23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo sita Ukawa wakutana faragha  

furaha-2NA WAANDISHI WETU

VIONGOZI wa juu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana walikutana jijini Dar es Salaam na kufanya kikao kizito cha faragha kwa saa tatu.

Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi binafsi za aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa, zilizopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam, inaelezwa pamoja na mambo mengine kilijadili mwenendo wa kisiasa nchini na ule unaovigusa moja kwa moja vyama vyao.

Katika kikao hicho nyeti ambacho ajenda zake hazikuwekwa wazi, viongozi sita  wa umoja huo walihudhuria.

Viongozi  hao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na Lowassa.

Mbali na viongozi hao kikao hicho kilihudhuriwa pia na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru na Balozi Timoth Bandora.

Viongozi wawili waliokuwa wahudhurie kikao hicho, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, hawakuhudhuria kutokana na dharura.

Taarifa za kuaminika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa pamoja na mambo mengine kikao hicho kilizungumzia mvutano wa kisiasa unaoendelea ndani ya CUF pamoja na kauli tata alizozitoa wiki iliyopita Rais John Magufuli wakati akiwa ziarani visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hizo mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ambao umeshuhudia kuvuliwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, ndio unaonekana kuwapasua vichwa viongozi hao hasa baada ya kuwapo kwa taarifa za kusukwa njama za kumwondoa ndani ya chama hicho, Maalim Seif.

Lipumba ambaye wiki hii amezungumzia hatima yake akisema sasa ipo mikononi mwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, lakini pia kitendo cha kulitaja jina la Lowassa moja kwa moja kama lipo nyuma ya mkakati wa kumng’oa ndani ya chama hicho ndiko kunakotajwa kuwasukuma viongozi hao kukutana ili kuangalia namna ya kushughulika na suala hilo.

Juzi katika mahojiano na kituo cha redio cha Clouds FM, Profesa Lipumba alisema mkutano wa chama hicho wa kumridhia Lowassa kuingia Ukawa ulifanyika Zanzibar bila yeye kuhusishwa kitendo kinachoonyesha kuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif alikuwa akimzunguka.

Mbali na tuhuma hiyo, kiongozi huyo alisema hatakuwa tayari kuona Chama cha CUF kikinunuliwa kwa bei chee na Lowassa au Chadema hata kama atakuwa nje ya chama hicho.

Katika maelezo yake, licha ya kusimamishwa uanachama lakini yeye alidai kuwa bado ni Mwenyekiti wa chama hicho kwa kuwa mamlaka iliyomchagua haijatengua nafasi yake kwa kuthibitisha barua yake ya kujiuzulu.

Mbali na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, pia taarifa za ndani zaidi zimelidokeza gazeti hili kuwa viongozi hao walifanya uchambuzi wa kauli tata alizozitoa Rais Magufuli wakati akiwa visiwani Zanzibar wiki iliyopita.

Moja ya kauli tata alizozitoa Rais Magufuli visiwani humo ni ile ya kupendekeza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, apewe tuzo kwa kusimamia uchaguzi vizuri.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na vita baridi kati ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif na mgombea wa CCM, Dk. Shein.

Kauli nyingine ni ile ya kuhoji sababu za  Dk. Shein kuendelea kusaini posho na mahitaji mengine kwa ajili ya Maalim Seif ambaye alikataa kumpa mkono wa salamu wakati wa mazishi ya aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais Abdu Jumbe Mwinyi.

“Juzi juzi tumeshuhudia hapa, Watanzania wote wa vyama vyote wameshuhudia, dunia yote imeshuhudia na vyombo vya habari navipongeza sana vilituonyesha, mtu mmekutana kwenye msiba, mahali kwenye majonzi, mnamsindikiza marehemu atangulie mbele ya haki kwa unyenyekevu wako Dk. Shein ukatoa mkono wako kumsalimu mtu fulani, huyo mtu akakatalia mikono yake, haya ni mapenzi makubwa sana,” alisema Dk. Magufuli.

“Halafu huyo mtu aendelee kula ruzuku kwa kusaini na mkono wako huo huo uliokataliwa, huyo huyo akiugua unampeleka hospitali, kwa kusaini posho ya kwenda hospitali, huyo huyo akitaka kusafiri kwenda nje unasaini, unampa posho na hela za kwenda nje, mimi nisingeweza,” alisema Rais Magufuli.

Wakati hayo yakijiri, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kubeba msalaba wake wa usaliti huku akisisitiza kwamba msomi huyo kwa sasa ameanguka kifikra.

Lissu ambaye alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na kauli ya Profesa Lipumba kwamba Chadema ipo katika mkakati wa kuiua CUF bara, alikumbushia historia ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake kikiwa chini ya Profesa Lipumba.

Mwanasiasa huyo machachari alisema wakati Profesa Lipumba akiwa Mwenyekiti na hata mgombea urais chama chake hicho hakijawahi kupata wabunge wengi kama kilivyopata mwaka jana wakati mgombea urais akiwa Lowassa.

“Profesa Lipumba anaposema Chadema ina njama ya kuibomoa CUF takwimu zikoje na hali ilikuwaje kabla ya Ukawa, hali ikoje baada ya Ukawa, hoja ya Profesa inaonyesha jinsi gani msomi huyo alivyoanguka kifikra hata task tu za kawaida hazioni,” alisema Lissu.

Alisema chini ya uongozi wa Profesa Lipumba na akiwa mgombea urais kwa miaka yote CUF ilikuwa ikipata wabunge wasiozidi wawili Bara.

“Ukawa ambao Lipumba aliuanzisha baadaye akausaliti, CUF kilipata wabunge kumi Bara wa majimbo miaka mingine yote haijawahi kutokea, kama Chadema ingekuwa inaibomoa CUF katika uchaguzi wasingepata kabisa ama kingepata pungufu ya viti walivyokuwa navyo awali lakini kwakuunganisha nguvu wakapata matokeo mazuri,” alisema Lissu.

Alisema kipindi cha uchaguzi Profesa Lipumba akiwa kama Mwenyekiti  mwenza wa Ukawa alimpokea mgombea urais Edward Lowassa na kukaa mwezi mzima baadaye nafsi yake ikamsuta na kukimbilia Rwanda kufanya utafiti.

“Alienda Rwanda sijui kufanya utafiti, lakini mwaka mmoja baadaye nafsi yake ilimsuta tena akaona uenyekiti wake haujafa bali ulizimia tu, aliona uenyekiti haujawa marehemu karudi, kwa kifupi ya Profesa Lipumba yasiwasumbue wanachama wa CUF wala sisi hayatusumbui yanawasumbua hao waliomtuma tu,” alisema Lissu.

Aliongeza kuwa Ukawa pia ulisaidia kumpatia ushindi wa asilimia 54 Maalim Seif kwa Zanzibar, huku mgombea urais wa Jamhuri kupitia umoja huo Lowassa akipata kura nyingi zaidi Zanzibar kushinda Rais John Magufuli.

Profesa Lipumba ambaye hivi karibuni alisimamishwa uanachama, alitangaza kuachia nafasi zake zote ndani ya CUF katika ya kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa madai kuwa nafsi yake ilimsuta baada ya umoja huo kumsimamisha Lowassa kugombea urais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles