27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI KUANZISHA MRADI WA MAZINGIRA

Na DENNIS LUAMBANO – MONDULI


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema Serikali inakusudia kuanzisha mradi wa mazingira utakaowasaidia wafugaji wasihamehame kutafuta malisho ya mifugo yao.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi alipozungumza na watumishi wa Wilaya ya Monduli kabla hajatembelea misitu ya Lendikinya na Monduli Juu.

January yuko katika ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kwamba shughuli za ufugaji zinategemea utunzaji wa mazingira kwa malisho na maji.

“Wamasai wanatakiwa kutunza zaidi mazingira kwa sababu yanaendana na shughuli zao. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kutotunza mazingira, hivi sasa wafugaji wanahama katika maeneo yao ya asili na kwenda maeneo mengine.

“Pia hali hiyo imewafanya Wamasai kukimbilia mijini kufanya shughuli nyingine, ikiwamo ulinzi na ususi kwa sababu wakibaki katika maeneo yao, hakuna malisho ya mifugo yao.

“Ushahidi wa hilo ni uharibifu wa ekari 1,400 za Msitu wa Lendikinya baada ya kuvamiwa na kuharibiwa, na wavamizi hao wasipodhibitiwa, msitu huo utapotea.

“Sisi serikalini hatuwezi kuruhusu hali hiyo itokee. Kutokana na hali hiyo, tutaanzisha mradi wa mazingira utakaokuwa maalumu kuwasaidia wafugaji, hasa wa Monduli na Longido wasihame ili kuepuka migogoro inayoepukika,” alisema January.

Akikagua chanzo cha maji cha Sailojia kilichopo Kijiji cha Kiranyi, Kata ya Kiranyi, Wilaya ya Arusha Mjini, January aliagiza wote waliojenga karibu na chanzo hicho waondolewe kwa kufuata taratibu za sheria.

Aliitaka kamati iliyoundwa kwa kuwajumuisha wanakijiji na maofisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha Mjini kushughulikia mgogoro wa watu waliojenga karibu na chanzo hicho, kumaliza kazi yake haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles