29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Makala| ‘Fedha’ inavyotengeneza udumavu, utoro kwa watoto Njombe

Na Elizabeth Kilindi, Njombe

Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inasema wazazi walezi wanapaswa kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kuchukua hatua pale ambapo watoto wanaonekana kunyimwa haki zao.

Wazazi, walezi na jamii wana wajibu wa kuhakikisha kwamba watoto wote, wakiwemo wale walio katika mkinzano na sheria wanafurahia haki zao na kutekeleza wajibu wao kikamilifu.

Wazazi, walezi na jamii wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanawaongoza watoto katika kutekeleza majukumu yao.

Hii ni tofauti kwa baadhi ya jamii wilayani Njombe mkoa wa Njombe ambako wazazi wanakuwa bize na shughuli za kipato ikiwemo kilimo na kushindwa kusimamia majukumu ya malezi ipasavyo kama sheria inavyosema.

Msimu wa kilimo unapofika familia nyingi zinakwenda shambani huku nyuma zikiwaacha watoto bila ya uangalizi.

Mbali na uangalizi hata chakula wanachokula watoto hawa ni huzuni kwa sababu mzazi akibandika makande asubuhi mtoto anashindia hadi jioni huku yakiwa yamejazwa maji hii ni kutokana na kukosekana mtu wa kuwapikia jambo ambalo linachochea udumavu kwa watoto hawa kutokana na kutokula mpangilio sahihi wa chakula kama inavyoshauriwa na wataalamu.

Athari za jambo hili ni kuendelea kusababisha matukio ya ubakaji, ulawiti hata mauaji sambamba na ukosefu wa lishe bora kutokana na kurudia mlo mmoja mara kwa mara.

Takwimu za mwaka 2018 kuhusu udumavu kwa watoto katika mkoa wa Njombe zinaonyesha kuwa mkoa huo unakabiliwa na udumavu kwa asilimia 53.6 ukifuatiwa na Rukwa 47.9, Songwe 43.3 na Kigoma 42.3.

Katika kukabiliana na tatizo hilo serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa masuala ya lishe kuondoa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi kati ya kesi 232 zilizohusisha ukatili kwa watoto wa chini ya miaka 18, zaidi ya kesi 143 zimefikishwa mahakamani huku 75 zikitolewa hukumu ya vifungo tofauti ikiwemo miaka 30 na wengine vifungo vya maisha.

Majira ya saa 10 jioni nafika hapa sokoni Mtwango wilayani Njombe nakutana  na mtoto, Michael Msigwa(7) akiwa na mdogo wake wa miaka miwili wanaoishi na bibi na mama yao.

“Tunaishi hapa na mama yetu pamoja na Bibi ambao wote wameenda shambani kupalilia mazao tangu saa 12 asubuhi, kurudi kwao huwa ni jioni. Chakuloa chetua hapa ni kande ambazo wametupiki jana usiku ambazo tutashindia siku nzima,” anasimua Msigwa.

Msigwa anasema kuwa anakosa muda wa kucheza na wenzake sababu yeye ndiye mlinzi wa mdogo wake.

“Nashindwa kucheza na wenzangu, nalazimika tu kushinda hapa nyumbani muda wote ili kumuangalia mdogo wangu,” anasema Msigwa.

Wakati Msigwa akieleza kukosa uhuru huo wa kusheza pamoja na kula chakula cha aina moja kila siku, upande wake, Mwanafunzi wa Kidato cha pili katika shule ya Sekondari Mtwango, Maria Sanga, ambaye humsaidia mama yake kuuza mgahawa anasema hali hiyo inamuathiri hata kimasomo sababu muda anaotoka kwenye biashara hizo si rafiki.

“Hii hali inaniathiri sana kwa sababu hapa tunatoka usiku naona vitu ambavyo sikustahili kuviona kwa umri wangu, lakini pia wakati mwingine nashindwa kwenda shule ili nije nisaidie kwenye biashara jambo ambalo halinisaidii kitaaluma,” anasema Maria.

Mmoja wa wakazi wilayani Njombe, Joseph Mwalongo anasema ni vema Serikali ikaendelea kutoa elimu kwa wazazi kutambua majukumu yao ya malezi ili shughuli za kiuchumi ziende sambamba na kuimarisha malezi kwa watoto.

Nae, Abu Mwabena anasema kuwa umasikini ndio chanzo cha wazazi kubaki upande wa kutafuta kipato na si watoto.

“Sio wazazi wote ambao wanaangalia kipato zaidi kuliko watoto, bali ni wachache ambao wamekosa elimu sahihi ya malezi pamoja na umasikini ambao ndio unasababisha wajikite katika biashara,” anasema Mwabena.

Mwabena anasema wazazi wasimame katika nafasi zao za majukumu kwa kutafuta njia sahihi ya kuwalea watoto pamoja na biashara zao.

Kwa upande wa Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Herieth Magaji anasema kumekuwepo na tabia ya wazazi kuwa bize na shughuli zao huku wakiwaacha watoto kujiamulia maisha ya kuishi wenyewe wakiwa nyumbani.

“Hii si sawa kumuacha mtoto peke yake au kwenda nae kwenye biashara ni hatari, hivi karibuni tulipata tukio la mzazi kwenda na mtoto wake mitaani katika biashara zake majira ya usiku na ukimuiliza anakwambia sina wa kumuachia baada ya kumuhoji sana akaamua kurudi nae nyumbani,” anasema Herieth.

Anasema bado elimu inaendea kutolewa kwa jamii ili ijue mipaka ya watoto na sheria inasemaje ili mtoto aweze kuwa salama.

Herieth anasema: “Huku Njombe kweli wanawake walio wengi wanajishughulisha na ndio walezi, sisi kama ustawi wa jamii sambamba na vyombo vya ulinzi na usalama tutaendelea kutoa elimu ili haki za mtoto zilindwe kwa sababu uwezi kukaa na mtoto hadi usiku au kumuacha nyumbani peke yake bila ya uangalizi,” anasema.

“Hatua zinapaswa kuchukuliwa pia kwa wazazi ambao wanaambatana na watoto kufanya biashara majira ya usiku, haikubaliki kwa sababu anaweza kufanyiwa vitendo vibaya vya ukatili ulawiti, ubakaji hata mauaji kwa sababu tuna historia hiyo,”anasema Herieth.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles