24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu kuwapeleka vigogo polisi mahakamani  

lisuAZIZA MASOUD NA HARRIETH MHUNGA (SJMC), DAR ES SALAAM

MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ametoa siku tatu kwa viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi kuwaachia vijana kumi waliokamatwa katika mikoa mbalimbali na kuwekwa mahabusu bila kufikishwa mahakamani kwa madai ya kusambaza jumbe za  uchochezi.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema viongozi hao wa polisi wasipotekeleza agizo hilo atapeleka hati ya dharura ya ombi la kisheria Mahakama Kuu (Habeas corpus) Jumanne ijayo ambayo itawataka  viongozi hao kufika mahakamani hapo kutoa maelezo ya kuwashikilia vijana hao bila kuwapatia dhamana wala kuwafikisha mahakamani.

Akizungumza jijini jana katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema, Lissu aliwataja wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo cha Oysterbay kuwa ni pamoja na Aristotle Magasi, Hosia Mbuba, Ignasia Mzenga, Shakira Abdallah Makame.

Wengine ni Dk. David Nicas aliyekuwa mgombea ubunge wa Busega, Mdude Nyangali, Juma Salum na Suleiman Said.

Na upande wa kituo cha kati wanaoshikiliwa ni Ben Nzogu na Mussa Sikabwe.

Lissu alisema polisi wamekuwa wakiwakamata vijana kinyume cha sheria ambao wanatuma jumbe mbalimbali zinazodaiwa kuwa ni za kichochezi kwakuwa zinakosoa Serikali ya Rais John Magufuli.

“Kuna vijana kumi kati ya hao wawili wapo Kituo cha Kati na wanane wapo Oysterbay wanashilikiwa na polisi bila kupelekwa mahakamani wala kupatiwa  dhamana na hawa ni wale ambao tunawajua lakini wapo wengine 73 hatujui walipo hadi sasa makosa yao ni kutuma jumbe za kumpinga Rais Magufuli mitandaoni na yupo mwingine inadaiwa alituma tu video ya dikteta uchwara ambayo nilikuwa nikiongea mimi, wapo wanaokaa mahabusu wanateswa kinyume cha sheria za nchi.

“Hawa lazima tuwasemee ili tuwasaidie watoke na kwa sababu Jumatatu ni sikukuu, Jumanne tutaenda Mahakama Kuu kupeleka hati ya kisheria ya Habeas corpus, hii maana yake mlete haraka ili viongozi wote wa polisi wakiwemo makamanda wanaowashikilia waende wakajieleze mahakamani,” alisema Lissu.

Alisema amri hiyo itakuwa utekelezaji wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 390, inayoruhusu Mahakama Kuu kutoa amri na kuelekeza mtu yeyote ambaye anashikiliwa  kinyume cha sheria kupelekwa mahakamani au kuachiwa huru.

Alisema vijana hao mbali na kushikiliwa, pia wapo wanaoteswa na kikosi kazi cha polisi kinachojumuisha watu mbalimbali kutoka taasisi za vyombo vya dola ambapo watuhumiwa hao hutolewa usiku na kupelekwa katika jumba moja lililopo Mikocheni.

“Nimeongea na wale wanane waliopo Oysterbay wao waliniambia mbele ya OCS kuwa wanateswa sana, wapo waliotolewa Mbozi kuanzia wanakamatwa hadi wanafikishwa Dar es Salaam ni wanateswa tu.

“Wanatolewa usiku na kupelekwa  Mikocheni kuteswa wanapigwa na marungu wakiwa wamevuliwa nguo wakirudi wanakuwa nyang’anyang’a, wengine wamevunjika viungo, wawili waliopo Central kwa zaidi ya wiki mbili sasa hawa hawana shida, hii imewatokea kwa sababu si viongozi na hawajulikani tusipochukua hatua maana yake watu wetu watakuwa wanateswa kila siku,” alisema Lissu.

Alisema mbali na hao, pia walipata taarifa kuna watu wamekaa mahabusu siku 46 na kuachiwa wiki hii jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Alisema polisi wanafanya matendo kama vile nchi haina sheria na kusisitiza kuwa hakuna sheria ambayo inaruhusu mtu kukaa mahabusu zaidi ya saa 24 na endapo atakuwa amekamatwa siku za mahakama anapaswa kufikishwa mahakamani siku inayofuata.

Alisema Jeshi la Polisi linavunja Katiba kwa kuwatesa wananchi katika vituo vya polisi  bila amri ya mahakama kwa sababu tu ya kutuhumiwa kufanya makosa jambo ambalo ni kinyume na Katiba ibara ya 13 (6)(e) ambayo inaeleza ni marufuku mtu kuteswa au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.

Alisema katika Katiba hakuna kifungu ambacho kinaonyesha mtu akivaa tisheti yenye maandishi ya maneno kama Ukuta wanavunja Katiba hivyo ni wazi kuwa polisi wanafanya vitendo kinyume cha sheria.

“Mimi hakuna wakunifunga mdomo si Mahakama wala polisi, nasema anayevaa tisheti ya Ukuta hana kosa lazima mjue  hakuna makosa ya hivyo kwenye Katiba,” alisema Lissu.

Aliongeza makosa wanayoyafanya vijana hao ni wazi na wanapaswa kupatiwa dhamana kwakuwa hawajatiwa kizuizini kama sheria ya kumtia mtu kizuizini inavyoeleza.

“Ipo sheria inayomruhusu mtakatifu rais akiamua kumtia mtu kizuizini, hawa hawajawekwa kizuizini hakuna hata mmoja kati ya hawa ambao wanastahili kuwekwa kizuizini kama ilivyo kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1962 hawa wamefanya makosa ya kawaida kabisa,” alisema Lissu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles