25.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Msalala wampongeza Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MADIWANI wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, Shinyanga wamemwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Mboni Mhita na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mary Mhoha kufikisha salamu za pongezi kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Ni kutokana na kuongeza fedha kwa ajili ya kuimarisha sekta ya elimu, afya, barabara, maji na nishati ya Umeme Vijijini kupitia mradi wa REA katika halmashauri hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani, wakuu wa idara na vitengo katika ukumbi wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki. Hoja ya pongezi kwa Rais Samia kwa niaba ya madiwani wa halmashauri hiyo, ilitolewa na Diwani wa Kata ya Mwakata, Sixbert Ibrahim ambapo iliungwa mkono na madiwani wote waliohudhuria mafunzo hayo.

Sixbert alisema, hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita kuelekeza fedha kwenye miradi mbalimbali kwenye wilaya hiyo, inatoa fursa kwa Halmashauri ya Msalala ‘kukimbia’. Katika mafunzo hayo, Mhita alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Khamis Katimba kwa jitihada na mikakati yake aliyoionesha katika muda mchache tangua aingie kwenye halmashauri hiyo.

“Halmashauri imepata mtu makini sana, tuungane naye kuhakikisha malengo yake mapana yanafikiwa. Kwa muda mchache tumeona mwelekeo wake chanya,” alisema. Kwenye mafunzo hayo, Mhita pia alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme kwa kukubali ombi la kutoa wakufunzi wawili kuwezesha mafunzo hayo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya maendeleo.

Madiwani hao walimpongeza mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mibako Mabubu na mkurugenzi wake (Katimba), kwa kuwezesha mafunzo hayo pamoja na mambo mengine, yalilenga viongozi hao kujua mipango ya bajeti ya halmashauri inayopanga hivyo kuwa rahisi kwao kufanya ufuatiliaji katika ngazi mbalimbali.

“Ninawaomba waheshimiwa madiwani kutokukubali vyanzo vya mapato kutoroshwa katika maeneo yenu ya utawala,” alisema Katimba.

Katibu Tawala wa Wialaya hiyo, Mohamed Mbega amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni ili kulinda heshima na maadili ya uongozi. Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Abdallah Urari amewaomba viongozi hao kutoa ushirikiano kwa maafisa wa taasisi hiyo.

Alisema kwamba, taasisi hiyo ina mpango wa kutembelea kata zote kwa ajili ya kuanzisha huduma ya TAKUKURU RAFIKI, yenye lengo la kuongeza uwajibikaji na utoaji huduma bora kwa jamii na kutatua changamoto.

Hata hivyo alisema, taarifa za udanganyifu katika ukusanyaji mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa baadhi ya wataalamu na viongozi wa halmashauri hiyo pamoja na ‘upigaji’ kwa madiwani, zipo mezani kwake, ameonya tabia hiyo na kuahidi kufanyia kazi taarifa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles