25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

May akiri makubaliano ya Brexit hayatapita bungeni

LONDON, Uingereza

WAZIRI Mkuu, Theresa May, amekiri kuwa mikakati ya serikali kuidhinishwa mpango wake wa Brexit bungeni imefeli na amesema kuna matarajio madogo kwa wabunge kuunga mkono makubaliano yaliokataliwa mara tatu.

Huku nchi hii  kwa mara nyingine ikibakisha siku chache tu kutoka tarehe ya mwisho ya kuondoka Umoja wa Ulaya, May aliwashinikiza wabunge wa upinzani kusaidia kupatikana kwa makubaliano ya mwafaka, akisema wapigakura wanatarajia wanasiasa wao kushirikiana pale maslahi ya kitaifa yanapotaka hivyo.

Baada ya makubaliano ya May na Umoja wa Ulaya kukataliwa kwa mara ya tatu na Bunge, waziri mkuu huyo alikialika chama cha upinzani cha Labour wiki iliyopita  kujadili mikakati mbadala,’lakini  siku tatu za mazungumzo ziliisha bila makubaliano na chama hicho cha Labour kikiishutumu serikali ya kihafidhina ya May kwa kutotoa mabadiliko ya kweli.

“Sijaona mabadiliko yoyote makubwa katika msimamo wa serikali mpaka sasa,” alisema kiongozi wa Labour Jeremy Corbyn juzi. “Nasubiri kuona misitari myekundu ikihamishwa,”aliongeza kiongozi huyo.

Chama cha Labour kinapendelea mchakato laini wa Brexit kuliko ilivyopendekezwa na serikali.

Chama hicho kinasema Uingereza inapaswa kubakia ikiongozwa na sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu biashara na kuendeleza viwango vya kanda hiyo katika maeneo kama haki za wafanyakazi na ulinzi wa mazingira.

 Kiongozi wa chama hicho cha Labour   anasema kwamba  hajaona mabadiliko katika msimamo wa serikali ya kihafidhina ya Waziri Mkuu  May.

Uingereza inatarajiwa kuondoka Umoja wa Ulaya siku ya Ijumaa iwapo May hatopata makubaliano ya kurefusha tena mchakato kutoka jumuiya hiyo, ambao tayari ulikubali kurefusha siku ya Brexit iliyopangwa awali kuwa Machi 29 mwaka huu.

 May sasa anaomba muda wa kuondoka Uingerea urefushwe hadi Juni 30, akitumaini kufikia mwafaka na chama cha Labour na makubaliano kupitishwa na Bunge katika muda wa wiki chache.

“Kadiri hii inavyochukuwa muda mrefu, ndivyo hatari inavyoongezeka ya Uingereza kuondoka kabisa,” alisema May katika taarifa yake. Lakini Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanapendelea ucheleweshaji mrefu zaidi ili kuepusha duru nyingine ya  matatizo ya maandalizi na kisiasa. Na wanasema Uingereza inahitaji kuwasilisha mpango madhubuti wa kukomesha mkwamo ili kupata uahirishaji zaidi.

Urefushaji unahitaji idhini ya viongozi wa mataifa yote 27 wanachama yanayosalia, ambao baadhi yao wamechoshwa na mashaka ya Brexit na wanasita kurefusha zaidi mchakato huo.

Mwezi uliopita, Umoja wa Ulaya uliipa Uingereza hadi Aprili 12 kuidhinisha makubaliano ya kujiondoa uliofikia na serikali ya May, kubadili mkondo na kutafuta ucheleweshaji zaidi wa Brexit, au kuondoka bila makubaliano au kuwepo na kipindi cha mpito kupunguza mshtuko.

Uchunguzi wa taasisi ya Infratest dimap unaonyesha kuwa idadi kubwa zaidi ya Waingereza wanajutia mpango huo wa Brexit.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,695FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles