25.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 28, 2022

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Chama cha Mapinduzi hakikurupuki

Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakikurupuki katika kuiwekea malengo Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Amesema CCM imekuwa ikiielekeza Serikali kutekeleza shughuli za maendeleo kupitia ilani ya uchaguzi ambayo imesheheni mambo yote ikiwemo miradi mbalimbali kama vile ya afya, maji, elimu na miundombinu.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Alhamisi, Septemba 3, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Polisi wilayani Longido mkoani Arusha wakati akimuombea kura Rais Dk. John Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Longido Dk. Stephen Kiluswa.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli na sasa imeandaa ilani nyingine ya 2020-2025 ambayo nayo imeweka msisitizo katika masuala mbalimbali ikiwemo uboreshwaji wa huduma za jamii.

Akizungumzia  sekta ya mifugo, alisema sekta hiyo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi hivyo Serikali itaendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na tayari kiwanda kikubwa cha kuchakata bidhaa za mifugo kimejengwa Namanga, wilayani Longido.

Alisema kiwanda hicho  kinauwezo wa kuchakata ng’ombe 300 hadi 500 kwa siku, mbuzi na kondoo 3,000 hadi 4,000 kwa siku na kinatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 300. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza uzalishaji Septemba, 2020, amewataka wananchi wa Longido kuendelea kuiamini CCM.

“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2015 hadi 2020 Chama Cha Mapinduzi kilijielekeza katika kuhakikisha sekta ya ufugaji inaimarishwa ili kuwawezesha wananchi kunufaika na ukuaji wa sekta hiyo na mafanikio tumeyaona,” amesema Majaliwa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido, wagombea wa nafasi ya ubunge kwa tiketi ya CCM wa majimbo yote ya mkoa wa Arusha na wagombea wa udiwani wa Kata 18 za wilaya ya Longido ambao wote wamepita bila kupingwa.

Wengi ni pamoja na viongozi wa kimila wa kabila ya Kimasai ambao waliweka msimamo wa kuhakikisha wanamchagua Rais Magufuli pamoja na mgombea wa ubunge Dk. Kiluswa kutokana na kuridhishwa na utekelezaji wa shughuli za maendeleo zilizofanyika nchini ikiwemo na Wilaya ya Longido.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles