27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YATOA MAELEKEZO BANDARI, RELI

Na BENJAMIN MASESE-KAGERA


SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), kuandaa mfumo wa pamoja wa kutoa stakabadhi za malipo ili kurahisisha huduma za usafirishaji wa mizigo.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua maendeleo ya Bandari ya Kemondo mkoani Kagera pamoja na ukarabati wa meli ya MV Umoja.

Profesa Mbarawa alisema taasisi hizo za umma zinapaswa kushirikiana pamoja ili kutatua changamoto zinazowakabili watumiaji wa vyombo vya usafiri wa majini na kuzitaka kuwa na mfumo mmoja wa stakabadhi za malipo.

Alizitaka taasisi hizo kuanza haraka mchakato wa kuwa na mfumo wa stakabadhi moja ya malipo ili kuondoa adha kwa wateja wa mizigo.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa alisema, kukamilika kwa meli hiyo kutarudisha huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa Kanda ya Ziwa kupitia Bandari ya Kemondo, huku akiuagiza uongozi wa TRL kuharakisha ukarabati wa njia za reli bandarini hapo.

"Serikali imefanya ukarabati wa meli ya MV Umoja ambayo itabeba mizigo ikiwa kwenye mabehewa, reli hii inahitaji ukarabati mapema ipasavyo, nawaagiza TRL kufanya ukarabati wa reli ili kusiwepo usumbufu wowote wakati wa kushusha na kupakia mizigo hiyo.

“Pia nawaagiza mamlaka  zote kuhakikisha mnaanza kutafuta tena wateja ambao kwa muda mrefu walikuwa wamepotea kutokana na  bandari hiyo kusuasua kutoa huduma zake kwa muda mrefu, waelezeni kuwa mambo yamekaa sawa ili warejee kutumia usafiri huu,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa, Abel Moyo, alimhakikishia waziri kutekeleza agizo hilo kwa kushirikiana na TRL pamoja na MSCL.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa alitembelea na kukagua Kivuko cha Kyanyabasa, kinachotoa huduma katika Mto Kyanyabasa na kumtaka Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo, Mhandisi Zephrine Bahyona, kutoa huduma bora sambamba na kukusanya mapato ili kutatua changamoto ndogondogo zinazowakabili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles