23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bakwata, Meya wawakumbuka yatima, watoa wito kwa familia

Na Clara Matimo, Mwanza      

Jamii imetakiwa kuwakumbuka watoto na kuhakikisha wanalelewa na kukua katika malezi bora pale wanapopoteza wazazi wao kuliko kuwaza mali na kuwasababishia  kuishi kwenye mazingira hatarishi.

Wito huo umetolewa jijini Mwanza Mei 3, mwaka huu na Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Costantine Sima, aliposhiriki  chakula cha pamoja na watoto  yatima, kilichoandaliwa  na Baraza  Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mfanyabiashara Zacharia Nzuki.

Alisema serikali inasisitiza umuhimu wa familia kutowatelekeza watoto lakini ndugu, jamaa  kuwatunza watoto yatima kwa kuwa  inatambua  jamii yote inaowajibu wa kuendelea kuwatunza kwa sababu nafasi mbalimbali za uongozi wa baadaye zitashikiliwa na watoto wa sasa.

 “Katika ujenzi  wa taifa lolote duniani ni lazima tuwahusishe watoto wetu yatima wakiwemo, leo upo una nguvu kesho nguvu zitakuishia utawahitaji, kama utawaharibu leo ukubali matokeo  mabaya ya kesho hivyo  tushiriki kujenga misingi yao tangu wakiwa wadogo.

“Watoto msikubali kudanyanywa na watu wazima wenye lengo la kuwaharibia maisha,  ambao mmepata nafasi ya kwenda shule kazanieni masomo yenu sasa hivi kila kitu kinahitaji elimu, kukosa wazazi, kuishi katika mazingira magumu na kuugua hayo siyo mwisho wa maisha yenu,”alisema Sima.

Akizungumza kwa niaba ya watoto hao, mtoto Al Bidh  Yusuph, (13) aliisihi  jamii kuwapenda  yatima na kuwahudumia mahitaji muhimu wasibahirie walivyo navyo kwani wanavyovitoa watavikuta kwa Mwenyezi Mungu kama ambavyo Mtume Mohamed alivyosema  kwamba mtu yeyote atakayeshika kichwa cha  mtoto yatima  na kujua anahitaji huruma, Mwenyezi Mungu anamuandikia baraka na kumfutia dhambi zote alizozifanya kwa kila nywele moja ya mtoto yatima aliyoigusa.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke, aliwataka  waumini  wa dini ya kiislamu kuwajali, kuwalea, kuwalinda na kuwathamini  watoto yatima kwani hayo ni maagizo ya  Mtume Mohamed ndiyo maana Bakwata mkoani humo  imejiwekea utaratibu wa kulisha yatima  Idd Mosi ya kila mwaka kwa kuwa   Idd El Fitri ni sikukuu ya kula.

“Mtume wetu Mohamed  alisema yeyote atakayelea  watoto yatima vizuri atakuwa  naye ahera siku ya kiama na watoto yatima inatakiwa walelewe ndani ya familia zetu wakifiwa na wazazi wao bado wanao ndugu wengine upande wa mama zao na baba zao.

“Zamani mtu akifa ndugu wanachukua watoto wake,  leo baada ya kufikiri watoto wa marehemu watalelewa vipi, wanawaza kuwadhulumu mali za wazazi wao,  watanzania turudi kwenye utaratibu wa kulea watoto yatima tukifanya hivyo hatutakuwa na watoto wanaoishi mazingira hatarishi, “alisema Sheikh Kabeke.

Kwa upande wake Zacharia Nzuki, alisema amewaandalia chakula kwa ajili ya sikukuu ya Idd El Fitr watoto hao kwa sababu ni kundi linalogusa kaya za watanzania wote kwa namna moja au nyingine huku akiihamasisha jamii kutowanyanyasa wala kuwabagua na kila mwenye nafasi ashiriki katika malezi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles