24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ACHUKUA SAMPULI YA MCHANGA BUZWAGI

Na PASCHAL MALULU-KAHAMA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Kampuni ya Acacia uliopo Buzwagi, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, kusitisha azma yake ya kupunguza wafanyakazi, baada ya Serikali kuzuia kusafirisha mchanga wenye chembechembe ya madini nje ya nchi.

Mbali na hilo, Majaliwa akiwa mgodini hapo alichukua sampuli ya mchanga kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi zaidi kujua kiwango cha madini kilichomo. Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza juzi jioni katika Mgodi wa Buzwagi, ambapo alitembelea na kukuta makontena mengine 180 ya mchanga yakiwa yameandaliwa kwa ajili ya kusafirishwa.

Alisema uamuzi wa Rais Dk John Magufuli wa kusitisha usafirishaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi uendelee kuheshimiwa na kusisitiza kuwa, suala hilo litamalizika mapema kwakuwa nia ya Serikali ni kujiridhisha zaidi.

Kuhusu usitishwaji ajira, Waziri Mkuu aliuambia uongozi wa mgodi huo kwamba, uamuzi wa Serikali kuzuia kusafirishwa kwa mchanga isiwe kigezo cha kuanza kufukuza wafanyakazi au kuwapunguza kwa namna yoyote ile.

 “Makontena haya yaacheni kwanza hadi taarifa ya majibu ya serikali itakapokamilika, kwani usafirishwaji huu una maswali mengi yanatakiwa kujulikana kwa Watanzania ambao wamekuwa wakihoji usafirishaji wake, hapa nabeba sampuli hii chache ya kwenda kubaini kuna madini aina ngapi ndani yake na kiwango cha dhahabu kilichomo ili baadaye tulinganishe na taarifa yenu ambayo mmekuwa mkitoa mara kwa mara kuwa ni mchanga usio na madini,” alisema Majaliwa.

Meneja wa mgodi huo, Stewart Hamilton, alisema wanaiomba Serikali kutoa taarifa hiyo ya mchanga mapema ili shughuli za usafirishaji ziendelee kama kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles