24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati ya Bunge yaipongeza Serikali kwa mazingira mazuri ya uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba kunakuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.

Pongezi hizo zimetolewa na jana Kamati hiyo ilipofanya ziara katika viwanda vya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kufuatilia uzingatiaji wa taratibu muhimu za usalama na afya kazini miongoni mwa waajiri nchini.

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wawekezaji wa kiwanda cha Buguruni Flour Mills pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao kifupi cha kutoa mrejesho mara baada ya wajumbe hao kutembelea maeneo ya uzalishaji ya kiwanda hicho wakiambatana na wakaguzi wa OSHA.

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara katika viwanda vya Bakharesa Flour Mill kilichopo Buguruni na kiwanda cha bidhaa za chuma cha Lodhia Steel Industries Ltd cha Mkuranga Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Hassan Toufiq ameipongeza serikali kwa kuwawezesha wawekezaji nchini kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija.

“Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu ya kawaida na tumefurahi kuona wenye viwanda tuliowatembelea leo wamepata mafanikio makubwa katika shughuli zao kwani wanafanya uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi yetu. Wawekezaji hawa wamekiri kupata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambao wamekuwa wakiwasaidia katika kuweka mifumo ya kudhibiti ajali na magonjwa pamoja na kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme na mitambo ya uzalishaji jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa ufanisi wa mitambo husika pamoja na kuiweka katika hali ya usalama wakati wote,” amesema Mwenyekiti Fatma Toufiq.

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (wapili kushoto), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Hassan Toufiq (watatu kushoto),Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (nyuma ya Waziri Ndalichako) pamoja na Wajumbe wa Kamati hiyo wakisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu wa maabara ya kiwanda cha Bakhresa (Buguruni Flour Mills) inayotumika kupima ubora wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa katika kiwanda hicho.

Aidha, Toufiq amesisitiza kuwa uwekezaji katika viwanda ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi kutokana na faida zake zikiwemo kuzalishaji ajira nyingi, kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu pamoja na kuongeza pato la Taifa kupitia ulipaji wa kodi.

“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hasa kwa wawekezaji wa ndani. Tunaishauri serikali kuendelea kujenga mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili wawekezaji wetu wazidi kukua na kuongeza mtandao wa uzalishaji wao ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,” amesema Toufiq.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Boniface Mwita, amesema uwekezaji nchini kwa kiwango kikubwa bado unategemea nguvukazi zaidi hivyo ni muhimu kuwekeza katika mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.

Awali, wakurugenzi wa viwanda vilivyotembelewa (Bw. Hussein Sufiani-Mkurugenzi wa Mahusiano wa Bakharesa Flour Mill na Sailesh Pandit-Mkurugenzi wa Lodhia Steel Industries Ltd) waliieleza Kamati jinsi walivyoweza kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uzalishaji kutokana na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA wanapofanya ukaguzi wa usalama na afya katika maeneo yao kila mwaka.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Ali Hassan King (aliyesimama) akitoa ushauri kwa wawekezaji wa kiwanda cha chuma cha Lodhia Industries juu ya namna sahihi ya kuboresha mifumo ya usalama na afya katika kiwanda hicho mara baada kubaini baadhi ya changamoto wakati kamati hiyo ikiambatana na wakaguzi wa OSHA kufanya ukaguzi katika kiwanda hicho.

Kwa upande wake Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu amesema: “Kwa kuzingatia wajibu wa Wizara ya Kazi na Taasisi chini yake ambao ni kusimamia uwepo wa mazingira mazuri ya kazi na kuhakikisha kwamba viwango vya kazi vinazingatiwa, tutaendelea kutekeleza wajibu huo ipasavyo kama tulivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani. Hivyo, niwasihi wawekezaji kuendela kutekeleza taratibu mbali mbali za kazi ikiwemo kuhakikisha kwamba wanalinda afya na usalama wa wafanyakazi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewashukuru wawekezaji kwa kutambua mchango wa OSHA katika kukuza biashara zao na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuboresha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akizungumza na mwakilishi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma cha Lodhia Industries Ltd wakati wa kikao kifupi cha kutoa mrejesho mara baada ya wajumbe wa Kamati kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji ya kiwanda hicho wakiambatana na wakaguzi wa OSHA.

“Tunawaomba wadau wetu waendelee kututumia ili kwa pamoja tuweze kulinda afya za wafanyakazi na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji kwani hakuna jambo lenye thamani zaidi ya uhai wa binadamu.Kazi ni uhai, kazi ni staha kwahiyo lazima tusimamie uwepo wa kazi zenye staha kwani pamoja na kwamba usalama na afya ni suala la kisheria lakini masuala ya usalama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles