22.6 C
Dar es Salaam
Sunday, May 5, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI: HAKUNA MISHAHARA MIPYA

 

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli amesema tangu alipoingia madarakani hajapandisha mishahara ya watumishi wa umma na  hatapandisha kwa sababu  anawatumikia Watanzania kwanza.

Kauli hiyo aliitoa   Dar es Salaam jana alipofungua Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ambao uliwakutanisha mameya na wenyeviti wa halmashauri nchini.

Rais Magufuli alieleza umuhimu wa ALAT katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mikakati yake kwa Watanzania.

Aliahidi kushughulikia changamoto za uhaba wa watumishi katika halmashauri na ucheleweshwaji wa ruzuku ya miradi ya maendeleo.

AWEKA WAZI MSHAHARA WAKE

Katika mkutano huo, Rais Magufuli pia alitaja mshahara wake anaolipwa kuwa ni Sh milioni tisa kwa mwezi.

“Watu walikuwa wanafanya ‘board meeting’ Dubai na wakienda kule wanapandisha mshahara mpaka Sh milioni 40, mimi mshahara wangu ni Sh milioni tisa. Naeleza ukweli. Watu walikuwa wanafanya kufuru,” alisema.

POSHO KWA MADIWANI

Akijibu mapendekezo ya ALAT ya kuongezewa posho ya madiwani kutoka  Sh 350,000 hadi Sh 800,000 kwa mwezi, aliwaomba viongozi hao kuwa wavumilivu na kufanya kazi kwa lengo la kuwatumikia Watanzania.

“Leo ukiniambia niongeze posho za madiwani maana yake nisipeleke madawa hospitalini, maana yake nisipeleke Sh bilioni 300 za watoto wetu kusoma.

“Hivyo niwaombe viongozi wetu tufanye kazi, tuwe wavumilivu. Na ndiyo maana nilipoingia madarakani sikupandisha mishahara na sitapandisha,”alisema Rais Magufuli.

Akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, Mei Mosi mwaka huu, Rais Magufuli aliahidi nyongeza ya kawaida ya mishahara na kuwapandishia madaraja wafanyakazi wanaostahili.

“Watumishi 9,932 walikuwa na vyeti feki, watumishi hewa walikuwa 19706, hivyo kama Serikali ingeongeza mishahara ina maana watumishi hawa pia wangefaidika na fedha ambazo hawakustahili kuzipata,”  alisema Rais Magufuli.

Pia alisema wafanyakazi 12,000 ‘waliotumbuliwa’ kwa vyeti feki hawawezi kumpenda na ndiyo maana wanapiga kelele kupitia mitandao ya  jamii kwa sababu  naye hahitaji kupendwa nao.

“Watu 12,000 waliotumbuliwa kwa vyeti feki hawawezi kunipenda na hao ndiyo wanaopiga kelele kwenye mitandao huko. Tanzania ina watu milioni 52 sasa hawa (12,000) hata hawanisumbui, nikiwaona ‘I just enjoy them’ hata sishtushwi na wanaolalamika.

“Ukimtumbua mtu jipu hawezi kufurahi akipona ndiyo ataanza kuelewa,”alisema.

DIWANI ASIYE NA KAZI AJIUZULU

Alisema endapo kuna diwani ambaye hana kazi ya kumpatia kipato huku akitegemea posho tu, ajiuzulu.

“Diwani unatakiwa uwe na kazi ya kukupatia kipato, unapojaza fomu za kugombea udiwani kuna sehemu unajaza kuwa uwe na kazi ya kukupatia kipato. Sasa kama kuna diwani hana kazi ya kumpatia kipato ajiuzulu,” alisema.

Alisema mwaka jana serikali haikuajiri wafanyakazi kwa sababu ilikuwa inasafisha kwanza na kuwaondoka wenye vyeti feki na wafanyakazi hewa.

“Kuhusu suala la wafanyakazi mwaka, jana hatukuajiri labda sehemu tu muhimu kwa dharura  kwa sababu tulikuwa tunataka kusafisha kwanza maana usingemleta mgeni kwenye nyumba ambayo ni chafu.

“Mtu atatoka na mafua, atatoka na kunguni hivyo tusingewachanganya mle… tulichokuwa tunafanya kwanza ni kuwaondoa wenye vyeti feki na wafanyakazi hewa.

“Mwaka huu tumetangaza nafasi za kazi, Wizara ya Afya wametangaza nafasi 3000, jeshini wametangaza na walimu nadhani wametangaza,”alisema.

Aliwataka wakurugenzi nchini kutowaajiri wenye vyeti feki hata kama ni ndugu zao kwa sababu  watawapa matatizo.

“Msije mkaajiri tena wenye vyeti feki hat kama ni ndgu yako achana naye atakuharibia maisha… nafuu upokee mshahara wewe ukampe kama unataka uishi vizuri.

“Hivyo niwaombe wakurugenzi wote kaajirini watu wenye qualification  kwenye sekta husika, nafasi ziko wazi lakini mkazisimamie.

“Tulipoingia tulikuwa tunalipa mishahara Sh bilioni 777 lakini tumepunguza mpaka mwezi uliopita tumelipa Sh bilioni 251 na wakati huo huo tunalipa deni la Sh bilioni 950,”alisema Rais Magufuli.

Pia aliwaambia ALAT   wazipe kipaumbele fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo kwa sababu imebainika mara nyingi utekelezaji wa miradi hauendani na fedha zinazotolewa.

“Tafadhalini zipeni kipaumbele pesa za Serikali. Nchi zinazoendelea wananchi wake hawakwepi kodi, niwahakikishie kuwa kila senti itakayokusanywa itatumika kwa ukamilifu,” alisema.

PENSHENI ZA WATUMISHI HEWA

Rais Magufuli aliagiza Sh bilioni 38 zilitokana na waliokuwa watumishi hewa zirudishwe serikalini.

“Zile pensheni zote za watumishi hewa zirudishwe serikalini, Sh bilioni 38 zirudishwe serikalini. Likizo hewa, likizo za uzazi hewa. Tunachukua hatua lakini ni kwa Taifa la Watanzania. Tulikuwa tunaenda kubaya, kuzimu,” alisema.

WAKURUGENZI WALEVI

Kiongozi huyo wa nchi alitumia mkutano huo, kuwaonya wakurugenzi wa halmashauri nchini ambao wanajihusisha na ulevi  wa pombe   akiwataka waache mara moja.

Ingawa hakuwataja kwa majina, alisema   wapo watumishi watatu walevi na kwamba anazo taarifa zao hivyo waache na wawatumikie wananchi.

“Nimepata taarifa kuwa kuna wakurungezi watatu, kama wanne ni walevi sana, hao lazima wataondoka, mimi nazungumza kwa uwazi. Wewe kama ni mkurungezi na unakunywa pombe kaa mbali na pombe… ukienda huko wakuone umebadilika,”alisema.

BENKI UFISADI

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema kulikuwa na benki moja   nchini ambayo ilipata hasara ya asilimia sita na hata ilipoongezewa fedha ilipata hasara zaidi.

“Ikapata hasara zaidi ikaongezewa hela sasa ikapata hasara ya asilimia 11 ikaongezewa hela ikapata hasara zaidi asilimia 22. Sasa tumeifunga.

“Watu kama hawa hawawezi kutupenda na mimi sitaki wanipende ilimradi napendwa na watanzania. Sikuja kuuza sura, nimependwa na mke wangu inatosha,”alisema.

Alisema kuna  benki makao makuu yake yalionekana Dar es Salaam lakini imefunguliwa Marekani na   hata wataalamu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hawakuligundua hilo.

“Kuna benki makao makuu yake yako Dar es Salaam lakini ikafunguliwa kule Marekani. Wataalamu wa BoT hawakugundua haya na fedha ambayo ipo kwenye hiyo benki haizidi asilimia tano,” alisema Rais Magufuli.

 

PEMBEJEO HEWA

Alisema kwenye halmashauri 140, kulikutwa na pembejeo hewa za kilimo zenye thamani ya Sh bilioni 57.9.

“Hata Chato kwetu kulikuwa na huu uozo pembejeo hewa za thamani ya Sh bilioni 1.5.

“Wanafunzi hewa 65,000 kutoka elimu ya msingi mpaka chuoni. Wanafunzi hewa wanaopokea mikopo walikuwa 8500.

“Ungekuwa mimi umekuta li-Tanzania liko hivi, uozo kila kona ungefanyaje? Ningekuwa Mhehe ningejinyonga, ningesema “Swela,”  alisema.

Alisema wakati anaingia madarakani alikuta mikoa mingi inasumbuliwa na kipindupindu lakini baadaye yalipelekwa madawa.

Pia alisema   bei ya mbolea ya kupandia imeweza kushuka, mathalani katika Mkoa wa Lindi kutoka Sh 100,00 hadi  Sh 51,000.

Alisema yanayofanyika kwenye migodi ni mambo ya ovyo huku nyaraka zikisainiwa na watanzania kwamba watu fulani wasilipe kodi wala ushuru.

“Kule kwenye Tanzanite, katika uuzwaji wa Tanzanite duniani kote Tanzania imepata asilimia tano tu na asilimia 95 kuliwa na nchi nyingine.

“Halafu mnataka nisiseme kwa sababu gani? Kisa kuogopa uhai wangu? Mlinichagua wa nini sasa!

“Tumekalia uchumi wetu na sisi viongozi lazima tueleze ukweli. Ndiyo maana pale tanzanite tumejenga uzio na thamani ya uzio hata hauzidi Sh bilioni sita.

“Na ndiyo maana tulivyozuia kidogo tu, uzalishaji wa tanzanite umepanda zaidi ya mara 30, siku moja walipata zaidi ya kilo 18, haijawai kutokea.

“Najua wapo walioumia na mabadiliko haya, kwa kiingereza wanasema ‘no sweet without sweat’ au ‘no pain no gain’ ila watu wengi wanaolalamika hivi sasa ni wale waliokuwa wanategemea mfumo wa zamani, alisema.

Alisema wapo watu ambao wanalalamika fedha imepotea na kwamba wanaolalamika ni wale ambao walizoea vya bure.

“Apartment zilikuwa zimepangishwa mtu ana washikaji 10 na wote anawatunza, wengine hadi baa walikuwa wanalipia viti kwamba kila siku lazima akae hapo. Watumishi wengine walikuwa wanasafiri kila wiki, wanabadilishana mabegi pale airport,”alisema Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Mmeifunga, je Mmewafunga na kuwapokonya mali zao? Kukimbiza si tija, Je ni nini mnachukua kisheria. Taifisha mali zao zote na wasweke ndani wote. Hapo nitakusifu. Si ngonjera maneno kila siku. Hayaendani na vitendo. Watu wanakuchezea hapa, unawahamishia pale, wengine unawateua tena. Hii ni kupoteza muda wa Watanzani. Adhabu haziendani na makosa. Hawa wote ni wanaCCM Mzee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles