24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wataka kanuni mpya za habari kutotambua uchochezi kwa wanahabari

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga ameshauri kanuni za habari ambazo zipo njiani kutungwa, zipoze suala la makosa ya kihabari kuitwa uchochezi.

Dk. Henga ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha siku moja cha Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), kilichoitishwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Kikao hicho kililenga kupitia vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari vilivyopitishwa na bunge mwaka huu pia kuangalia mwelekeo wa Kanuni za Habari abazo zipo njiani kutungwa.

“Sera ya habari inayokuja, ipooze hili suala la wanahabari kuitwa wachochezi. Iondoe yale makosa ya jinai kwani suala la kupashana habari halipaswi kuwa na jinai ndani yake,” alisema.

Dk. Henga alisema, suala la kupashana habari ni haki ya kikatiba, na makosa yanaweza kutoka kama ilivyo kwa manaadamu yoyote hivyo, kufanya makosa hayo ya kitaaluma kuwa jinai, ni kuifinya tasnia ya habari.

“Katiba yetu Ibara ya 18 inasema, mtu ana haki ya kutoa, kupokea na kupata habari. Kanuni zitu zizipe ile mianya inayomtia mashaka mwanahabari,” alisema Dk. Henga.

Pia alishauri serikali kuendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wanahabari kama ilivyo nia ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba, inawezekana sheria kurejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho hata kama haijaanza kutumika.

“Wito wangi, sheria haikatazi kufanya mabadiliko ya sheria mara kwa mara, kwa kuwa sheria ya habari bado ina kasoro, inaweza kupelekwa tena bungeni na kurekebishwa,” alisema.

Kwa upande wake, Dk. Darius Mukiza kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari cha SJMC, alishauri mafunzo kuhusu sheria ya habari yanapaswa kutolewa vyuoni.

“Mambo yote kuhusu sheria ya habari yanapaswa kuingizwa kwenye vyuo vya habari, vijana wanatoka vyuoni wakiwa hawajui chochote kuhusu sheria hizi,” alisema Dk. Mukiza.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TEF, Neville Meena alisema, wanahabari wasio na sifa ya elimu inayohitajika katika tasnia ya habari, wanapaswa kushinikizwa kufanya hivyo kwa kuwa fursa ipo.

“Tutakua watu wa ajabu kama tutaendelea kukumbatia watu wasio na sifa kwenye tasnia ya habari, fursa ipo tuwahimize ili wawe na sifa,” alisema Meena.

Makamu Mwenyekiti wa MISA, James Marenga TAN alisema, hatua ya Bodi ya Ithibati kusimamiwa na serikali, inanyima uhuru wanahabari kujisimamia.

“Bodi ya Ithibati wajumbe wake wanateuliwa na waziri, kinasimamiwa na waziri kwa maana ya serikali na ndicho chenye mamlaka ya kusimamia waandishi na hata kuwanyang’anya leseni. Hili linanyima uhuru wanahabari,” alisema Marenga.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema, mchakato wa kutunga nanuni za habari unakaribia kuiba, hivyo ameishauri serikali kukutana na wadau wa habari na kupitia kanuni hizo kabla ya kuanza kutumika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles