26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Matonyok yatoa miche ya parachichi Rombo

Safina Sarwatt, Rombo

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Matonyok Organization linalojishughulisha na Utunzaji wa Mazingira wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, limeanza kutoa miche ya parachichi na matunda mengine bure kwa wakulima, lengo ni kutunza mazingira na kuongeza kipato cha wakulima.

Mkurugenzi wa Matonyok Organization, Alais Lenana Momoi, ameyasema hayo jana wakati wa ziara ya kikazi ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo Kanali Hamisi Maigwa, alipolitembelea shamba darasa hilo kwa ajili ya kujifunza.

Amesema tayari shirika hilo limegawa miche ya parachichi na matunda 200,000 kwa wakulima wadogo na  miche 26,000 tayari ipo  katika kitaru ambapo wanatarajia kuanza kuigawa kwa wakulima wakati wa msimu wa mvua.

“Tangu mradi huu uanze mwaka 2018 wakulima wapatao 870 wamenufaika na miche ya matunda zikiwamo taasisi mbali mbali za serikali, shule na makanisa,”amesema

Aidha Momoi amesema wameshatoa msaada wa mizinga 80 ya kisasa ya kufugia nyuki ili wakulima hawa waweze kujiongezea kipato na kuacha tabia ya kuingia katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro kutafuta kuni.

Amefafanua kuwa mti mmoja wa parachichi unatoa kiasi cha wastani wa kilo 150 hadi 500 ambapo inakadiriwa kuzalisha parachichi zenye thamani ya shilingi 200,000 hadi shilingi 750,000 kwa mti wenye umri wa miaka mitano hadi 10 na kwamba huzaa baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu.

Akitoa taarifa ya mradi, Mratibu wa Shirika la Matonyok, Poul Momoi, amesema lengo la mradi huo ni kuboresha mazingira na kuongeza kipato cha wakulima wadogo wadogo kiuchumi.

Amesema hatua hiyo itawasaidia wakulima kuwa na kipato cha kujikimu kimaisha,changamoto iliyopo kwa sasa baadhi ya wakulima wamekuwa wakichukua miche ya matunda na kwenda kuiuza kinyume na malengo ya mradi.

“Lengo la mradi huu ni kuwapatia wakulima wadogo miche ya matunda bure, lakini kwa sasa kumejitokeza changamoto ya watu kuja kuchukua miche hii na kwenda kuiuza,”amesema.

Amesema utaratibu uliopo kwa sasa ni kumsajili mkulima na baada ya kumsajili tunakwenda kukagua shamba lake na kuendelea kumfuatilia hatua kwa hatua ili kuondokana na tabia ya baadhi ya wakulima wasio waaminifu kuchukua miche hiyo na kwenda kuiuza.

Naye  Mkuu wa Wilaya, Kanali Maiga, amesema Serikali imedhamiria kuboresha kilimo cha parachichi kwani thamani na uhitaji wa zao hilo nje ya nchi umekuwa ni mkubwa.

“Serikali kwa sasa ina mpango wa kuwaondoa wananchi wote walioko katika maeneo ya msitu wa nusu maili, kutokana na uharibifu wa mazingira, hivyo niwaomba sasa kuitumia fursa hii kwa ajili ya kuanza kulima zao la parachichi.

“Zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na gharama za uzalishaji ni nafuu wahimize wananchi kulilima zao hili kwa wingi kwa ajili ya kujipatia pesa,”amesema Kanali Maiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles