24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 28, 2023

Contact us: [email protected]

Kwaheri ‘mpambanaji’ Samuel John Sitta

sitta-2Na Owen Mwandumbya

TAIFA lipo katika maombolezi ya kuondokewa na mwanasiasa mkongwe na Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010) Samuel Sitta.

Taarifa za kifo cha Sitta kimelishtua Bunge kama chombo alichowahi kukiongoza akiwa Spika kwa takribani miaka mitano.

Falsafa yake ya ‘Standard and Speed’ (Kasi na Viwango) ilikifanya chombo hiki cha kutunga sheria kipate mvuto mbele ya umma wa Watanzania ambao pengine hawakuyajua majukumu yake na hata kufuatilia kwa ukaribu shughuli za mhimili huu.

Nikiwa mwanafamilia wa Ofisi ya Bunge, namlilia Sitta, sambamba na watumishi wa Bunge. Nimepata fursa ya kumfahamu na kufanya naye kazi katika kipindi chake cha uongozi ndani ya Bunge na wakati wa Bunge la Katiba mwaka 2014.

Si rahisi kumwelezea ikatosha kwa makala moja, kama mtumishi wa Bunge, nimebahatika kuchota mengi kutoka kwake hasa kupitia matendo yake na namna alivyoongoza mhimili huu wa Bunge.

Yako mengi ambayo daima yatabaki kuwa ni jitihada za Sitta ambayo tunaendelea kujivunia hivi sasa katika mhimili huu. Moja ya mambo ambayo hakika kila mbunge atamlilia na kumkumbuka ni pamoja na kupigania, kusimamia na hatimaye kutungwa kwa Sheria ya Mfuko wa Jimbo (Constituency Development Catalyst Fund) ambayo msingi wake ulilenga kuwawezesha wabunge kushiriki katika kusaidia miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi majimboni kwao.

Licha ya kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya utekelezaji wa sheria hii, nakumbuka Sitta alivyojitoa kimasomaso kuhakikisha umma unaelewa malengo ya sheria hiyo na hatimaye Bunge kuipitisha.

Katika matamshi yake kila siku, alitaka kuona Bunge lenye ‘meno’, Bunge lenye uwezo na ufanisi katika kutekeleza majukumu yake. Ni chini ya uongozi wake Bunge liliweza kupata Sheria ya Utawala wa Bunge mwaka 2008 iliyolipa madaraka ya uongozi kupitia Tume ya Utumishi wa Bunge, huku akipigania uanzishwaji wa Mfuko wa Bunge ili kuliwezesha Bunge kuwa na uwezo wake kifedha.

Pamoja na kwamba mapambano kwake ilikuwa sehemu ya maisha yake, naamini watumishi wa Bunge wengi watamkumbuka kwa mengi hasa alipopigania masilahi na mazingira bora ya utendaji kazi kwa watumishi wa Bunge.

Moja ya maono yake ni kuhakikisha kuwa Utumishi katika Bunge unakuwa wa mfano katika mihimili ya dola kutokana na changamoto wanazokumbana nazo watumishi wake za kufanya kazi katika mazingira ya kisiasa, jambo ambalo limeendelea kuasisiwa na kila Spika aliyeingia madarakani.

Kwa kuwa kwake ipo misamiati ambayo hakupenda kuisikia katika vinywa vya watendaji katika kufikia falsafa yake ya kasi na viwango kama vile maneno  ‘tunashughulikia’, ‘tuko kwenye mchakato’au ‘subiri tutakujibu’ aliweza kumpatia kitabu kiitwacho ‘Getting Things Done’ kila mtumishi aliyeonekana kuwa mzito kutekeleza majukumu yake kwa kasi.

Mara zote aliweza kutoa fursa kwa wanahabari kuzungumza naye na kubadilishana mawazo na hata kukosolewa katika mambo mbalimbali.

Uwezo wake wa kupokea changamoto na hata kukosolewa uliwavutia wengi hasa waliweza kutumia kalamu kuandika mapungufu yake ambapo pia alikuwa akiyafanyia kazi.

Hivi sasa licha ya jina la Sitta kubaki katika vitabu vya historia ya Bunge, bado matendo yake na maono yake tutaendelea kuyaishi na  kuyatekeleza. Uwezo wake wa kutambua mchango wa kila mtu katika mijadala uliweza kuvuta hisia na imani ya wananchi mbele ya umma.

Naamini katika uongozi wake katika Bunge la tisa, licha ya kulifanya Bunge kuwa na sauti, wadau wengi waliweza pia kutoa pongezi zao nyingi sana kutokana na mabadiliko makubwa aliyoyaanzisha ya kuboresha kanuni za Bunge kwa kushirikiana na Spika wa sasa, Job Ndugai.

Hakika, Bunge litamlilia daima Samuel Sitta, siku zote amekuwa kipenzi cha watu ndani na nje ya Bunge kupitia maneno yake yaliyosheheni utani na vibwagizo vyenye kuleta raha hata kwa waliokwazika katika mijadala bungeni.

Kifo chake umekuwa mwiba si tu kwa wabunge waliokuwa wakichota hekima zake pia hata kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakifuatilia baadhi ya maamuzi yake bungeni.

Kwa mara ya kwanza Bunge kupitia Kamati ya Uongozi chini ya Uenyekiti wa Spika wa Bunge wameweza kutengua kanuni na kuahirisha shughuli za Bunge kutoa fursa kwa wabunge kuomboleza kifo cha shujaa wetu na mpambanaji Samuel sitta.

Hakika hatua hii itabaki katika vitabu vya Bunge na busara za Spika Ndugai zitaendelea kuenziwa kizazi na kizazi.

Kwa heri Samuel sitta, tutaendelea kuenzi yale yote uliotuachia!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,224FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles