongeza waandaji wa mbio hizo kwa hatua iliyofikia hadi sasa tangu kuanzishwa kwake hasa kwa mchango wake katika kukuza utalii wa michezo na uchumi wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

“Tunajivunia mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon kwani zimeonekana kuwa moja ya matukio makubwa ya kimataifa katika ukanda huu kwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 12,000 na idadi kama hiyo ya watazamaji kutoka zaidi ya nchi 56 ambao wote hawa ni watalii watarajiwa,” amesema na kuongeza, hili ni tukio kubwa sana na muhimu kwa Taifa letu.

Nzunda ameendelea kusema kuwa hakuna mashindano mengine yanayoweza kufikia Kilimanjaro Marathon kwa maana ya matokeo yake katika kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuna haja kubwa kwa wadau wote wa michezo na wale wanaohusika na maswala ya biashara kufanya kazi kwa karibu katika kuhakikisha mashindano hayo makubwa yanaendelea kuweko kwa mstakabali mzuri wa kukuza michezo pamoja na uchumi wa Taifa na watu wake.

“Tumekuwa tukiandaa mbio za marathon kwa miaka 22 sasa na jumuiya ya wafanyabiashara itakubaliana nami kwamba kwa kawaida wakati wa mbio hizi ni msimu wa biashara aina mbalimbali mkoani hapa kukua ikiwa ni pamoja na hoteli zote na nyumba za kulala wageni kufanya biashara kubwa,” amesema Nzunda.

Aliongeza; “Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote kuzingatia ubora wa bidhaa zao pamoja na huduma watakazotoa ili kuhakikisha wageni wanapata thamani ya fedha watakazotumia.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza wadhamini wote wa mbio hizi wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager (mdhamini mkuu) na Tigo-21km Half Marathon, Gee Soseji wanaodhamini 5 km Fun Run kwa mchango wenu mkubwa,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania, Kanda ya Kaskazini Mashariki, Neema Patrick amesema wanajivunia kupitia Kilimanjaro Premium Lager, kudhamini hafla hiyo kwa miaka 22 iliyopita na kuwa miongoni mwa udhamini wa muda mrefu nchini Tanzania, ambapo alisema mbio hizo zimeendelea kuchangia utalii na utamaduni wa Mtanzania kwa ujumla.

Amesema TBL imetenga Sh milioni 28 ikiwa ni zawadi ya fedha huku washindi wa kwanza katika kitengo cha wanaume na wanawake wakitarajiwa kupata Sh milioni 4 kila mmoja.

Alitoa wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizo kujiandikisha kwa wakati kwani usajili tayari unaendelea kupitia www.kilimanjaromarathon.com.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya amesema;“Tunayo furaha kubwa kuwa wadhamini wa mbio za Tigo Half Marathon kwa mwaka wa tisa mfululizo; Tigo Half Marathon inawahusisha washiriki zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja wakiwemo wanariadha wa daraja la juu Barani Afrika; napenda kuwajulisha ya kuwa zawadi katika kitengo hiki zimeongezeka,” amesema.

Aliongeza, “Dirisha la usajili katika kitengo hiki linaendelea na washiriki wanaweza kupiga 15001#, kisha bonyeza 5 LKS, kisha bonyeza 5 (Tiketi) na kufuata maelekezo ili kukamilisha usajili wao.

Meneja wa Biashara na Masoko wa Gee Soseji, Margaret Karua, ambaye kampuni yake ndiyo wadhamini wapya wa 5 KM Fun Run amesema, mashindano hayo ni jukwaa sahihi la kutangazia bidhaa za kampuni hiyo.

“Kwa kushiriki mbio hizi, tutashirikiana na watumiaji wa bidhaa yetu kwa njia ya kujifurahisha na kuelimishana juu ya faida za kutumia bidhaa yetu kwa ajili ya kujenga afya kwa ujumla,” amesema na kuongeza, dhamira yetu ni kufanya mapinduzi katika soko la soseji kwani tumekuja na soseji zenye ubora, zilizoandaliwa kwa usafi, za gharama nafuu na zenye ladha nzuri zitakazovutia watu wengi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Salinero Hotels ambao ndiyo walikuwa wenyeji wakati wa uzinduzi huo, Ben Mengi amesema mashindano hayo yamekuwa chachu kubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo sekta ya utalii kupitia michezo.

“Sisi tunayo fahari kubwa kuwa sehemu ya mashindano haya maarufu ulimwenguni kwa sasa; katika kuhamasisha washiriki wa mbio hizi Salinero inaahidi kutoa ofa kwa washindi wa kwanza wa 42 km na 21 km katika vitengo vyote vya wanaume na wanawake ya kulala usiku mmoja katika Serengeti Lodge,” alisema.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon zitakazofanyika Jumapili Februari 25, 2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles